Featured Post

DKT ABBASI: RAIS MAGUFULI MTUMISHI WA WATANZANIA WOTE.


Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
Kilimanjaro
UFAHAMU wa shida na kero za Watanzania, nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na mfumo imara wa ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo vinaelezwa kuwa ndiyo siri kubwa ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Hayo yamesemwa jana Mkoani Kilimanjaro na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi wakati wa mahojiano ya kipindi maalum na Redio Boma FM, akizungumzia kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo iliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Dkt. Abbasi alisema katika kipindi cha Utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa mfano katika kusimamia utekelezaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali anayoyatoa kwa Watendaji Serikalini, hatua inayosadia kujenga dhana ya nidhamu na uwajibikaji katika kuyafikia maendeleo ya wananchi.
“Rais Magufuli katika kipindi cha miaka yake mitatu ya utawala ameweza kuishi katika dhana ya kutenda na kufuatilia, mfano mzuri ni suala la kuhamia Dodoma ambapo leo hii Viongozi wote wakuu wa Serikali wapo huko” alisema Dkt. Abbasi.
Aidha Dkt. Abbasi alisema ipo mifano mbalimbali inayoakisi azma ya Rais Magufuli ya kutaka kuleta maendeleo ya kweli kwa Watanzania ikiwemo ujenzi wa uchumi imara ambapo hadi sasa ipo miradi mbalimbali ya maendeleio inayoendelea kutekelezwa nchini ikiwemo ongezeko la ujenzi wa viwanda ambavyo vimeweza kuzalisha ajira kubwa kwa Watanzania.
Akifafanua zaidi Dkt. Abbasi alisema ni wajibu wa Watendaji wote Serikalini kusimamia na kuyasemea mafanikio hayo katika maeneo yao ya kazi, kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kutoa ufafanuzi wa hoja na masuala mbalimbali ambayo yamekuwa yakipotoshwa kwa makusudi na baadhi ya watu katika jamii.
Aidha aliwataka Maafisa Habari na Mawasiliano Serilalini kujenga mazoea ya kutumia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii ili kuweza kuisemea Serikali katika kwa kujibu hoja mbalimbali zinazoelezwa katika maeneo yao ya kazi kwani kwa kufanya hivyo wataweza kuisaidia Serikali kwa kutoa ufafanuzi katika upotoshaji unaofanywa na watu wachache.
Dkt. Abbasi alisema Serikali ya Awamu ya Tano kamwe haikatishwi tamaa na wakosoaji wa maendeleo, na badala yake inaendelea kufanya kazi kwa kasi na itahakikisha kuwa itaendelea kuonyesha na kutangaza mafanikio ya miradi mikubwa ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali katika maeneo mbalimbali nchini.

“Hata maendeleo ya miji mikubwa duniani ikiwemo Beijing, New York na London  watu wake walifanya kazi kubwa sana na Sisi katika Serikali ya Awamu ya Tano tunaahidi na tuatekeleza kwa kupigania maisha ya Watanzania ili kufikia malengo tuliyojiwekea” alisema Dkt. Abbasi.

Comments