Featured Post

WANYISANZU: JINSIA NA MIZIMU HUSABABISHA MVUA

 Kipeyo au Lukulu (Kinyisanzu) ni chombo cha kunywea vinywaji mbali mbali kwa kabila la Wanyisanzu.

Na Innocent Nganyagwa
KARIBUNI ndugu zangu, ni siku nyingine tena tunakutana kupata fursa ya kutopea kwenye ujadi wetu.
Baada ya kuwatembelea ndugu zetu Wakimbu, leo tunaendelea mbele na ziara zetu za kijadi, zinazotuwezesha kufahamu japo kwa uchache, baadhi ya mambo mbalimbali ya makabila.

Ndugu zetu Wanyisanzu wanapatikana zaidi mkoani Singida, Wilaya ya Iramba, Tarafa ya Kirumi, wakipakana na Wilaya ya Maswa na Meatu kwa Mkoa wa Simiyu (zamani Shinyanga).
Pia kutokana na mahali walipo, wanapakana na wilaya za Mbulu na Karatu. Kwa uchache, makabila majirani zao ni Wasukuma, Wairaqw, Wamang’ati, Watindiga na Wasandawe, kwenye eneo hilo la katikati na kaskazini magharibi mwa nchi yetu.
Wanyisanzu ambao wanatokea mbari ya Kibantu, si wengi sana kwa idadi, kwa hiyo si moja ya makabila makubwa hapa nchini.
Naamini kuna baadhi yenu Wajadi hamjawahi kuwasikia, lakini wapo na wana mambo yao. Kimsingi wao ni wakulima, japo kwa uchache hufuga pia wanyama kama mbuzi, kondoo na kadhalika.
Wao hulima ufuta, mtama na mahindi, yakiwa ni baadhi ya mazao wanayoyategemea zaidi kwa chakula.
Maziwa na samaki wakavu ndivyo vitoweo vyao vikuu, vinavyotumika kwa chakula hicho kitokanacho na mazao hayo.
Eneo wanalopatikana lina utata mkubwa wa upatikanaji wa mvua, huku likikabiliwa na vipindi vya ukame wa hapa na pale. Kutokana na hali hiyo, ndugu zetu hawa ni mahodari kwa matambiko na uganga wa kutengeneza mvua, tangu siku nyingi zilizopita.
Kuzalisha mvua kwao ni kama uzao wa kiumbe mpya, hivyo kwenye mbinu hizo za kusababisha mvua, jinsia huthaminiwa sana.
Kwao, uzao wa kitu chochote, si kwa binadamu tu, hutegemea jinsia. Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa, wanazingatia sana ujinsia katika kutenda mambo yao.
Japokuwa kwenye ujinsia huo kama ilivyo kwa makabila mengi, hakuna usawa, kama inavyofahamika upande mmoja huukiritimba mwingine.
Utengenezaji mvua kwao hutekelezwa kwa utoaji sadaka za kuchinja wanyama kama kondoo, ambao ni matoleo ya kafara kwa mababu wanaotarajiwa kujibu kwa kuleta mvua.
Mambo hayo ya kuamini ujinsia kwao, huvuka hata kwenye vitu vya kawaida sana, mathalan, uwashaji moto kwa kutumia vijiti. Kile kisuguacho chenye kitundu ili kutoa mwako, huchukuliwa kuwa dume na kisiguliwacho jike.
Uwashaji moto wa aina hiyo, kwa ajili ya kuchoma nyama ya kafara ya mnyama wa sadaka ya kuomba mvua, huambatana na utamkaji maneno ya kuomba mizimu ijibu maombi.
Nyumba ya asili ya Wanyisanzu
Kwa imani yao, ushirikiano wa jinsia ya kiume (mtenda) na ya kike (mtendwa), pamoja na nguvu za mizimu, huleta matarajio yanayotazamiwa.
Huo ni ushirikiano wa nguvu mbili za kijinsia na moja ya kimizimu, inayoidhinisha kinachotakiwa kutokea kwa ushirikiano wa zile jinsia mbili.
Japokuwa ni jinsia ya kiume ndiyo inayoonekana kutaka ukiritimba, kwenye kabila hilo lililoelemea kwenye uzao wa kikeni.
Misigano ya kutafuta nguvu baina ya jinsia hizo mbili, hutokea kwenye mambo mengine si kwenye yale mambo ya kutengeneza mvua, ambapo kila moja hukubali nafasi yake.
Kufanikiwa jambo lolote kwao, ni lazima kutegemee jinsia mbili, hakuna linalowezekana kutendeka kinyume cha hivyo.
Pamoja na kabila hili kutofahamika na wengi, lakini ni maarufu si kwa mambo hayo tu niliyoyaeleza, bali pia lina ufanisi na utajiri mkubwa wa mambo ya uganga.
Kutoka katika kabila hili kuna waganga wenye uwezo mkubwa wanaojitofautisha na ulaghai, si kama ilivyo kwa baadhi ya waganga wanaozingatia maslahi yao na si kutimiza matarajio ya wenye shida.
Tayari tumeshawapigia hodi hawa ndugu zetu Wanyisanzu. Tutaendelea kuchambua kwa kina zaidi mambo yao kesho.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Januari 03, 2009.

Comments