Featured Post

AAFP YASIFU KASI YA RAIS MAGUFULI



NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
CHAMA cha The Alliance African Farmers for Tanzania (AAFP ) kimesifu uamuzi wa Rais Dkt. John Magufuli kukutana na viongozi wastaafu wa serikali zote mbili na kuwataka watoe maoni, ushauri na mitazamo yao ni zaidi ya moyo wa chuma  huku akitaka nchi ifike mbali kimaendeleo.

Kimesema hatua hiyo licha ya kufungua milango na serikali ikitaka  kuchota maoni, ushauri na kuondosha baadhi ya kasoro pia imelenga kujenga haiba ya mapatano hivyo ni vyema pia akakutana na viongozi wa vyama vya siasa.
Ushauri huo umetolewa juzi na Mwenyekiti wa Taifa wa AAFP, Said Soud Said, huko Mombasa kwenye Ofisi za chama hicho akisema mkutano uliowakutanisha viongozi wastaafu wa serikali kwa sehemu kubwa utaondosha au kupunguza joto la mshawasha, sintofahamu na upekepeke.
Soud alisema, Rais Magufuli amewapa jukwaa la wazi wastaafu hao ili wafunguke kwa kutema nyongo, kushauri, kutoa maoni na mitazamo yao hivyo kama yupo aliyeogopa na baadaye atake kusema kwenye vibuyu, atakuwa hajafanya uungwana.
Alisema kikao kile kilikuwa na umuhimu wa pekee kwani kila kiongozi alipaswa kueleza kwa kadri anavyofikiri, kupendekeza, kushauri lakini pia kukosoa iwapo zipo hitilafu na dosari za kiutawala zinazaoonekana kuchomoza au kwenda ndivyo sivyo.
"AAFP inasifu uamuzi wa Dkt. Magufuli kukutana na viongozi wastaafu wa serikali zote mbili. Ameunda jukwaa la wazi akiwataka wafunguke. Ameonyesha ujasiri na uwazi wa serikali yake kupokea maoni. Ipo haja sasa akakutana na viongozi wa vyama vya siasa," alisema Soud.
Aidha, Mwenyekiti huyo alisema Rais Magufuli amesifu misingi iliyowekwa na watangulizi wake katika ujenzi wa nchi, hivyo akataka apate ushauri mpya iwapo ndani ya miaka yake miwili na ushee akiwa madarakani kama kuna dosari na hitilafu ili serikali yake ijiweke sawa.
"Hakuna mtawala Kusini mwa Afrika aliyethubutu kuitisha kikao kama kile. Amekuwa na moyo wa chuma akitaka kukusanya mawazo ya pamoja katika ujenzi wa nchi. Kama yupo kiongozi mstaafu aliyeshindwa kushauri lolote au kukosoa, huyo hakutimiza wajibu wake," alieleza.
Alisema ingawaje katika mkutano na viongozi wa vyama vya siasa atakabiliana na wapinzani wake kisera, vyama pinzani vina wajibu wa kujenga indhar ya ushauri wenye nguvu ya hoja badala ya propaganda kwani Rais aliye madarakani muda wake wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi haujamalizika.
"Kiwe ni kikao cha ushauri na ukusanyaji maoni kisiwe cha malumbano wala mipasho ya kisiasa. Yatupasa wote tujiandae kimkakati kushauri na kama zipo dosari zinazohitaji makemeo ya kisiasa, vyama visubiri mwaka 2020 au watumie kampeni za chaguzi ndogo za katika majimbo ya Jang'ombe na Buhingwe," alieleza.
Pia Mwenyekiti huyo wa AAFP alisema kitendo cha kuwaita watangulizi wake akiwataka watoe mitazamo na fikara zao ni katika namna ya mbinu za kiongozi kutaka aidha kujipima, kujisahihisha na kujipanga zaidi ili Taifa liwe na mshikamano badala ya kuishi kwa mivutano isio na tija.
"Ikiwa vitendo vya ufisadi, rushwa na maonevu vinazidi kupungua, wafanyakazi kwenye taasisi za umma wanatoa huduma kwa nidhamu, Serikali inakusanya kodi huku huduma za jamii zikiboreshwa, lazima anayeshauri awe na mawazo mbadala na si porojo," alisisitiza.
Hata hivyo, Soud alisema viongozi wastaafu walioitwa kushiriki kikao kile ni wakongwe na wabobezi katika medani za siasa, utawala na uongozi,  hivyo ushauri wote waliotoa mbele ya Rais bila shaka utachukuliwa na serikali kwa umuhimu na kupewa kipaumbele.


Comments