- Get link
- Other Apps
Featured Post
MAPORI MATANO YA AKIBA MKOANI KAGERA NA GEITA KUPANDISHWA HADHI YA KUWA HIFADHI ZA TAIFA (NATIONAL PARKS)
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- Other Apps
Waziri wa Maliasili na Utalii,
Dkt Hamisi Kigwangalla akizungumza bungeni alipokuwa akijibu hoja wa wabunge
waliochangia mjadala wa bajeti wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya
wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma juzi. (Picha na Hamza
Temba-Wizara ya Maliasili na Utalii).
Na Hamza Temba - Dodoma
Wizara
ya Maliasili na Utalii imetangaza kuanza mchakato wa kuyapandisha hadhi Mapori
ya Akiba ya Burigi, Kimisi, Biharamulo, Ibanda na Rumanyika kuwa Hifadhi za
Taifa.
Mchakato
huo tayari umeungwa mkono na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Hayo
yameelezwa juzi bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.
Hamisi Kigwangalla wakati akihitimisha mjadala wa bajeti wa makadirio ya mapato
na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
“Mheshimiwa
Spika, ninaomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa Rais ameridhia
ombi letu la kupandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Burigi, Kimisi, Biharamulo,
Ibanda na Chief Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa, kipekee namshukuru sana Rais kwa kuridhia ombi letu hilo,” amesema Dkt. Kigwangalla.
Amesema
kufuatia hatua hiyo, wizara yake inaanzisha mchakato rasmi wa kukamilisha
taratibu za kupandisha hadhi mapori hayo ili kupanua wigo wa vivutio vya
utalii katika kanda ya Kaskazini Magharibi na hivyo kufikia azma ya Serikali
kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 8 na mapato ya dola za kimarekani
bilioni 16 katika kipindi cha miaka 7 ijayo.
Inaelezwa
kuwa mchakato huo utapitia hatua mbalimbali ikiwemo kuwashirikisha wadau husika
kupata maoni yao, mapendekezo kuwasilishwa baraza la mawaziri kabla ya
kujadiliwa bungeni na hatimaye kuwasilishwa kwa Mhe. Rais kwa ajili ya
kuidhinishwa kuwa Sheria kamili ya kupandisha hadhi mapori hayo.
Akizungumzia
mikakati mingine mipya ya kuboresha sekta ya maliasili na utalii
itakayotekelezwa, Dkt. Kigwangalla amesema ni pamoja na kuanzisha mamlaka ya
usimamizi na uendelezaji wa utalii wa fukwe nchini, kuhuisha maeneo ya vivutio
vya Mambo ya Kale na kuviunganisha katika 'package' moja ya utalii na vivutio
vya wanyamapori.
Mikakati
mingine ni kuunda mfumo mmoja funganishi wa TEHAMA uitwao "MNRT
Portal" kwa ajili ya kutoa leseni na vibali, ukusanyaji wa takwimu na
mapato kutoka vyanzo mbalimbali vya sekta ya maliasili na utalii, ambapo
utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali iliwemo GePG, NIDA, TIRA, BRELA,
TRA na NBS.
Amesema
mikakati mingine ni kuanzisha Jeshi Usu, Utambulisho wa Utalii wa Tanzania
Kimataifa ujulikanao kama "Tanzania, Unforgettable", kufungua utalii
wa kanda ya kusini, kuanzisha mwezi wa maadhimisho ya Urithi wa Mtanzania
"Urithi Festival" (Septemba), kuhuisha sheria za TANAPA, TAWA
na TFS, pamoja na kuunda kanuni mpya za kusimamia vizuri sekta hizo.
Pori
la Akiba Burigi lina ukubwa wa kilomita za mraba 2,941 katika wilaya za
Karagwe, Muleba na Ngara mkoani Kagera, wakati Pori la Kimisi likiwa na ukubwa
wa kilomita za mraba 1,030 katika wilaya za Ngara na Karagwe mkoani humo.
Pori
la Akiba Biharamulo lina ukubwa wa kilomita za mraba 731 katika wilaya ya
Muleba mkoani Kagera na wilaya ya Chato mkoani Geita, huku Pori la Akiba Ibanda
likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 200 na Pori la Akiba Rumanyika kilomita
za mraba 800 katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Mapori
haya yapo katika ukanda muhimu wa kuunganisha watalii kutoka ikolojia za
Magharibi na Mashariki ambapo uwanja wa ndege wa Chato utakuwa muhimu katika
kutoa mawasiliano.
Mapori
hayo ambayo yanasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA
sasa yatakuwa chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania - TANAPA punde
baada ya mchakato wa kuyapandisha hadhi kukamilika.
Bunge
limeidhinisha Sh. bilioni 115.794 kwa ajili ya makadirio ya mapato na matumizi
ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo Sh.
bilioni 85.816 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Sh. bilioni 29,978 ni kwa
ajili ya miradi ya maendeleo.
Comments
Post a Comment