Featured Post

HII NI BAJETI YA KULINDA NA KUOKOA VIWANDA VYA NDANI 2018/2019



NA WAANDISHI WETU
SERIKALI imewasilisha Makadirio ya Bajeti ya Shilingi trilioni 32.48 kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 yenye vipaumbele vikubwa vinne huku ikilenga kulinda viwanda vya ndani kwa kutopandisha ushuru wa baadhi ya bidhaa.

Mbali ya kutopandisha ushuru wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani, Serikali pia imefuta baadhi ya ushuru, ukiwemo wa taulo za kike, lengo likiwa kulinda afya za wanawake na wasichana.
Akiwasilisha makadirio hayo bungeni jijini Dodoma jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alisema bajeti ya matumizi katika mwaka 2018/19 itaweka mkazo zaidi katika uendelezaji wa miradi ya kielelezo, kufungamanisha maendeleo ya watu, na ujenzi wa mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji na uendeshaji biashara.
Alisema kwamba, Serikali imeyaangazia maeneo manne ya kipaumbele - kilimo, viwanda, huduma za jamii, na miundombinu wezeshi - ambayo wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema, bajeti hiyo inaendana na azma ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Kuhusu kilimo, Dkt. Mpango alisema kwamba, fedha zitaelekezwa zaidi kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, maghala na masoko, kuimarisha upatikanaji wa  pembejeo na zana za kilimo, kupanua huduma za ugani, kuboresha mfumo wa utafiti na utoaji wa matokeo ya utafiti kwa wananchi, na uendelezaji wa sekta ndogo za uvuvi na mifugo.
"Mkazo umewekwa katika sekta hii kwa kuzingatia kuwa inategemewa na wananchi wengi na ndiyo itakayotupatia malighafi kwa ajili ya viwanda, kutuhakikishia usalama wa chakula na kuongezeka kwa kipato cha wananchi," alisema.
Aidha, alisema, katika kuchochea ukuaji wa viwanda nchini, Serikali itaelekeza nguvu zake kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi hususan viwanda vya nguo, ngozi na nyama, samaki, mafuta ya kula, madawa na vifaa tiba, vyakula vya binadamu na mifugo, na katika sekta ya madini.
Katika huduma za jamii, bajeti hiyo imelenga maeneo ya maji, elimu na afya.
"Eneo lingine muhimu ni kuongeza upatikanaji na usambazaji wa maji safi hasa vijijini na uondoshaji wa majitaka, uchimbaji wa visima katika maeneo kame nchini na ujenzi wa mabwawa makubwa ya kimkakati.  
"Serikali itaendelea kugharamia elimu msingi bila ada, kuongeza idadi ya wataalam katika fani adimu kwenye maeneo ya madini, mafuta na gesi, madaktari bingwa (moyo na figo) pamoja na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu," alisema.
Kuhusu afya, Dkt. Mpango alisema, rasilimali fedha zitaelekezwa kuongeza usambazaji wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na uboreshaji wa huduma katika vituo vya afya, zahanati na hospitali za rufaa.
Aidha, alisema, Serikali itaelekeza fedha zaidi za LGCD kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri, hususan miradi ya elimu na afya.
"Serikali itaweka msukumo kuimarisha upatikanaji wa lishe bora kwa mama na mtoto hususan katika siku 1,000 za mtoto tangu kutungwa kwa mimba ili kuondokana na changamoto ya kuwa na watoto wenye udumavu na hivyo kukua vema kimwili na kiakili.
"Aidha, mahitaji ya makundi maalum katika jamii yetu (wanawake, vijana, watoto, watu wenye ulemavu na wazee) yataendelea kuangaliwa kipekee," alisema.
Bajeti hiyo pia inalenga kujenga na kukarabati miundombinu wezeshi hususan kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali, kuendelea na ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge), ujenzi wa barabara za kuunganisha mikoa na zile za vijijini, na kuimarisha usafiri wa anga na majini.
Alisema maeneo mengine ya kipaumbele ni kurahisisha umiliki wa ardhi,  kuimarisha huduma za mawasiliano,  kifedha na utalii na kuimarisha ulinzi, usalama, utawala bora, na utoaji haki.

Ushuru wa Bidhaa
Waziri Mpango alisema kwamba, kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Kifungu cha 124(2), marekebisho ya viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa (specific duty rates) zisizo za petroli yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla.
Hata hivyo, alisema, ili kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda, imependekezwa kutofanya mabadiliko ya viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa zisizo za petroli zinazozalishwa nchini na kuongeza viwango vya Ushuru wa Bidhaa zisizo za petroli zinazoagizwa kutoka nje.
Alisema, Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji baridi utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 61 kwa lita.
"Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa yaliyoagizwa kutoka nje utaongezeka kutoka shilingi 61 kwa lita hadi shilingi 64.05 kwa lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye maji yanayozalishwa hapa nchini utaendelea kutozwa kwa kiwango cha  sasa cha shilingi 58 kwa lita," alisema.
Alisema kwamba, Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa nchini (local juices) hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 9 kwa lita.
Hata hivyo, Ushuru wa Bidhaa kwenye juisi zilizotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi nchini (imported juices) utaongezeka kutoka shilingi 221 hadi shilingi 232 kwa lita.
Ushuru wa Bidhaa kwenye bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 450 kwa lita, wakati bia zinazoagizwa kutoka nje zitatozwa shilingi 803.25 badala ya shilingi 765 kwa lita.
"Ushuru wa Bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu vinavyoagizwa kutoka nje utaongezeka kutoka shilingi 561 hadi shilingi 589.05 kwa lita, na bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu vinavyozalishwa nchini utaendelea kutozwa kwa kiwango cha sasa cha shilingi 561 kwa lita," alisema Waziri Mpango.
Dkt. Mpango alisema, Serikali itaanzisha Ushuru wa Bidhaa wa shilingi 200 kwa lita kwenye mvinyo uliotengenezwa kutokana na usindikaji wa matunda (kama ndizi, rozela/choya, nyanya, nk) yanayozalishwa hapa nchini tofauti na zabibu kwa kiwango kinachozidi asilimia 75.
Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 200 kwa lita, wakati ambapo kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, utaongezeka kutoka shilingi 2,349 hadi shilingi 2,466 kwa lita.
Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje utaongezeka kutoka shilingi 3,481 hadi shilingi 3,655.05 kwa lita, na Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyozalishwa nchini hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 3,315 kwa lita.
Kwa upande mwingine, Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 12,447 kwa kila sigara elfu moja.
Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 29,425 kwa kila sigara elfu moja.
"Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zenye sifa tofauti na hizo zilizotajwa juu utaongezeka kutoka shilingi 53,235 hadi shilingi 55,896.75 kwa kila sigara elfu moja ikiwa ni ongezeko la shilingi 2,661.75 kwa kila sigara elfu moja.
"Ushuru wa Bidhaa kwenye tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) inayoagizwa kutoka nje utaongezeka kutoka shilingi 26,888 hadi shilingi 28,232.4 kwa kilo, ikiwa ni ongezeko la shilingi 1,344.4 kwa kilo; na Ushuru wa Bidhaa wa ‘cigar’ unabaki kuwa asilimia 30," alisema.


Comments