Featured Post

WASI (WAALAGWA) - 2: MASIMANGO YA NGOMANI YALILETA NJAA


Na Innocent Nganyagwa
KARIBUNI kwenye safu yetu ya utopevu wa kijadi na mambo ya historia, tunapochambua historia za makabila yetu mbalimbali ya hapa nchini na kwingineko.
Leo tunaingia katika sehemu ya pili itakayotuhitimishia simulizi za ndugu zetu Wasi (Waalagwa) tulioanza kuwatembelea jana.

Basi kabla sijaendelea, kwanza niwakumbushe baadhi ya wale ambao hamkubahatika kusoma simulizi za Waalagwa jana, tuliongelea nini juu yao.
Kwa kifupi tulieleza kuwa ndugu zetu hawa wanaozungumza lugha yao ya Chasi, wamegubikwa utata wa utambulisho wao halisi kutokana na sababu kadhaa.
Kwanza hudhaniwa ni sehemu ya jamii za Kirangi na Kiiraqw, ambazo ni za Kihamitiki na Kikushi. Lakini la pia wao wenyewe kuhusishwa na mbari hizo mbili za Kihamitiki na Kikushi, japo kwa kabila kutokana na mbari zaidi ya moja si jambo la kustaajabisha sana. Kwa kawaida kuna makabila yanayotokana na mbari kuu, lakini pia yapo yanayotokana na mchanganyiko wa mbari.
Nadhani unazikumbuka mbari hizo kuu tano za Kiafrika ambazo huwa tunarudia kuzitaja mara kwa mara kwenye safu yetu hii. Niwakumbushe kuwa kuna Wanailotiki, Wakhoisan, Wakushi, Wahamitiki na Wabantu.
Inakupasa ufahamu kuwa sisi wote ni Waafrika lakini tuna mafungu yetu ya kijamii, ambayo yamezalisha makabila tunayotokea.
Mafungu hayo ndiyo huitwa mbari, neno hilo mbari halijazoeleka sana ila kwa sasa linaanza kufahamika zaidi, kutokana na kukua kwa lugha ya Kiswahili.
Ndiyo maana wakati fulani yalipotokea mauaji makubwa kwa ndugu zetu wa Rwanda na Burundi, vyombo vya habari vya Kimataifa vilikuwa na kawaida ya kusema ‘Mauaji ya Kimbari’.
Japo walilenga zaidi msigano wa Wahutu na Watutsi, lakini kwa kina hasa ilimaanisha jamii ya mbari moja dhidi ya jamii ya mbari nyingine.
Kwa hiyo, wewe umezaliwa kwenye familia yako, lakini wewe na wenzio mliozaliwa pamoja mna jina la ukoo wenu.
Basi huo ukoo wenu ni wa kabila fulani na hilo kabila linatokana na mbari fulani, kwa kifupi huko ndiko hasa unakotokea.
Ni mlolongo mrefu lakini nadhani umenielewa Mjadi, haya, nilikuwa nakumegea elimu kidogo ya kina cha ujadi.
Tukiendelea na mambo ya Waalagwa (Wasi), ndugu zetu hawa si wengi, ni wachache kwa kweli. Wengi kati ya hao wachache wanaishi kwenye eneo la nchi yao ya Ualagwa, wakitangamana na Waburunge na Warangi.
Basi tukiwatazama kwa ukaribu zaidi hawa Wasi, ni kwamba, nchi yao ina mabonde na vilima vyenye miamba. Vilima hivyo vina baadhi ya wanyama pori na huwapatia nishati ya kuni, lakini udongo wa nchi yao ni mgumu kutokana na kuwa na asili ya miamba.
Eneo lenye rutuba zaidi katika nchi ya Waalagwa lipo katikati, kutokana na mto wa Bubu wenye maji safi unaokatiza mahali hapo. Lakini kule kwenye miinuko ya vilima kuna ukame na uhaba wa maji, hali inayochangiwa na mvua kidogo inayonyesha. Nilisema, kwa kawaida kwenye nchi hiyo ya Ualagwa mvua za kuaminika hunyesha mara moja tu, kati ya mwezi Desemba na Mei.
Na kuhusu utata wa utambulisho wao ni kwamba licha ya zile sababu nilizokueleza awali zilizosababisha wadhaniwe kuwa ni jamii za makabila ya Warangi na Wairaqw, lakini pia kuna sababu nyingine. Wao wenyewe wanatokana na mchanganyiko wa mbari mbili, Ukushi na Uhamitiki. Lakini tofauti na makabila mengine, wao walipata mchanganyiko huo kutokana na sababu nyingine pia.
Usichanganyikiwe, maana hapo unaona sababu moja inazalisha nyingine, ndivyo udadavuaji wa utopevu wa kijadi ulivyo.
Tuyaona kwenye simulizi za makabila tuyakayoyatembelea kwenye safu hii, kuwa yale yaliyoko kaskazini mengi yalitokea kaskazini mwa bara letu na kuja huku kusini.
Baada ya kulowea na kuanzisha makazi, baadaye jamii au makabila yake tanzu yalitawanyikia maeneo ya pembezoni. Lakini tofauti na hali hiyo, watu wa masalia ya jamii zilizozalisha Wasi walitoka Iramba-Singida na kwenda Mashariki ya Kati mnamo miaka mingi iliyopita. Na kama unakumbuka, ni kwamba ukitoka hapo Mashariki ya Kati kuelekea Mashariki ya Mbali, eneo hilo la kipitio ndiyo chanzo cha mbari ya Kihamitiki.
Kwa hiyo, hawa Wasi walikwenda kinyume, kwa kutoka huku na kwenda huko wanakotokea wengine kuja huku. Lakini walipofika huko hawakutangamana na wenyeji, kutokana na kusigana kulikosababishwa na imani zao kuwa tofauti. Wenyeji wa huko walishaukumbatia Uislamu na hawa Wasi walikuwa na imani zao za kijadi za kuabudu mizimu, Basi hawakuwiva, wakasigana.
Eneo hilo la Mashariki ya Kati kuelekea Mashariki ya mbali ni kiini cha Uhamitiki, lakini pia ni eneo la kiini cha chanzo cha Uislamu.
Hawa Wasi waliofika hadi huko Mecca, baada ya kushindwa kutangamana na wale wenyeji wa Kiislamu wakaamua kugeuza na kurudi walikotokea. Katika safari yao ya kurudi wakapitia eneo la Uhabeshi, Ethiopia, mahali wanakopatikana Wakushi kwa wingi.
Wakatangamana na kuzaliana nao, hapo ndipo Ukushi ulipolowea damuni mwao na kusababisha wawe Wahamitiki-Wakushi. Maana ule Uhamitiki waligubikwa nao vilivyo walivyofika kule Uhamitikini, halafu katika kurudi wakalowea kwa muda kwenye nchi ya Ukushi.
Kutoka hapo kwenye nchi ya Ukushi, wakaingia hapa nchini kwa kupitia Kaskazini Mashariki. Wakaweka kituo cha muda mrefu kidogo kwenye eneo lililo katikati ya Mlima Hanang’ na Kondoa, mahala hapo panaitwa Halas’o.
Kutoka hapo ndipo safari yao ikawafikisha mahali walipo sasa kwenye nchi ya Ualagwa, huko Kondoa. Lakini pale walipolowea mara ya mwisho kabla ya kuingia Kondoa, wameacha urithi wa mizimu yao.
Mara kadhaa nyakati za usiku, mahali hapo husikika ngoma zikipigwa na watu wakiimba na kucheza, lakini watu hao hawaonekani.
Kwa ujumla, hawa Waalagwa wana mambo yao ya kijadi yanayozingatia matambiko.
Mathalan, kwenye tambiko la kuita mvua huchinja kondoo mweusi na kunyunyiza damu yake kwenye majani ya mti yaliyopondwapondwa, kisha kusambazwa kuuzunguka mti huo.
Namaanisha mti ambao huchaguliwa kufanyikia tambiko husika, basi ile damu kwa kutapakazwa kwenye majani yaliyouzunguka ule mti ni kuitapakaza kuuzunguka mti wenyewe pia.
Hayo ni baadhi ya mambo ya ndugu zetu hawa tuliyoyaona jana, tulipoanza kuwatembelea.
Tukiendelea mbele na simulizi zao, ni kwamba Wasi ni wakulima na wafugaji pia na wanapendelea kulima mahindi na mtama. Hawana kawaida ya kulima mbali na makazi yao, pia hufuga mifugo mbalimbali midogo midogo kama mbuzi na kuku.
Ndugu zetu hawa hupenda kujenga nyumba zenye mapaa marefu ya msonge, yaani yamechongoka kwa juu na nyumba hizo huwa na uzio wa nje unaotengenezwa kwa matete.
Waganga kwao ni watu wanaoheshimika na huwasaidia sana kwa matibabu ya maradhi, pia kuondoa matatizo yanayohitaji uwezo wa kijadi kuyakabili.
Waalagwa wana mchanganyiko mwingine ambao unaweza kukutatanisha pia, lakini huu unahusiana na lugha yao.
Mara nyingi wakiwa kwenye maeneo yao hujiita Waalagwa, na lugha yao huiita Kialagwa. Lakini kwa kule kufahamika na wengine kwa jina la Wasi, basi wakiwa ugenini hupenda sana kujiita Wasi na kuita lugha yao Chasi.
Kama utakumbuka, awali nilisema kuwa wana mchanganyiko wa mbari za Ukushi na Uhamitiki, lakini kwa upande wa lugha wameelemea zaidi kwenye Ukushi. Na kama utakumbuka pia, nilisema kuwa wao na Waburunge ni sehemu ya mabaki ya Wairaqw, kabila ambalo pia lilizalisha kabila la Wagorowa. Hata hao Wagorowa nao lugha yao ni ya Kikushi, ila wao wako karibu na waliko Wairaqw hivi sasa.
Waburunge na Waalagwa wao walisalia kule Kondoa, kwa kuwa ni masalia yaliyoachwa hapo na Wairaqw wakiwa njiani kwenda iliko nchi ya Uiraqw kwa sasa.
Kwa hiyo, Wasi na Waburunge wakatangamana kwa ukaribu zaidi, nikimaanisha kuwa zamani walikuwa jamii moja ya masalia.
Walikuja kutenganishwa na Warangi waliolowea katikati yao, hali iliyosababisha Waalagwa wawe Kaskazini-Magharibi na Waburunge Kusini-Mashariki mwa nchi waliyokuwapo.
Ndugu zetu hawa hutahiri jinsia zote na tohara ya jinsia ya kike ilianzia maeneo ya Kolo wakati ule walipokuwa wanarudi kutoka kule kaskazini.
Sherehe hizo za tohara ya kike ziliambatana na ngoma, lakini muda si mrefu baada ya kuanza mila hiyo ya tohara njaa kubwa iliwakumba.
Njaa hiyo ilisababishwa na masimango ya wanawake wa kabila hilo, kwa mwanamke mgumba ambaye hakuwa na mtoto.
Ilitokea mwanamke huyo alikuwa hodari sana wa kucheza ngoma, mara nyingi alipendelea kwenda kwenye sherehe za tohara za mabinti wa wenzie na kucheza ngoma. Lakini kwenye sherehe moja alisimangwa na mwanamke mwenziye, kuwa anapenda sana kucheza ngoma kwenye tohara za mabinti wa wenziwe, lini nao wataenda kucheza ngoma kwake? Masimango hayo yalimchoma moyo sana yule mwanamke, akaazimia kulipiza kisasi.
Maana ni dhahiri, wenzake walimsimanga kwa kumuonea wivu kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusakata ngoma.
Kimbilio lake lilikuwa kwa mganga, aliyemfanyia dawa iliyosababisha njaa kubwa kwa muda wa miaka minne. Alichofanya yule mganga ni kutumia uwezo wake wa ulozi kuwaita ndege wa porini waliotumwa kufukua mbegu zilizopandwa kwenye mashamba ya wale wanawake waliomsimanga mwenzao.
Ndege walikuwa wengi na mchanganyiko, ila wengi wao wakiwa aina ya hapanga’ch. Basi walitekeleza maagizo ya kilozi kama walivyotumwa, kwa kufukua mbegu mashambani mara baada ya kupandwa kabla mvua haijazirutubisha.
Kwa muda wa miaka minne waliendelea kufanya hivyo, licha ya mvua kunyesha sana kwa muda huo lakini hakukuwa na mavuno.
Njaa ikanuka, wale wanawake wasimangaji wakakimbilia kwa majirani kuomba chakula.
Lakini wale ndege walilogelezwa, kiasi kwamba walienda kufukua pia mbegu za mashamba ya majirani hao. Njaa ikapiga hodi hadi huko pia, hatimaye ikawabidi waende maporini kutafuta chakula ambako walianza kula mizizi ya miti.
Hiyo, ilikuwa njaa mbaya na ya kihistoria, iliyoua watoto wengi wa wale wanawake waliomsimanga mwenzao na wa wengine pia.
Katika kumbukumbu za simulizi za historia ya Waalagwa, njaa hiyo haisahauliki hata sasa. Maana hakuna aliyejua ilisababishwa na nini, kwa kuwa wale ndege walifukua mbegu katika muda ambao hawakuonekana na mtu.
Na kwa kuwa walipewa nguvu ya kilozi, haikuwa rahisi kuona dalili za kufukuliwa mbegu zile ukifika shambani. Ni njaa hii ambayo kwa kiasi kikubwa, iliwapa fursa Warangi kujichomeka katikati ya jamii hiyo na kuigawanya. Maana kuna Waalagwa walioenda Isabe kutafuta mizizi na Waburunge walioenda Goima.
Kama utakumbuka hizo ni zile pande nilizokutajia awali, za mgawanyiko wa umoja wa Waburunge na Waalagwa kijamii.
Haya Wajadi wenzangu, simulizi zinanoga lakini fursa imetuishia na bado kuna mengi ya kuvutia kuhusu ndugu zetu hawa ambayo hatujayasimulia ila tunaishia hapa kwa leo.
Tujumuike tena kesho kwa simulizi zaidi za kijadi.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Juni 13, 2009.

Comments