Featured Post

KISWAHILI CHAENDELEA KUSHIKA KASI AFRIKA



NA MWANDISHI WETU
LUGHA ya Kiswahili inazungumzwa katika nchi za Afrika mashariki. Kiswahili hutumika nchini Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Msumbiji na Rwanda.
Kiswahili ndiyo lugha ya taifa katika nchi nne za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Zaidi ya watu milioni 15 hutumia lugha hiyo kama lugha ya kwanza huku wengine 150 kutoka nchi nyingine wakitumia Kiswahili kama lugha ya pili au ya tatu. Ni lugha pekee ya Kiafrika ambayo ni rasmi ya Umoja wa Afrika pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Lugha ya Kicomoro inayozungumzwa katika Visiwa vya Comoro  wakati mwingine hufananishwa na lafudhi ya Kiswahili, ingawa wengine wanaoiona kama ni lugha isiyoshabihiana.
Kiswahili sanifu ya kisasa kimeegemea zaidi katika lafudhi ya Kiunguja inayozungumza Unguja, lakini kuna lafudhi mbalimbali za Kiswahili, baadhi ambazo zinawiana.
Lafudhi za zamani zinazorandanda na Kiswahili ni Kimwani (inazungumzwa Visiwa vya Kerimba katika pwani ya kaskazini ya Msumbiji), Chimwiini kinazungumzwa na baadhi ya wakazi wa mji wa Barawa katika pwani ya kusini ya Somalia, Kibajuni kinazungumzwa na Wabajuni kwenye Visiwa vya Bajuni kwenye mpaka wa Kenya na Somalia ambapo pia kinafahamika kama Kitikuu au Kigunya.
Lafudhi nyingine za Kiswahili ni kama cha Mombasa-Lamu ambako kuna Kiamu, Kipate, Kingozi, Chijomvu, Kimvita, na Kingare.
Kiswahili ya Kimrima kinazungumzwa zaidi Pangani, Vanga, Dar es Salaam, Rufiji na Kisiwa cha Mafia wakati Kiunguja kinazungumzwa zaidi Unguja na Kitumbatu kinazungumzwa Kisiwani Pemba kama ilivyo kwa Kipemba.
Kwa ujumla, lugha ya Kiswahili imekuwa kinara wa lugha nyingine za Kiafrika na inazungumzwa katika nchi hizi zifuatazo:

KENYA
Kiswahili nchini Kenya ni lugha rasmi na pia ni lugha ya Taifa. Rais wa kwanza wa taifa la Kenya hayati Mzee Jomo Kenyatta alitoa kauli kwamba Kiswahili kinafaa kutumika kama lugha rasmi ya Kenya mwaka 1969. Mwaka 1975 Kiswahili kilianza kutumika bungeni.
Serikali ya Kenya ilianzisha somo la Kiswahili katika Idara ya Lugha za Kiafrika na Isimu ya Chuo Kikuu cha Nairobi.
Kuanzia miaka ya themanini mwishoni, takriban vyuo vikuu vyote vilivyoanzishwa na Serikali vilifundisha masomo ya Kiswahili kwa lugha ya Kiswahili.

TANZANIA
Kiswahili nchini Tanzania ni lugha rasmi na lugha ya Taifa. Ni lugha ya utambulisho kwa Mtanzania na inatumika kama lugha ya kuimarisha uelewano, ushirikiano na umoja wa kitaifa.
Katika kuiendeleza lugha hiyo, juhudi za usanifishaji zimefanyika kwa kuwatumia wataalam wa fasihi na isimu, wadau wengine na wachapishaji vitabu.
Vyombo mbalimbali vianzishwa kama Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita), Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza), Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (Takiluki), Taasisi ya Elimu, Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (Uwavita) na Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (Ukuta).
Pia vyuo vikuu mbalimbali vya Bara na Visiwani vilianza kusomesha Kiswahili kuanzia shahada ya kwanza, ya uzamili na uzamivu.

RWANDA
Kiswahili ni lugha rasmi nchini Rwanda. Kabla ya mwaka 1994, wakati wa mauaji ya kimbari lugha ya Kiswahili ilizungumzwa kwenye miji tofauti.
Lugha ya Kiswahili ilisambaa baada ya Wanyarwanda kuwaruhusu Wajerumani nchini mwao kama watawala karne ya 19.
Mwaka wa 1976 -1977 lugha ya Kiswahili ilianza kufundishwa katika shule za upili (sekondari) na Chuo Kikuu Cha Rwanda.

UGANDA
Mwaka 1960, Serikali ya Uganda iliruhusu na kulazimisha Kiswahili kitumike nchini humo; Kiingereza na lugha za kikabila zilikuwa tayari zinatawala mawasiliano Uganda nzima.
Lugha ya maandishi ya Kiswahili yalianza kutumika katika Baraza la Kifalme la Buganda na Bunyoro, hata kabla ya ukoloni (1862).
Kiswahili hutumika katika shughuli za biashara, dini na mila.
Nchini Uganda Kiswahili kilifikiriwa kwamba ni lugha ya watumwa. Lakini Kiswahili kilitumiwa zaidi na Polisi na Wanajeshi.
Katibu mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, Keneth Cimara, aliipongeza serikali ya Uganda kwa juhudi ya kuendeleza Kiswahili tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Mapema mwezi huu ilifanyika warsha ya siku mbili katika hoteli ya Imperial Royal mjini Kamapla iliyowajumuisha walimu wa vyuo vikuu, shule za upili na taasisi mbalimbali nchini Uganda.
Keneth Cimara amesema miaka ya themani raia wengi wa Uganda walikiona Kiswahili kama lugha ya wahalifu ikitumiwa na askari kuwanyang'anya mali zao, aidha kuwatendea uhalifu.
Cimara ameongeza kwamba, sasa Serikali ya Uganda ni miongoni mwa mataifa ya Jumuia ya Afrika mashariki ambayo yameweka mikakati ya kuendeleza matumizi ya lugha ya Kiswahili.

JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO
Kiswahili kiliingia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzia karne ya 19.
Kiswahili kilianza kuenea kutoka Mashariki mwa nchi hiyo, kuelekea kandokando ya Mto Congo.

Comments