Featured Post

RC MWANRI AWASHUKI WANAOWATUMIKISHA WATOTO



MKOA wa Tabora umedhamiria na kuweka mikakati ya kupambana kuhakikisha unaondokana na utumikishwaji wa watoto unaosababisha utoro shuleni, mimba na ndoa za utotoni.

Matukio hayo ndiyo yanayodaiwa kusababisha mkoa huo kuongoza kwa utoro kitaifa na hivyo kupoteza dira ya watoto hao.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, alieleza hayo juzi wakati akifungua rasmi warsha ya Mkakati wa Taifa wa kutokomeza utumikishwaji wa watoto nchini iliyoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kushirikiana na asasi ya ARISE ya mjini hapa kwenye ukumbi wa Georges Complex uliopo Kata ya Cheyo A mjini hapa.
Mwanri alisema kuwa, mkoa huo umedhamiria kuondokana na utumikishwaji wa watoto kwa kuorodhesha majina ya watoto wote wanaotumikishwa, watoro, wenye mimba na walioolewa ikiwa ni pamoja na majina ya wazazi ama walezi wao ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika wote.
Alieleza kuwa, amewaagiza viongozi na watendaji wote kuanzia ngazi ya vijiji, vitongoji, kata na wilaya zote kuorodhesha majina yote ya walengwa na kuyapeleka ofisini kwake na yeye atamkabidhi Kamanda wa Polisi (RPC) mkoani humo, ambaye atawakabidhi wakuu wa polisi wa wilaya zote ili kuwakamata wahusika wote na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
 “Haiwezekani mkoa huu uwe unaongoza kwa matukio mabaya tu, utumikishwaji wa watoto, utoro, mimba na ndoa za utotoni, mauaji ya watu kwa imani potofu za kishirikina, yote haya tunaongoza wakati viongozi tupo na wahusika wanafahamika.
"Nasema sasa basi na hakuna jiwe litakalobakia juu ya jiwe na nitahakikisha Tabora inaondokana na yote hayo na kuwa Taa Bora na itabakia historia,” alieleza mkuu huyo wa mkoa.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Dayosisi mpya ya Magharibi na Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Isaack Leizer Kissiri, akitoa salamu zake kwa niaba ya  madhehebu yote, alieleza kuwa, wao kama watumishi wa Mungu watafundisha kwa vitendo na kusimamia msimamo wa serikali katika kutokomeza utumikishwaji wa watoto nchini.
Askofu Kissiri alisema kuwa, watapambana kutoa elimu kwa waumini wao na jamii nzima na kuhakikisha wanapatikana raia wema wenye maadili yanayoendana na Taifa pamoja na kuiunga mkono serikali kuhakikisha inaboresha maisha ya wananchi na serikali kwa ujumla.
Naye Kamishna Msaidizi wa Kazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu), Hawa Wenga, alisema serikali itaandaa sera na sheria kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kupingana na utuimikishwaji wa watoto nchini.
Wenga alisema kwamba, serikali itaendelea kushirikiana na asasi mbalimbali katika kupambana na utumikishwaji huo wa watoto na kuhakikisha kunakuwapo na kizazi salama chenye afya bora kama ilivyo kauli mbiu ya Taifa ya siku hiyo ya kupinga utumikishwaji huo.
Mratibu wa Taifa wa asasi yenye mradi wa kutokomeza utumikishwaji wa watoto katika jamii ya wakulima wa tumbaku mkoani Tabora (ARISE), Dkt. Gerson Nyadzi, alisema kuwa mradi huo unatekelezwa katika wilaya za Uyui na Urambo mkoani humo tangu Julai 2016 ambapo wameweza kuwaibua zaidi ya watoto 94 waliokutwa wakitumikishwa katika mashamba ya tumbaku.
Dkt. Nyadzi alisema, kati ya watoto hao, wa kiume ni 61 na wa kike ni 33 wanatoka katika Kijiji cha Migungumalo, Kata ya Usagali, Wilaya ya Uyui mkoani hapa ambacho kinakadiriwa kuwa na watoto 1,145 wakiwemo wasichana 582 na wavulana 563, kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Azizi Makungu.
Alisema, asasi hiyo imeweza kuwaelimisha wazazi na walezi wa watoto hao pamoja na watoto wenyewe na baadhi yao wamerejea shuleni, wengine wamepatiwa elimu ya ujasiriamali wa kutengeneza bidhaa mbalimbali kama batiki na sabuni za maji kupitia asasi ya JIDA na wengine watapatiwa mifugo ya kuku, mbuzi na nguruwe ili familia zao ziwafuge hadi watoto hao watakapofikisha umri wa kujitegemea ndipo watakabidhiwa ili kujikomboa kiuchumi.


Comments