Featured Post

WAJAWAZITO WATAKIWA KUHUDHURIA KLINIKI MARA KWA MARA KUZUIA FISTULA

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akizunguza na waandishi wa habari mapema leo jijini Dar,kulia kwake ni Mgeni rasmi Mwakilishi Mkazi wa Shirika la kimataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) Bi Jacqueline Mahon.
NA WAMJW-DAR ES SALAAM.

WANAWAKE wajawazito wanatakiwa kuhudhuria Kliniki mara kwa mara ili kuangalia maendeleo ya ujauzito wao na kupata vipimo na matibabu kama itagundulika kuna uwezekano wa kupata ugonjwa wa Fistula.Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa kutoa tamko la ugonjwa wa Fistula katika kuadhimisha siku ya ugonjwa huo duniani.

“Asilimia 60 ya wanawake nchini ndiyo wanahudhuria Kliniki mara kwa mara hii ni dalili mbaya kwani kama mwanamke mjamzito anaweza kuwa na viashiria vya fistula hatoweza kugundulika mapema na kupata matibabu na badala yake asilimia 40 tu ndo wanaohudhuria Kliniki” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha, Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika kutokomeza ugonjwa huo Serikali kupitia Wizara ya Afya imeandaa mkakati wa kupeleka wataalam kwenye kila mkoa kujua idadi ya wagonjwa wa fistula ili kuweza kutokomeza ugonjwa huo.

Vilevile Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali imeimarisha na kukarabati vituo vya Afya vipatavyo 288 katika vitengo vya kuhudumia wenye uzazi pingamizi kwani hiyo nayo ni sababu inayopelekea kwa wanamke kupata fistula.

Hata hivyo Dkt. Ndugulile amesema kuwa huduma za Fistula zinapatikana Bure nchini hasa kwenye hospitali za CCBRT,Bugando na Celian hivyo mwanamke akijiona ana dalili za ugonjwa huo anatakiwa kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za afya na kupata ushauri.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linayoshughulikia mambo ya afya Dkt. Frolence Temu amesema kuwa katika kupambana na ugonjwa wa Fistula nchini wanajenga uwezo kwa watumishi wa Hospitali za Wilaya na Mkoa.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulikia idadi ya Watu UNFPA Bi. Jacqueline Mahon amesema kuwa Shirika hilo limetoa mafunzo kwa watoa huduma za afya wapatao elfu nne ili kupamabana na ugonjwa huo.
“Mbali na kujengea uwezo watumishi hao pamoja na ukarabati wa vituo vya afya ,watanzania wanatakiwa kuacha vitendo vya udhalilishaji kwa wagonjwa wa fistula na wenye ugonjwa huu wajitokeze mara moja kwa ajili ya kupata matibabu” alisema Bi. Mahon.

Mbali na hayo Mkurugenzi Mkuu wa uendeshaji hospitali ya CCBRT inashirikkiana na Serikali katika kupambana na ugonjwa wa Fistula Hospitali yake inafanya matibabu kwa wagonjwa 1500 kila mwaka .Ugonjwa wa Fistula huadhimishwa Mei 23 kila mwaka na maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “BILA YA KUMUACHA MWANAMKE YEYOTE MWENYE TATIZO LA FISTULA NYUMA SHARTI TUDHAMIRIE KUTOKOMEZA FISTULA SASA”

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo mbele ya Waandishi wakati akitoa tamko la ugonjwa wa Fistula katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es salaam.

Mkurugenzi wa Shirika la Amref Afrika Dkt. Floriance Temu akiongea na waandishi wa habari wakati maazimisho ya siku ya ugonjwa wa fistula Duniani mbele ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam.

Comments