Featured Post

MRADI WA UMEME WA STIEGLER'S GORGE WATENGEWA SHILINGI BILIONI 700

SERIKALI imetenga shilingi bilioni 700 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa Rufiji (Stieglers Gorge) unaotarajiwa kukamilika Julai 2018.

Hayo yalibainishwa jijini hapa leo na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, wakati akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2018/19 ambayo ni shilingi trilioni 1.69.

Waziri Kalemani alisema, mkandarasi ataanza kazi za awali kwa miezi mitatu na kufuatiwa na ujenzi wa miundombinu ya mradi unaotarajiwa kukamilika kwa kipindi cha miezi 36.
Alisema lengo la kutekeleza mradi huo ni kuzalisha umeme wa jumla ya Megawati 2,100 kwa kutumia maji, katika Bonde la Mto Rufiji.
“Utekelezwaji wa mradi huu mkubwa nchini ni kichocheo muhimu katika kuwezesha Tanzania kufikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” alisema.
Aliongeza kuwa, katika kipindi cha mwaka 2017/18 hatua iliyofikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi wa zabuni zilizowasilishwa na wakandarasi walioonyesha nia ya kutekeleza mradi huo.
Aidha, ujenzi wa njia ya msongo wa kV 33 kutoka eneo la Dakawa kwa ajili ya kupeleka umeme unaotumiwa na mkandarasi wakati wa ujenzi wa mradi huo ulianza Novemba mwaka 2017 na unatarajiwa kukamilika Julai 2018.
“Katika kipindi cha mwaka 2017/18 serikali itaendelea kutekeleza mradi huu ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa kambi na ofisi za wafanyakazi, ujenzi wa bwawa na njia kuu za kupitisha maji,” alisema.
Aliongeza kuwa, utekelezaji wa shughuli za ujenzi huo unatarajiwa kuanza Julai mwaka huu na kwamba tayari mkandarasi anakaribia kuanza kazi ya awali.
Miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na upanuzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi 1 kwa kuongeza mitambo itakayozalisha Megawati 185 na kukifanya kutoka uzalishaji wa Megawati 150 kuzalisha Megawati 335.
Alisema mradi huo unagharamiwa na serial kea asilimia 100 kea gharama ya takribani shilingi. bilioni 434 na kwamba katika mwaka wa fedha 2017/18 kazi zilizokamilika ni ujenzi wa misingi ya kusimika mitambo ya kuzalisha umeme na transfoma.
Nyingine ni ujenzi wa kituo cha kupoza umeme, ujenzi wa njia ya msongo wa kV 220 inayounganisha mtambo wa Kinyerezi 1 na 11 na kuunganishwa katika gridi ya taifa.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2018/19 kazi ya usimikaji wa mitambo pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme zitafanyika kwa gharama ya shilingi bilioni 164 ambazo ni fedha za ndani.

Comments