Featured Post

USHIRIKA NGUZO YA MAENDELEO YA KILIMO, UHAKIKA WA CHAKULA



NA ALOYCE NDELEIO
UMUHIMU wa vyama vya ushirika katika kuboresha maisha ya mamilioni ya wakulima wadogo na familia zao hauwezi ukapingika kwani umewawezesha kujiunga na kuunda kundi kubwa linaloweza kujadiliana katika suala zima la uzalishaji endelevu.

Hatua hiyo ndio inaoufanya ushirika kuitwa kuwa ni ushirika ni fimbo ya mnyonge. 
Vyama vya ushirika kuanzia vyama vidogo hadi vikubwa vyenye mitaji ya mamilioni ya fedha duniani vimekuwa vinaendeshwa kwenye sekta zote za uchumi.
Vimekuwa vinahesabika kuwa vina zaidi ya wanachama milioni 800 na vinamudu kutoa fursa za ajira milioni 100 kiwango ambacho ni zaidi ya asilimia 20 ya  fursa zinazotolewa na makampuni ya kimataifa.
Kutokana na hali hiyo wakulima wadogo wanaweza kuishi maisha endelevu, kuboresha uhakika wa chakula ndani ya jumuia zao  na kutoa mchango mkubwa katika ongezeko la mahitaji ya chakula kwenye masoko ya ndani, kitaifa na kimataifa.

Mkombozi wa maskini
Katika warsha ya uwezeshaji wa vyama vya ushirika vya ngazi za chini, iliyoandaliwa hivi karibuni na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET), Dar es Salaam, mmoja wa wataalam na mwanataaluma wa masuala ya ushirika Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, mstaafu Profesa Suleiman Chambo, alisema, vyama vya ushirika pekee ndivyo vyenye uwezo wa kufika sehemu za vijijini tofauti na taasisi nyingine za fedha.
Profesa Chambo alisema kutokana na vyama vya ushirika kuwa nguzo muhimu vijijini, ingekuwa vyema serikali kuangalia uwezekano wa kuvifufua upya vyama hivyo ili wananchi waishio vijijini waweze kutoa mawazo yao badala ya kuwatilia mkazo kutumia njia za taasisi nyingine.
Mwanataaluma huyo alisema iwapo ushirika utatiliwa mkazo katika mikoa mbalimbali, hususani maeneo ya vijijini, utafufua uchumi wa taifa kutokana na maeneo hayo kuwa na idadi kubwa ya wakulima ambao hawajui ni wapi wanaweza kuwekeza.
Si jambo lililofichika kuwa wakati wa uhai wa vyama vya ushirika wanachama waliweza kupata huduma za viwango vya juu hususan katika suala la masoko ya mazao yao na hivyo kuwa nguzo yao ya karibu zaidi kuliko vyombo vingine.
Kwa kiwango kikubwa vyombo hivyo vilikuwa ni  swahiba mkubwa wa wakulima hasa waliojishughulisha na kilimo cha mazao ya biashara kama vile kahawa na pamba na si siri kuwa neema ilikuwa inawashukia.
Pamoja na hali hiyo, vyama hivyo katika miaka ya hivi karibuni vimepitia katika kipindi kigumu kutokana na ubadhirifu uliofanywa na baadhi ya  walafi wachache ambao kwa kiasi kikubwa walivihujumu.
Profesa Chambo alibainisha kuwa ushirika umezorota kwa sasa kutokana na kuingiliwa na masuala ya siasa, hivyo kuvifanya vyama hivyo kushindwa kujitawala kama ilivyokuwa awali.
Hapa jambo linalojiweka wazi ni kwamba masuala ya siasa yalivizorotesha vyama vya ushirika kutokana na siasa zenyewe kujikita mno ndani ya vyama hivyo na masuala hayo kuupa kisogo mchango uliokuwa umetolewa navyo katika wakati wa mapambano ya kutafuta uhuru wa Tanganyika.

Ushirika ulichangia kudai uhuru
Haiyumkiniki kuwa mchango wa vyama hivyo katika mapambano ya kupatikana uhuru wa Tanganyika ni mkubwa na kwamba ni moja ya silaha iliyotumiwa na waasisi wa Chama cha TANU kuwaunganisha wananchi.
Kwa wafutaliaji wa masuala ya historia ya mapambano ya uhuru, hakuna atakayebeza mchango uliotolewa na Shirikisho la Vyama vya Ushirika  Kanda ya Ziwa (Victoria Federation of Cooperative Unions (VFCU) chini ya uongozi wa Hayati Paulo Bomani.
Aidha, ni kupitia ushirika huo, Chama cha TANU, kiliweza kuzoa wanachama wengi katika kanda hiyo na hivyo kukiongezea nguvu katika harakati zake za kuikomboa Tanganyika.
Ni wazi kuwa haikuwapo njia nyingine rahisi ya kuwafikia watu walioishi ndani vijijini na kuwawezesha kupokea sera zilizokuwa zinasambazwa na TANU, tena kwa siri kama si ushirika huo.
Kwa vyovyote vile kufufua vyama hivyo itakuwa ni kuendeleza historia na kuthamini mchango wake katika kumkomboa mwanajamii wa leo ambaye anajivunia kuwepo kwa Tanzania huru.
Vyama vya ushirika havikuishia kwenye utando wa kusukuma mbele mapambano ya kupatia uhuru bali pia viliangalia nyanja ya uchumi na uwezeshwaji wa wanachama wake kwa njia ya mikopo.
Kwa vyovyote vile, ndivyo vilikuwa vyanzo vya awali vya kutoa mikopo miongoni mwa wakulima waliokuwa wanachama wake, ikiwa ni njia moja ya kuhakikisha kuwa uzalishaji wa mazao yao unakuwa endelevu kwa upande mmoja na kwa upande mwingine wakiwa wanakidhi mahitaji yao muhimu ya maisha.
Miongoni mwa vyama vya ushirika vikongwe barani Afrika na ambacho ni cha kujivunia leo hii hapa nchini ni Chama cha Ushirika cha Wazawa Kilimanjaro (Kilimanjaro Native Cooperative Union (KNCU)), ambacho kimekuwa kinashughulika na wakulima wa zao la kahawa aina ya Arabica.
Kikiwa kimeanzishwa mwaka 1924 pamoja na vyama vingine vya ushirika, vilivunjwa mwaka 1976 lakini mwaka 1984 vilianzishwa tena na hivi sasa KNCU ina vyama vya msingi 90.
Aidha, chama hicho kilipata tuzo ya uthibitisho wa kushiriki ya Shirika la Maonyesho ya Biashara (FLO) mwaka 1993. Lakini muhimu ni kwamba wanachama wamekuwa wanashiriki katika kuchagua viongozi wa chama kwa njia ya kidemokrasia na kuwa na wawakilishi kutoka kila chama cha msingi.
Kikiwa ni chama kilichojizatiti, kilianzisha mfuko wa elimu ambao wanachama wake wamekuwa wanachangia kwa hiari na umetumika kujenga na kuendesha shule kwa ajili ya watoto wa wakulima na hata kulipia baadhi ya watoto wa wakulima wa zao hilo ada za masomo yao.
Moja ya shule zilizojengwa na kusimamiwa na KNCU ni Shule ya Sekondari ya Lyamungo, ambayo ni moja ya shule kongwe hapa nchini.
Haiyumkini Profesa Chambo pia aliguswa na hali kwamba chuo kikuu hicho ambacho yeye alikuwa ni mkuu wake ni moja ya matunda ya kazi za Chama cha Ushirika cha KNCU.
Hadi miaka ya hivi karibuni kabla ya kuingia kwa soko huria na kampuni za watu binafsi kuanza kununua zao hilo wanachama wake walikuwa wameridhia kukatwa kiasi fulani cha fedha kwa kila kilo moja ya kahawa waliyouza kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa shule mbalimbali za sekondari mkoani humo.
Makato ya fedha hizo pale ilipotokea kuwa shule inayochangiwa ipo katika kata ambayo ndani yake kuna chama cha msingi cha ushirika hayakuwa na ubishi bali yalikuwa ni jambo lisilopingika.
Hali hiyo ikawa ni mvuto kwa vyama vingine vya msingi kuchangia shule na hivyo kuwa moja ya sababu zilizochangia kupanuka kwa elimu mkoani humo.
Kutokana na kuingia kwa kampuni na watu binafsi katika ununuzi wa zao hilo, basi michango iliyokuwa inapatikana kwa ajili ya maendeleo ya ujenzi wa shule hizo nayo ikawa imefikia ukomo kama si kifo.
Chama hicho pia kina Benki ya Ushirika Kilimanjaro (Kilimanjaro Cooperative Bank (KCB) ambayo imewezesha wakulima kupata mikopo kutoka kwenye huduma ya kuweka na kukopa.
Hata hivyo licha ya kufikia kiwango cha kuanzisha benki, ni vyema kuangalia ni vipi ushirika ulikuwa karibu na mkulima wa kijijini katika kumwezesha kupata mikopo.
Awali ilikuwa ni rahisi kufanya sensa ya miche ya kahawa ambayo mkulima alikuwa nayo na ilikuwa rahisi kufanya makadirio ya mazao atakayovuna kwa msimu.
Takwimu hizo zilitumika katika kutoa mikopo, na kwa hali hiyo amana aliyokuwa nayo mkulima ilikuwa tayari imeshafanyiwa tathmini.
Aidha, mikopo mingine ilikuwa ni endelevu kwa sababu ilimzalishia mkulima. Mfano mkulima aliweza kupata mkopo wa ng’ombe wa maziwa na gharama yake akawa anailipa kwa kukatwa kwenye mauzo ya kahawa taratibu na alipomaliza aliweza kuomba mkopo mwingine kwa ajili ya shughuli nyingine.
Kwa namna moja au nyingine, ni dhahiri kuwa vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) vilikuwa tayari vimo ndani ya Chama cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU).
Ni dhahiri kuwa amana aliyonayo mkulima ni mazao anayolima na hiyo ndiyo ilikuwa inamwezesha kupata mikopo kutoka kwenye chama chake cha ushirika ambacho ndicho kinafahamu fika hali ya uzalishaji ndani ya amana yake.
Kwa maana hiyo taasisi nyingine za fedha si rahisi kufikia misingi hiyo, kwa kuwa zenyewe zinaweza zisione amana kama dhamana zitazowawezesha wakulima kupatiwa mikopo.

Comments