Featured Post

WARANGI: KABILA LILILOTAFUTA VYANZO VYA MAJI


Na Innocent Nganyagwa
KAMA kawaida, leo tunakutana tena kwenye safu yetu ya utopevu wa kijadi na kujivunia asili zetu.
Basi nawakaribisheni nyote, ambapo leo tunapata fursa ya kusogea hadi kwa ndugu zetu Warangi, kabila linalopatikana kwenye eneo lililopo kati ya Babati na Kondoa, lakini hasa wakiwa kwa wingi huko Kondoa.

Ndugu zetu hawa kwa sasa wengi wetu tunawaita Warangi na wanaongea lugha yao ya Kirangi, lakini kwa asili wao wenyewe wanajiita ‘Valangi’ kwa matamshi yao halisi na lugha yao ni ‘Kilangi’ au ‘Kilaangi’.
Kutokana na historia yao na namna walivyofika eneo walilopo, ndugu zetu hawa wanatangamana na makundi kadhaa ya makabila mengine yakiwemo yale ya kizururaji, lakini wamefaulu kulinda utambulisho wao na kubaki kama walivyo.
Baadhi ya majirani zao ambao kihistoria wameshawahi kuwepo na wengine bado wapo mkabala nao kwenye eneo hilo ni Wamasaai ambao ni Wanailotiki, Wasandawe ambao ni Wakhoisan, Wairaqw, Waburunge, Wasi na Wagorowa makabila yanayotokea mbari ya Kikushi na Wambugwe ambao ni Wabantu.
Lugha ya Warangi imeathiriwa na makabila haya wanayotangamana nayo kwenye eneo moja, lakini ina ukaribu zaidi na Kimbugwe kuliko lugha za yale makabila mengine.
Ndugu zetu hawa wametoka mbali kabla hawajafika eneo walilopo, japokuwa unaweza kuwa umeshazisikia historia nyingine zinazoeleza maeneo mengine tofauti waliyotokea.
Jamii za awali za mababu wa Warangi kwa asili zinatokea kaskazini na mashariki mwa bara hili, walisafiri kutoka upande huo na kupitia eneo la Bonde la Ufa hadi Kenya wakipita Ethiopia kwanza.
Walipofika hapa nchini walilowea Babati kwanza, kabla ya kujisogeza kwenye maeneo mengine ya pembezoni.
Katika safari zao, ndugu zetu hawa walipita maeneo mengi kwa misimu tofauti ya hali ya hewa ukiwemo wakati wa ukame.
Kutokana na maeneo waliyopitia nyakati za kiangazi, walikuwa na kawaida ya kutafuta maji kwa mbinu mbalimbali.
Wakifanikiwa kupata maji katika eneo husika, basi huamini mahali hapo panawafaa kuishi na huamua kulowea na kuanzisha makazi yao.
Kwa kawaida walikuwa wakichimba mashimo marefu na kutumbukiza vyombo ndani ya mashimo hayo, kisha waliendelea na safari zao.
Wakirudi kwa mara ya pili katika eneo hilo na kukuta vyombo hivyo walivyoviweka kwenye mashimo vimejaa maji, huamini sehemu hiyo ina neema na wanaweza kuishi mahali hapo.
Katika historia ya misafara yao, waligawanyika makundi mawili walipofika Babati. Kundi la vijana walikwenda kuwinda ndege aina ya kanga pembezoni mwa maeneo waliyokuwepo ya Babati, waliporudi hawakuwakuta wenzao waliowaacha na kuendelea na safari ya kutafuta nchi mpya ya kuishi.
Kanga kwa Kirangi huitwa ‘mbuwe’, basi wale vijana walioachwa mahali pale waliamua kuendelea kuishi pale na kuwa sehemu ya Wambugwe.
Hiyo ndiyo sababu inayofanya lugha zao ziwe na namna fulani ya maingiliano ya karibu zaidi, kuliko lugha za yale makabila mengine wanayotangamana nayo tuliyoyataja hapo awali.
Lile kundi lingine lililowaacha wale wenzao, lilielekea kusini zaidi na kufika hadi eneo la Haubi. Sehemu hiyo waliikuta ina kile walichokitafuta, maana maji yalipatikana kwa wingi na hayakuwa yakikauka kwa misimu yote, basi wakalowea mahali hapo.
Ndiyo maana hata sasa kuna Warangi wanaofahamu na kuamini kuwa kwa asili wao wanatokea hapo Haubi.
Ndugu zetu hawa ambao pia hulima mahindi na mtama, kiini cha nchi yao ya Kirangi ni kusini magharibi huko Kondoa waliko kwa wingi.
Nadhani bado unakumbuka kuwa tukisema nchi ya jina la kabila fulani tunamaanisha nini.
Eneo hilo la kiini cha nchi yao lina vijito vingi vidogo vidogo, lakini ambavyo kukiwa na kiangazi kikali na ukame hukauka na kwa nyakati hizo hulazimika kuchimba ili kupata maji.
Tuseme ni kama walivyokuwa wakifanya mwanzoni, walipokuwa wakizurura kutafuta maji tangu huko kaskazini walikotokea.
Katika eneo hilo la kiini cha nchi ya Kirangi kuna vijiji kama vile Hurui, Mwaikisabe, Kibaya, Mangoroma, Mafai, Mesanga, Mnenya (Mnenia), Loo na Iyoli.
Eneo lao hilo la kiini cha nchi ya Urangi limezungukwa na milima na miinuko ya nchi na uwanda, hali inayosababisha makundi yao mengi kupatikana kwenye maeneo sawia.
Hiyo inamaanisha kuwa, waliishi kwa makundi kwenye maeneo hayo na hakukuwa na watu wengine waliotawanyikia kwenye maeneo ya pembezoni mwa nchi yao, kutokana na jiografia halisi inayowazunguka ilivyo.
Hata yale makabila mengine yaliyo pembezoni mwao, kama vile Wasandawe, hupatikana mbali kidogo kutoka kwenye kiini cha nchi ya Urangi, baada ya kupita misitu.
Kwa hiyo, hawa Warangi wenyewe ni kabila lenye jamii inayopenda kujiweka karibu kwa pamoja kwenye mambo yao.
Kwa hulka hizo basi, utaona kuwa ndugu zetu hawa wanajivunia sana asili yao na hawagubikwi kirahisi na jamii nyingine na kuacha mambo yao.
Mathalan, licha ya lugha yao kuwa na muingiliano na Kimbugwe, lakini wanapokutana Mrangi na Mbugwe, Mrangi akiongea Kirangi watasikilizana na Mbugwe.
Lakini wao Warangi hawapendi kusemeshwa Kimbugwe, bali Kirangi. Kuna baadhi ya maneno kama vile jua ambalo kwa Kimbugwe ni ‘ijova’ kwa Kirangi ni ‘ijuva’ ikimaanisha alama ya uwepo wa Mungu.
Japo kwa sasa kwa Kirangi jua linafahamika zaidi kama ‘mwaasu’, lakini Mbugwe akitaja ‘ijova’ Mrangi anamuelewa kuwa anamaanisha ijuva, yaani jua.
Kujivunia na kuhifadhi lugha yao, ni moja kati ya mambo yanayowafanya watambulike kuwa wapo.
Hata katika kuoana, mara nyingi wao hupendelea zaidi ndoa za jamii yao wenyewe.
Na ikitokea wakaoa jamii za pembezoni mwao, basi watu wa zile jamii ndiyo hutakiwa kufuata lugha na mambo yao na sio wao kuwafuata wengine.
Lakini hiyo isikusababishe uwaelewe tofauti, hapana, hawa ni watu waungwana na wapole tu wanaowiana vyema na jamii nyingine, kwenye maeneo wanayoishi walikochanganyika na watu wa makabila mengine.
Leo ndiyo kwanza tumewapigia hodi hawa ndugu zetu Warangi, ambao wao na Wambugwe wana uwiano fulani kwenye lugha yao kama tulivyoona.
Tutakavyoendelea kuchambua mambo yao kesho, tutaona uwiano huo na mambo yao mengine.
Basi tukutane tena kesho kwenye safu yetu, ili tuendelee kutathmini mambo ya ndugu zetu hawa.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Machi 14, 2009.

Comments