Featured Post

SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA NISHATI MBADALA ILI KUHIFADHI MAZINGIRA

Pix 01
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Afisa Misitu Mwandamizi toka Ofisi ya Makamu wa Rais  Timotheo Mande.

Pix 02a Pix 02c
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Afisa Misitu Mwandamizi toka Ofisi ya Makamu wa Rais  Timotheo Mande.
Picha na Eliphace Marwa -MAELEZO
…………………….
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali imewasisitiza wananchi kuacha matumizi ya mkaa na badala yake watumie nishati nyingine ili kuepuka changamoto za uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea kote nchini kutokana na matumizi ya mkaa.
Msisitizo huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayotarajiwa kufanyika Juni 5 mwaka huu.
Waziri Makamba alisema kuwa maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwapa fursa wananchi wa Jiji la Da re Salaam kuelimishwa na kuhamasishwa kupambana na changamoto za uharibifu wa mazingira unaolikumba jiji hilo ikiwemo mafuriko, uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki, kubomoka kwa kuta za fukwe za Bahari ya Hindi pamoja na utumiaji wa kiasi kikubwa cha nishati ya mkaa.
“Nasisitiza kwamba, sote tuna jukumu la kuanza kubadilika kutoka kwenye matumizi ya mkaa na kuanza kutumia nishati mbadala wa mkaa. Tukumbuke kwamba suala la kuhifadhi mazingira ni jukumu letu sote na tunapaswa kulitekeleza kwa vitendo,” alisema Makamba.
Waziri Makamba alieleza kuwa matumizi makubwa ya mkaa hayapo tu katika Jiji la Dar es Salaam bali pia yapo katika maeneo mengine ya nchi, hivyo kutokana na matumizi makubwa ya nishati hiyo, maadhimisho ya kitaifa yataongozwa na Kaulimbiu inayosema; “Mkaa Gharama; Tumia Nishati Mbadala”.
Alibainisha kuwa takwimu zinaonyesha kwamba mpaka mwaka 2017 kiasi cha hekta 46,942 za misitu huharibiwa kila mwaka kwa ajili ya kupata mkaa ambapo matumizi makubwa yako katika miji mikubwa ikiwemo Dar es Salaam, ambako wastani wa tani 500,000 za mkaa hutumiwa kila mwaka.
Waziri Makamba alieleza kuwa uharibifu wa misitu unasababisha kuwepo kwa changamoto nyingine za mazingira kama vile ukame, majangwa, uharibifu wa ardhi, upotevu wa mimea asilia, upotevu wa viumbe hai mbalimbali, upungufu wa upatikanaji wa maji na upungufu wa uzalishaji kwenye kilimo.
“Kutokana na changamoto hizo, wakati wa wiki ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, kutakuwepo maonesho ya nishati mbadala wa mkaa na teknolojia zake. Maonesho haya yatafanyika katika viwanja vya mnazi mmoja kuanzia Mei 31 hadi tarehe Juni 5, 2018,” alisema Makamba.
Alieleza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na Kongamano la Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Uchumi litakalofanyika Juni 1, 2018, Kongamano la viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali litakalofanyika Juni 2, 2018 pamoja na kongamano la wananchi wa Mkoa wa Da res Salaam litakalofanyika tarehe 3 Juni, 2018 katika viwanja vya Zakhem Mbagala.  
Aidha Waziri Makamba alitoa wito kwa mikoa mingine yote nchini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo kwa kuhamasishana, kelimishana masuala yahusuyo hifadhi ya mazingira.
Tarehe 5 Juni, 2018 watanzania wataungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira yaliamuliwa mwaka 1972, katika mji wa Stockholm nchini Sweden, kwenye mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira.
Mwaka huu maadhimisho hayo kimataifa yatafanyika nchini India katika mji wa New Delhi. Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho hayo ni “Beat Plastic Pollution” ambayo inahimiza jamii kuepuka uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki.

Comments