Featured Post

BARAZA LA MICHEZO LATOA UTARATIBU WA KUWASILISHA RUFAA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BARAZA LA MICHEZO LA TAIFA (BMT)
 



Simu: +255 (222) 2850015                                                                                                                               Barabara ya Taifa,
Baruapepeinfo@nationalsportscouncil.go.tz                                                                            Uwanja wa Taifa,
Tovuti: www.nationalsportscouncil.go.tz                                                                                         Ghorofa ya 2,
S.L.P 20116,
                                                                                                                                                           DAR ES SALAAM.
               
                                                                         

                                                                                            8 Februari, 2018


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UTARATIBU WA KUWASILISHA MALALAMIKO AU RUFAA KATIKA SEKTA YA MICHEZO NCHINI

Shughuli za Michezo nchini zinafanyika kwa mujibu wa sheria ya Baraza la Michezo la Taifa namba 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya sheria namba 6 ya mwaka 1971.
Aidha, kutokana na kufanyika kwa  shughuli mbalimbali, kila chama, shirikisho, klabu au asasi na taasisi zina miongozo mbalimbali inayosaidia kuendesha michezo katika maeneo yao.
Hata hivyo, katika kutekeleza shughuli za michezo kama vile mashindano, yamekuwa yakiibuka malalamiko/migogoro ambayo kwa namna moja au nyingine inahitaji utatuzi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu stahiki hasa kwa vyama vilivyosajiliwa kama vile:-
(a)             Vyama vya Michezo;
(b)            Mashirikisho ya Michezo;
(c)             Vilabu vya Michezo;
(d)            Taasisi za Kimichezo
(e)             Wadau wote wa michezo nchini.
Ieleweke kuwa, ziko taratibu za kufuata katika kuwasilisha malalamiko/migogoro  kama ifuatavyo:
1)            Malalamiko/rufaa ya Mchezaji, Kiongozi, Chama, Klabu, Mwalimu, Mwamuzi, Daktari wa Timu  au mdau mwingine wa michezo anao uhuru na haki ya kuwasilisha malalamiko yake/rufaa kwa kufuata utaratibu kwa ngazi ya juu endapo hakuridhika na uamuzi uliotolewa na Uongozi wa Ngazi husika kama vile;

a)   Katika ngazi ya Wilaya:
i)            Malalamiko yatapelekwa kwa Chama cha Mchezo husika na kwa mujibu wa Kanuni za mchezo husika.  Nakala yake itapelekwa katika Kamati ya Michezo ya Wilaya katika muda usiozidi siku tatu (3) baada ya uamuzi kutolewa;

ii)          Kama mlalamikaji hataridhika atakata rufaa kwa Kamati ya Nidhamu, Rufaa na Usuluhishi ngazi ya Wilaya katika muda usiozidi siku saba (7).  Nakala yake itapelekwa ngazi ya michezo ya Mkoa na Kamati ya Michezo ya Mkoa;

iii)       Kama mlalamikaji hataridhika na uamuzi wa Kamati ya Michezo ya Wilaya atakata rufaa kwa Kamati ya Michezo ya Mkoa katika muda usiozidi siku saba (7) na nakala itapelekwa Baraza la Michezo na Chama cha Mchezo ngazi ya Taifa;

iv)        Endapo hataridhika na Uamuzi wa Baraza atakuwa na haki ya kukata rufaa kwa Waziri katika muda wa siku saba (7) na maamuzi ya Waziri yatakuwa ya mwisho.

b)    Katika Ngazi Mkoa.
i)             Mlalamikaji atakata rufaa kwa Chama cha Michezo ngazi ya Mkoa katika muda usiozidi siku tatu (3) na nakala itapelekwa kwenye Kamati ya Michezo ya Mkoa;

ii)           Kama hajaridhika na maamuzi ya Chama cha Michezo ngazi ya Mkoa atakata rufaa kwa Kamati ya Michezo ya Mkoa katika muda usiozidi siku saba (7) nakala yake itapelekwa kwa Chama cha Mchezo cha Taifa na Baraza la Michezo la Taifa.  Kamati ya Michezo ya Mkoa itahakikisha upo ujumbe wa Chama ngazi ya Mkoa rufaa hiyo itakaposikilizwa;

iii)        Kama mlalamikaji hataridhika, atakata rufaa kwa Baraza la Michezo la Taifa katika muda usiozidi siku saba (7).  Baraza la Michezo la Taifa lihakikishe kuna ujumbe wa Chama ngazi ya Taifa linapojadili rufaa hiyo;

iv)         Endapo mlalamikaji hataridhika na uamuzi wa Baraza la Michezo atakuwa na haki ya kukata rufaa kwa Waziri wa Michezo katika siku saba (7) na maamuzi ya Waziri yatakuwa ni ya mwisho.

c)      Ngazi ya Taifa:

i)             Mlalamikaji atakata rufaa kwa Baraza la Michezo la Taifa katika muda usiozidi siku saba (7) nakala itapelekwa kwa Waziri;

ii)           Asiporidhika na uamuzi wa Baraza atakata rufaa kwa Waziri katika muda usiozidi siku saba (7) na uamuzi wa Waziri utakuwa ni wa mwisho.

Hivyo Basi, kwa utaratibu huu, Vyama vyote, mashirikisho na Vilabu na Wadau wa Michezo nchini, mnasisitizwa kufuata utaratibu huu ambao ni muhimu ili kutoruka ngazi ili kupata maamuzi na ushauri stahiki kwa manufaa ya maendeleo ya Michezo, ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla katika kuimarisha Utawala Bora.

Imetolewa na:

Frank Mgunga,
Afisa Habari.


Comments