Featured Post

HATIMILIKI ZA KIMILA 747 KUTOLEWA HALMASHAURI YA WILAYA YA MUFINDI

Evance Kibasa Mwananchi kutoka kijiji cha Usokame akiwa na Hatimiliki yake ya kimila baada ya kukabidhiwa.
Mmoja wa wananchi toka kijiji cha Usokame akikabidhiwa hatimiliki ya kimila na Afisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi Simon Mbago
Asafu Mgelekwa na Mkewe Atuganule Lunyungu wakiwa na hati yao yenye umiliki wa pamoja
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ugesa wakiwa na hatimiliki zao za kimila
Simon Mbago Afisa Ardhi Mufindi akimsaidia mwananchi kuweka saini kwenye fomu kama uthibitisho ya kuwa amepokea hati.

Shirika la PELUM Tanzania kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imeanza zoezi la kutoa hatimiliki za kimila zipatazo 747 kwa wananchi wa vijiji vitano ambao wamefanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi kupitia mradi wa ushiriki wa wananchi katika kusimamia sekta ya kilimo ulio chini ya watu wa marekani

Hatimiliki hizo zinatarajia kunufaisha wanawake 250, wanaume 385, wenza wenye ushiriki wa pamoja 97 pamoja na maeneo ya Taasisis 97 toka vijiji vya Usokame, Ugesa, Magunguli, Isaula na Makungu

Simon Mbago Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Mufindi anayesimamia zoezi hili, mbali na kulishukuru Shirika la PELUM Tanzania kwa kufanya nao kazi kwenye vijiji hivyo amesema kufanyika kwa mpango wa matumzi ya ardhi hadi kufikia utoaji wa hatimiliki imesaidia kutekeleza majukumu ya Halmashauri ambayo yalipaswa kutekelezwa na Halmashauri husika.

“Ni jukumu la kila Halmshauri kuhakikisha inatenga fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo ili kufanyia vijiji vyake mpango wa matumizi ya ardhi lakini uwepo wa mashirika binafsi kutekeleza jukumu hili ikiwemo PELUM Tanzania imesaidia kwa kiwango kikubwa kuchochochea maendeleo katika Halmashauri yetu.”

Hivyo basi uwepo wa hatimiliki hizi tunazogawa zitasaidia wananchi wa Halmashauri yetu kuzitumia kuomba mikopo kwenye taasisi za fedha kwa kuweka dhamana maeneo yao jambo ambalo wamekuwa wakilisubiri kwa kipindi kirefu ili kuwawezesha kufanya shughuli nyingine za kiuchumi kupita fedha watakazopata.

Mbali na hilo, Mbago amesema pia zoezi hili si tu limesaidia kupunguza migogoro ya ardhi kwenye vijiji husika lakini pia limesaidia kwa kiwango kikubwa kubaini kuwa wapo wananchi ambao maeneo yao ya muda mrefu ambayo yamepimwa kupitia mradi huu hayapo kwenye Wilaya ya Mufindi bali yapo kwenye wilaya ya Kilolo na hivyo kupunguza idadi ya hatimiliki walizopaswa kupewa wananchi jambo ambalo pia limesaidia kuzuia uwepo wa migogoro ya ardhi baina ya wananchi walipo mpakani mwa wilaya ya Mufindi na Kilolo.

Evance Kibasa ni mwananchi wa kijiji cha Usokame ambaye eneo lake lilipimwa anasema hatimiliki ya kimila aliyokabidhiwa sio tu itamsaidia kupata mkopo kwenye taasisi za fedha na kuweza kutanua biashara zake kama njia ya kujiongezea kipato zaidi bali pia imemuhakikishia ulinzi halali na wa kisheria wa eneo lake kijijini hapo.

Naye Asafu Mgelekwa ambaye amekabidhiwa hatimiliki ya umiliki wa pamoja na mwenza wake Atuganile Lunyungu amesema anashukuru kwa zoezi hili kukamilika na sasa ana uhakika hata akitangulia mbele ya haki amemuacha mke wake kwenye mikono salama kutokana na kuwepo kwa migogoro mingi ya kifamilia baada ya mume kufariki, mke hunyang’anywa mali zote na familia ya mume.

Kaimu mtendaji wa kijiji cha Ugesa Malianusi Mdalingwa amesema, awali wakati zoezi la upimaji maeneo likiendelea wapo wananchi wengi waliobeza zoezi hilo na kusema maeneo yao yanaporwa ila baada ya kuona wenzao wanahakiki taarifa zao na sasa wamepata hatimiliki za kimila wanarudi ofisini wakiomba wapimiwe maeneo yao.

“Awali walibeza sana zoezi hili na kutucheka kuwa PELUM Tanzania kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mufindi wana lengo la kutudhulumu maeneo yetu na walitushawishi tuachane na mafunzo tunayopewa ila baada ya kuona zoezi linakamilika kila mtu anakuja ofisini akilalamika naye anataka apimiwe eneo lake ila baada ya kuwaambia kwa sasa itawapasa watumie gharama zao kidogo tofauti na sisi wa awali bado wanaona kama wanaonewa”.

Kupitia changamoto hiyo, Mdalingwa ameomba Shirika la PELUM Tanzania kurudi tena kijijini hapo kuwapimia wananchi waliobaki kama watafamikiwa kupata mradi wingine.

Santina Mdalingwa yeye ni mjane, anasema wakati wa mafunzo na zoezi la upimaji maeneo likiendelea, aliwashauri ndugu wa mume wake wapime eneo la nyumba ambayo alitafuta na mume wake, ila kutokana na ndugu kuona atanufaika walimkatalia kupima eneo hilo na hivyo kuamua kwenda kupima shamba lake la miti leye ukubwa wa hekari moja alilopewa na baba yake. Kwa sasa anasema hatimiliki aiyoipata ni ulinzi tosha wa eneo lake hakuna atakayemdhulumu ikiwemo ndugu aliozaliwa nao.

Kupitia zoezi hilo endelevu, Simon Mbago amebainisha kuwa kati ya vijiji 121 vilivyo Halmashauri ya wilaya ya Mufindi ni vijiji 50 tu ambavyo wananchi wake wanamiliki ardhi kwa hati hivyo ameliomba Shirika la PELUM Tanzania kurudi tena katika Halmashari hiyo kuendelea kufanya kazi nao kama watapata mradi mwingine lengo ni kuwawezesha wananchi wote wawe na umiliki halali wa kishera wa ardhi zao. 

Comments