Featured Post

KOMBE LA DUNIA 2018: NANI ATAIBUKA BINGWA URUSI?



MOSCOW, RUSSIA
KUNA mataifa 32 yanayoshiriki Kombe la Dunia, lakini mshindi atakuwa mmoja. Je, unawezaje kubashiri nani atainua Kombe la Dunia mjini Moscow 15 Julai?

Kwa kuangalia mtindo, takwimu na yaliyotokea katika mashindano ya awali, BBC Sport imeondoa mataifa 31 na kusalia na taifa moja ambalo kwa mujibu wa vigezo hivyo ina nafasi kubwa zaidi ya kuwa mabingwa wa dunia.
Hapa kuna mambo ambayo mshindi wa Kombe la Dunia wa mwaka 2018 anafaa kutimiza:

Awe wa kwanza kwenye chungu
Tangu Kombe la Dunia lilipopanuliwa na kuwa na timu 32 mwaka 1998, mabingwa wote walikuwa ni taifa ambalo lilikuwa la kwanza kwenye chungu wakati wa kufanyika kwa droo.
Timu ya mwisho kushinda bila kuwa kwenye chungu ilikuwa ni mwaka 1986 Argentna waliposhinda wakiwa na Diego Maradona na bao lake la 'mkono wa Mungu'. Kwa kutumia kigezo hicho, tumeondoa mataifa 24 ambayo yanashiriki mashindano hayo mwaka huu, na kusalia na timu nane.

Usiwe mwenyeji
Urusi imefaidika kushiriki michuano hiyo kwa sababu ya kuwa taifa mwenyeji.
Kumekuwa na utaratibu kwamba taifa mwenyeji lazima liwe kwenye chungu. Hilo limekuwepo kwa miaka 44.
Lakini ukizingatia kwamba nafasi yao kwenye orodha ya viwango vya soka duniani ya Fifa ni 66, hawangekuwa miongoni mwa nchi hizo nane za kuwekwa kwenye chungu kama hawangekuwa wenyeji.
Kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia siku hizi pia si hakikisho kwamba utafanya vyema kama ilivyokuwa zamani.
Katika makala 11 ya michuano hiyo, 1930 hadi 1978, mara tano mwenyeji ndiye aliyeshinda.
Tangu wakati huo, katika michuano tisa iliyochezwa karibuni mwenyeji alishinda mara moja pekee - Ufaransa 1998.
Ingawa ni kweli hakukuwa na matarajio yoyote kwamba Marekani, Japan, Korea Kusini au Afrika Kusini wangeshinda Kombe la Dunia, Italia mwaka 1990, Ujerumani mwaka 2006 na Brazil miaka minne iliyopita ni mataifa ambayo yalitarajiwa kushinda wakiwa wenyeji. Lakini hawakufanikiwa.

Usifungwe mabao mengi
Katika enzi hii ya timu 32, mabingwa wote watano hawajafungwa zaidi ya magoli manne katika mechi saba walizocheza.
Ukiangalia timu saba tulizosalia nazo, Poland ndio walio na safu ya ulinzi hafifu zaidi ukiangalia mechi zao za kufuzu, walifungwa bao 1.4 kwa kila mechi.
Ujerumani na Ureno walifungwa 0.4 kila mechi, Ubelgiji na Ufaransa 0.6, Brazil 0.61 na Argentina 0.88.

Uwe kutoka Ulaya
Washindi wa Kombe la Dunia kufikia sasa wote wametokea Ulaya na Amerika Kusini. Hadi miaka ya karibuni, timu za Ulaya zilikuwa hazisafiri mbali kwa mechi hizo. Lakini ufanisi wa Uhispania nchini Afrika Kusini na Ujerumani nchini Brazil umeonesha kwamba wanafanikiwa hata wakisafiri mbali.
Michuano inayoandaliwa Ulaya, hata hivyo, mara nyingi hushindwa na wenyeji. Kati ya michuano 10 iliyoandaliwa na nchi kutoka Ulaya, ni moja pekee ambayo mshindi alikuwa wa kutoka nje.
Na inakulazimu kurudi nyuma hadi mwaka 1958 Brazil waliposhinda michuano iliyoandaliwa Sweden.

Kuwa na kipa bora zaidi
Unaweza ukafikiria kwamba wafungaji mabao ndio husaidia mataifa kushinda Kombe la Dunia, lakini ni mara mbili pekee tangu 1982 ambapo mshindi alikuwa na mfungaji mabao bora.
Mwaka 2002 Brazil iliposhinda ikiwa na Ronaldo na David Villa na Uhispania mwaka 2010.
Washindi wa Kombe la Dunia zaidi husaidiwa na walinda lango wao.
Washindi mara nne kati ya tano wa kipa bora wa michuano walikuwa magolikipa wa timu ambayo iliibuka mshindi mwishowe.
Kati ya mataifa manne yaliyosalia, si vigumu kufikiria mmoja kati ya Manuel Neuer (Ujerumani), Hugo Lloris (Ufaransa) au Thibaut Courtois (Ubelgiji) akitawazwa kipa bora zaidi wakati huu.

Uwe na uzoefu
Mataifa yaliyoshinda Kombe la Dunia yamekuwa na wachezaji ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa na uzoefu. Ni mtindo ulioanza michuano hii ilipopanuliwa na kuwa na timu 32 mwaka 1998.
Wakati huo, mabingwa Ufaransa walikuwa na kikosi cha wachezaji ambao kwa wastani walikuwa wamechezea taifa mechi 22.77 kwa wastani.
Miaka minne iliyopita, mabingwa Ujerumani walikuwa na uzoefu wa mechi 42.21.
Hapo katikati kulikuwa na kuimarika pakubwa.
Brazil wachezaji wake walikuwa wamecheza kwa wastani mechi 28.04 mwaka 2002, Italia 32.91 mwaka 2006 na Uhispania 38.30 mwaka 2010.
Mataifa matatu tuliyobaki nayo yalipotangaza wachezaji wake, Ufaransa uzoefu wa wastani wachezaji wake ni mechi 24.56, Ujerumani 43.26 na Ubelgiji 45.13.

Usiwe bingwa mtetezi
Kombe la Dunia huwa ngumu sana kutetea. Haijatokea tangu Brazil walipofanikiwa kutetea taji hilo kwa kushinda 1958 na 1962 ambapo taifa limeshinda mara mbili mfululizo.
Kusema kweli, tangu wakati huo wa Brazil, mabingwa watetezi 13 ambao wamekuwepo walipita nusu fainali mara mbili pekee.
Argentina mwaka 1990 na Brazil mwaka 1998, ingawa Brazil walimaliza wa nne mwaka 1974 mpangilio ulipokuwa wa hatua mbili za makundi na kisha fainali.
Katika michuano minne iliyopita, mabingwa watetezi waliondolewa hatua ya makundi mara tatu.
Ujerumani wamefanikiwa sana Kombe la Dunia miaka ya karibuni.
Katika michuano tisa iliyoandaliwa karibuni - ikiwemo mitatu wakiwa Ujerumani magharibi - wameshinda mara mbili, wakafika fainali mara nyingine tatu na wakamaliza nafasi ya tatu mara nyingine mbili.
Hata hivyo, ukiangalia uwezekano wao wa kushinda tena Urusi, historia haipo nao.
Kwa hivyo, tuko hapo sasa. Ubelgiji watashinda Kombe la Dunia. Taifa jingine lisiposhinda. Jambo ambalo linawezekana.


Comments