Featured Post

KAMATI YA MAADILI YA TFF YAMFUNGIA MWENYEKITI WA ABAJALO

Kamati ya Maadili ya TFF iliyokutana Januari 28, 2018 imepitia shauri la mwenyekiti wa Abajalo FC Edgar Chibula lililofikishwa kwenye kamati hiyo na Sektretarieti ya TFF.
HUKUMU
Shauri la Ndugu Edgar Chibula Mwenyekiti wa Klabu ya Abajalo FC lililosikilizwa mbele ya Kamati alishtakiwa kwa kosa la kuongea maneno ya kuikashifu,kuidhalilisha na kuivunjia heshima TFF katika vyombo vya habari ikiwa ni kinyume na kifungu cha 50(1), (2) na (6) cha katiba ya TFF toleo la 2015,Vilevile ni kinyume na kanuni ya 15 na 16 ya kanuni za maadili ya TFF toleo la 2013.
MAELEZO YA KOSA
Chibula akiwa Mwenyekiti wa klabu ya Abajalo FC na mjumbe wa Bodi ya Ligi aliongea maneno ya kuikashifu, kuidhalilisha na kuivunjia heshima TFF katika vyombo vya habari,Akiwa mmoja wa viongozi wa juu wa mchezo wa mpira hapa nchini hakupaswa kuongea maneno ya kukashfu taasisi anayoiongoza, kwa kufanya hivyo amevunja kanuni ya uwajibikaji wa pamoja na utunzaji wa siri za taasisi.
Kwenye shauri hilo, mtuhumiwa hakuweza kuhudhuria na badala yake alileta utetezi wake kwa njia ya maandishi ambao unakubalika kikanuni. Sekretarieti ya TFF iliwasilisha ushahidi wa sauti (audio clip) ya mahojiano aliyofanya na kituo kimoja cha redio ambapo kwenye mahojiano hayo mtuhumiwa alisikika akitamka maneno hayo yasiyo na afya kwa maendeleo ya mpira wetu.
Pia Sekretarieti ya TFF imewasilisha barua ya utetezi kutoka kwa mtuhumiwa ambapo alikiri kuongea na vyombo vya habari baada ya kufanya kila njia ya kuwasiliana na uongozi wa TFF bila mafanikio. Hata hivyo Kamati haikupata nakala ya mawasialiano hayo kutoka kwa mtuhumiwa. Aidha katika barua hiyo mtuhumiwa aliandika maneno yenye kukera na ya kichonganishi.
Baada ya Kamati kupitia shauri hili imeridhika pasipo na shaka tuhuma dhidi ya mtuhumiwa, kitendo cha kumhusisha mdhamini kwa kuishutumu taasisi inayoongoza mpira ni uchonganishi na ni hatari kwa maendeleo ya mpira; kinaweza kuwaogopesha wadhamini wengine ambao wana nia ya kuwekeza katika mpira,Mtuhumiwa hakuwa na ushahidi wowote uliombatana na tuhuma hizo zinazoweza kudidimiza jitihada za kuinua mchezo wa mpira nchini.

Kamati imemtia hatiani Bw. Edgar Chibula kwa kosa la kuongea maneno ya kuikashifu, kuidhalilisha na kuivunjia heshima TFF katika vyombo vya habari ikiwa ni kinyume na kifungu cha 50 (1), (2) na (6) cha katiba ya TFF toleo la 2015. Hivyo Kamati inamuhukumu kifungo cha kutojihusisha na shughuli za mpira kwa kipindi cha mwaka mmoja (1) na faini ya shilingi milioni tatu (sh.3,000,000) chini ya kifungu cha 73(4) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.

Comments