Featured Post

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI IMEUNDA TIMU YA WATAALAMU 15 KUFUATILIA UTEKELEZAJI ZOEZI LA UPIGAJI CHAPA KATIKA MIKOA 26 TANZANIA BAR

 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Maria Mashingo akipiga chapa ng’ombe katika Kijiji cha Igalula Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi ikiwa ni sehemu ya timu ya wataalamu 15 ya Wizara hiyo walioko katika mikoa 26 ya Tanzania bara kufuatilia na kusimamia kikamilifu zoezi la upigaji chapa ambapo Dk Mashingo alisema mifugo itakayokuwa haijapigwa chapa hadi kufikia Januari 31 mwaka huu haijulikani Serikali nini kuhusu mifugo hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo) Dk. Maria Mashingo akiwaonesha wafugaji sehemu sahihi ambayo ng’ombe anatakiwa kupigwa chapa ili kuepuka kuharibu ngozi baada ya kushiriki zoezi la upigaji chapa katika Kijiji cha Igalula wilayani Tanganyika mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya timu ya wataalamu 15 iliyoundwa na Wizara hiyo kufuatiliaji na kusimamia upigaji chapa kabla ya Januari 30 mwaka huu
NA  MWANAHAMISI MSANGI, WMVU
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imeunda timu ya wataalamu 15 iliyopo katika mikoa 26 ya Tanzania bara ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Mifugo) Dk. Maria Mashingo kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa zoezi la upigaji chapa mifugo yote nchini kabla ya kufika tarehe ya mwisho ya muda wa nyongeza wa Januari 31 mwaka huu.
Timu hiyo ya wataalamu imeanza kutekeleza majukumu yake Januari 4 mwaka huu ambapo kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Maria Mashingo wilaya 30 ambazo bado hazijaanza zoezi la chapa na zimetiliwa mkazo katika ufuatiliaji ikiwemo Monduli,  Kilwa, Liwale, Ruangwa, Mafia.
Aidha, Wilaya nyingine ni Sikonge, Tabora, Urambo, Mwanza, Ilemela Manispaa, Magu, Ukerewe, Buchosa, Tarime, Kyerwa, Ngara, Newala, Newala Mjini, Tandahimba, Nanyamba, Mtwara, Mikindani Manispaa, Masasi, Masasi Mjini, Nanyumbu, Moshi DC, Hai, Same, Rombo, na Kigamboni.
Dk.  Mashingo amesema suala la upigaji chapa mifugo lipo kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa mifugo Namba  12 ya Mwaka 2010 ili kudhibiti magonjwa ya mifugo pamoja  na wizi wa mifugo, kuimarisha usalama wa afya na mazao ya mifugo pamoja na kudhibiti usafirishaji na uhamaji holela wa mifugo.
Amesema jumla ya ng’ombe millioni 19, 219,487 sawa na theluthi mbili ya ng’ombe  wote milioni 28, 829,231 walioko nchini ambapo mpaka sasa jumla ya ng’ombe milioni 7, 701,661 sawa na asilimia 38.5 ndio wamepigwa chapa ambapo wamechangia kiasi cha shs. Bilioni 3, 700,830,500 kwa malipo ya Tsh 500 kwa kila ng’ombe.
Hivyo, Tathmini iliyofanyika kutokana na taarifa zilizokusanywa kutoka halmashauri zinaonesha kwamba, kati ya malengo waliojiwekea, Halmashauri 62 wamepiga chapa zaidi ya asilimia 50; Halmashauri 43 zimepiga kati ya asilimia 10 hadi 50; Halmashauri 23 zimepiga chini ya asilimia 10 na Halmashauri 30 hazijaanza lakini ziko kwenye maandalizi.
Ametaja baadhi ya changamoto zilizochangia kuathiri utekelezaji wa zoezi la chapa ni wafugaji kukataliwa kupiga chapa mifugo yao kwa kisingizio kuwa ni wavamizi na wahamiaji haramu katika Wilaya za Kibiti, Rufiji, Sumbawanga, Tanganyika, Kibondo.
Pia kutofautiana kwa gharama za uchangiaji ambapo baadhi ya wafugaji waliogomea kiwango cha sh 1000/= ambacho ni kinyume na kiwango elekezi cha sh 500/= kwa kila ng’ombe mfano katika Wilaya za Chunya na Tanganyika.
Vilevile fedha zilizochangwa kugharamia zoezi la chapa kutotolewa kwa wakati katika baadhi ya Halmshauri ikiwemo Mbarali na Misungwi hivyo kukwamisha utekelezaji wa kazi hiyo.
Timu hiyo ya watalaamu imegawanyika katika makundi saba kwenye mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Singida, Dodoma, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam.
Mikoa mingine ni Tabora, Katavi,Rukwa, Kigoma, Shinyanga, Simiyu, Mara,Mwanza, Geita, Kagera, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Comments