Featured Post

DKT ABBASI: WATANZANIA TUENDELEE KUMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI KATIKA KULETA MAGEUZI YA KIUCHUMI


Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
Kilimanjaro
WATANZANIA wametakiwa kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini kwa kuhakikisha kuwa wanakuwa mstari wa mbele katika kulipa kodi ili kuiwekeza Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dkt. Hassan Abbasi wakati wa mahojiano ya kipindi maalum na Redio Boma FM Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro na kuwataka wananchi kuiachia Serikali yao iwatendee haki ya kikatiba katika kuwaletea maendeleo yaliyokusudiwa.
Dkt. Abbasi alisema Watanzania kwa sasa wamepata Serikali makini na sikivu inayowajibika kwa wananchi wake kwa kuwa imeweza kuelewa matatizo na kero mbalimbali za muda mrefu zilizokuwa zikiwakabili katika jitihada zao za kujieletea maendeleo.
Alisema tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kumekuwa na shabaha mbalimbali zilizowekwa ikiwemo malengo ya kuwa na nchi ya uchumi wa viwanda ambayo hata hivyo ilishindwa kufikiwa lakini kwa sasa imefanikiwa katika Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Aliongeza kuwa yapo maendeleo makubwa yanayoendelea kufanyika katika sekta zote za maendeleo nchini hususani kupitia miradi mikubwa inayogusa maisha ya kila siku ya wananchi ikiwemo nishati, maji, elimu, afya na kadhalika ambapo tayari mageuzi yake yameanza kuleta matokeo chanya kwa Watanzania walio wengi.
“Kwa kipindi kirefu tumekuwa na kilio cha umeme wa uhakika hususani kwa wananchi wa vijijini, lakini tunapozungumza kwa sasa Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya umeme ikiwemo Kinyerezi I na kuongeza upanuzi wa megawati kutoka Megawati 150 hadi 185, ni umeme mkubwa unaoweza kulisha mikoa mingi zaidi”  alisema Dkt. Abbasi.
Akiendelea kugusia sekta ya nishati, Dkt. Abbasi alisema Serikali pia imeanza maandalizi ya mradi wa umeme wa Stieglers Gorges ambao ni mradi wa kihistoria uliopangwa kutekelezwa na Hayati Baba wa Taifa na kushindwa kufanyika ambapo hata hivyo Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi chake cha utawala wa miaka mitatu tayari imetangaza zabuni ya ujenzi wa mradi huo unaotarajia kuzalisha megawati 2500.
Aidha Dkt. Abbasi anasema Serikali ya Awamu ya Tano pia inatekeleza miradi mikubwa ya maji katika Mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini katika kasi ya kuridhisha ambapo wakandarasi wake wanaendelea kusimamiwa kwa karibu zaidi na Serikali ili kuifanya kazi hiyo kwa ubora na viwango vilivyopo katika mikataba ya zabuni.
Kuhusu Viwanda, Dkt. Abbasi anasema Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuwa na nchi ya Uchumi wa Viwanda, ambapo hadi sasa kuna zaidi ya viwanda 3000 vilivyoanzishwa chini ya Utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, juhudi zinazolengwa kutengeneza ajira nyingi zaidi kwa Watanzania.
Aliongeza kuwa ili kufanikisha adhma ya kufikia uchumi wa Viwanda, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha na kuimarisha sekta ya usafirishaji nchini ikiwemo usafiri wa anga na majini kwa kununua ndege na meli kubwa zitakazoweza kusafirisha bidhaa mbalimbali ndani na nje ya nchi.

“Serikali imekamilisha meli mbili za MV Ruvuma na MV Njombe ambazo ni meli za mizigo zitakazokuwa zikisafirisha mizigo baina ya Tanzania na Malawi sambamba na kuboresha na kukarabati Meli ya MV Glorias ambazo tayari zimeanza kufanya kazi katika Ziwa Tanganyika sambamba na miradi mingine mikubwa ya Maendeleo” alisema Dkt. Abbasi.

Comments