Featured Post

PROF. NDULU APEWA TUZO YA GAVANA BORA WA MWAKA BARANI AFRIKA

ndulu249-660x400
Gavana mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Benno Ndulu, leo jioni ametunukiwa tuzo yamwaka 2018 ya Gavana Bora Barani Afrika inayotolewa na jarida maarufu la African Banker.

Sherehe za kutoa tuzo hizo, zimefanyika jijini Busan, Korea Kusini, katika mikutano yamwaka ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inayoendelea kuanzia tarehe 21 hadi 25 Mei, 2018.
“Hii tuzo nimepewa mimi kutokana na mchango mkubwa kutoka BoT wakati wa uongozi wangu. Kwa hiyo, tuzo hii ni heshima kubwa kwangu na kwa Benki Kuu ya Tanzania,” alisema katika mahojiano jijini Dar es Salaam jana jioni.
“Awali niliwaomba waandaaji nao walikubali kwamba Dkt. Namajeje Weggoro, Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB, Kanda ya Afrika Mashariki, apokee tuzo hiyo kwa niaba yangu. Sikujua kama Naibu Gavana wa BoT, Bw. Julian Banzi Raphael, anashiriki katika mikutano ya AfDB; vinginevyo yeye ndiye angepokea kwa niaba yangu,” alisema Prof. Ndulu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa jarida la African Banker, Bw. Omar Ben Yedder, Prof. Ndulu ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza huduma jumuishi za kifedha na kuchangia katika kuhakikisha zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanafikiwa na huduma rasmi za kibenki.

 “Wewe (Prof. Ndulu) ni mwanzilishi barani Afrika na duniani kote.Umekuwa mstari wa mbele hasa katika kuandaa kanuni na usimamizi makini wa sekta ya kibenki, pamoja na kuhamasisha usahihi na utendaji bora katika sekta hiyo,” alisema Bw. Yedder katika barua yake ya mwaliko kwa Prof. Ndulu.
Hii ni mara ya tatukwa Prof. Ndulu kushinda tuzo ya Gavana Bora wa Benki Kuu barani Afrika. Mwaka 2009 Gavana Ndulu alitangazwa kuwa Gavana Bora wa mwaka Afrika na jarida la Emerging Markets linalochapishwa jijini London, Uingereza. Sherehe hizo zilifanyika katika mikutano yamwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) iliyofanyika Istanbul, Uturuki.
Aidha, Prof. Ndulu alishinda tuzo ya pili ya Gavana Bora wa Benki Kuu barani Afrika mwaka 2015 iliyotolewa na jarida lingine maarufu la Africa InvestorjijiniNew York wakati mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulipokuwa ukiendelea. Alitunukiwa tuzo hizo kutokana na mchango wake mkubwa katika kufanikisha upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha kwa wananchi walio wengi pamoja na kuvutia na kuandaa mazingira bora ya uwekezaji barani Afrika.
Prof. Ndulu amekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kwa muda wa miaka 10 kuanzia Januari 2008 hadi Januari 2018.

Comments