Featured Post

WANYISANZU - 2: KABILA LILILOAMBUKIZA UTAMADUNI



Na Innocent Nganyagwa
NI siku nyingine tena ninapokukaribisha kwenye mambo yetu ya mila, utamaduni na desturi zetu Waafrika na Watanzania kwa ujumla. Leo tunaingia kwenye sehemu ya pili ya ziara yetu kwa ndugu zetu Wanyisanzu, ambao tulianza kuwatembelea jana.
Nikukumbushe kidogo japo kwa ufupi, baadhi ya mambo tuliyoyaona kuhusu ndugu zetu hawa, kwenye sehemu hiyo ya kwanza. Kama ulikosa sehemu hiyo, basi utaweza kwenda nasi sawa baada ya muhtasari huu, tutakapoendelea kutokea pale tulipoishia. Hawa Wanyisanzu wako zaidi mkoani Singida, kule Iramba, eneo la Kirumi linalopakana na Maswa, Meatu, Mbulu na Karatu.
Hapo walipo wanatangamana na Wasukuma, Wairaqw, Wamang’ati, Watindiga na Wasandawe. Huo ni upande wa katikati kidogo, kwa kuelekea kaskazini magharibi mwa nchi yetu.

Wanyisanzu ambao ni Wabantu, si miongoni mwa makabila makubwa hapa nchini, kwa hiyo ndugu Mjadi kama hujalisikia kabila hili, usishangae. Lakini wapo na wana mambo yao ya kuvutia kuyafahamu, wao ni wakulima, mazao yao yanajumuisha ufuta, mtama na mahindi.
Lakini pia wanafuga, wanapendelea maziwa na samaki wa kukaushwa kama mboga.
Mfumo wao wa kuishi na kujitosheleza kwa chakula, ni kutokana na eneo walilopo, ambalo lina hali isiyotabirika kwa vipindi vya mvua na ukame.
Mazingira ya hali ya hewa ya eneo lao, yamewapelekea wawe mafundi wa kutengeneza mvua. Hufanya hivyo kwa kutumia waganga na matambiko ya kuomba mvua, wakitekeleza hayo kwa kutegemea mizania ya kijinsia.
Wao wanaamini kuwa, hakuna chochote kinachoweza kuzaliwa bila jinsia, kwa hiyo, kwao, chochote kinachozalishwa lazima kitokane na jinsia mbili – ya kike na kiume.
Imani hiyo si kwa viumbe hai tu, hata kwa mambo yanayotengenezwa na binadamu.
Licha ya kuzingatia jinsia, lakini kuna mivutano, ambapo kama kawaida jinsia dume hutaka kuikiritimba ya kike.
Kwenye mambo ya utengenezaji mvua kwa matambiko, huchinja wanyama hususan kondoo na kutoa kafara kwa mababu, ambao hujibu kwa kuleta mvua.
Matambiko, huambatana na maneno ya ibada za kijadi, lakini ili utekelezaji huo ufanikiwe, lazima kuwe na nguvu ya utatu.
Najua unaweza kustuka, maana utatu unaweza kuwa umeusikia kwenye imani fulani za kigeni, lakini hata wao wana nguvu ya utatu.
Kwamba, jinsia mbili na mizimu huleta matokeo tarajiwa, hasa katika kutengeneza mvua.
Lakini, licha ya hizo jinsia kuvutana kwenye mambo mengine, zinaheshimiana kwenye matambiko, hasa yale ya kutengeneza mvua na kila moja hukubali nafasi yake.
Uhodari wao mwingine ni kwenye mambo ya uganga, ni kabila lenye waganga wenye uwezo mkubwa usio wa kibabaishaji. Kwa kifupi hayo ndiyo tuliyoyaona jana.
Sasa basi tuendelee mbele kutokea hapo. Ni kwamba, licha ya wale majirani niliokutajia awali wa Wanyisanzu, lakini pia zamani, Wahdazabe walikuwa majirani zao wa karibu.
Hao Wahadzabe hawakuoleana na makabila mengine, isipokuwa hawa Wanyisanzu, ambao walifika kwenye eneo hilo tangu mwanzoni mwa karne ya 18, katika kule kujitanua kwa Wabantu kwenye ukanda wa kusini mwa Afrika.
Wanyisanzu ndiyo wanaowafahamu vyema Wahadzabe, kuliko makabila mengine, hata watalii na wavumbuzi wengi wa mambo ya miji ya kale waliwatumia wao ili kusikilizana na hao Wahdazabe.
Kutokana na jambo hilo, kuna Wahadzabe wenye mchanganyiko wa damu na Wanyisanzu, japo kwa asilimia ndogo tu ya idadi.
Ufundi wa uganga na utengenezaji wa pombe, waliutoa kwa Wanyisanzu, ambao walionekana kuwa na maarifa mengi yaliyoyavutia makabila mengine.
Kwa ujumla wao Wanyisanzu, waliambukiza utamaduni wao kwa makabila mengine yaliyowazunguka, japo eneo lao lilionekana dogo, hasa kutokana na kutangamana na makabila mengi ya jirani nao.
Mathalan, hata yale mapambo ya kutoga masikio yanayopatikana kwa Wahdazabe, wameyatoa kwa Wanyisanzu.
Hata ufundi wa mambo ya uganga, waliutoa kwao, kama tulivyoona pale awali kuwa wao ni mahodari katika fani hiyo.
Lakini lazima ufahamu kwamba, wakati huo hawa Wanyisanzu ambao ni Wabantu, walipoingia na kujitanua kwenye eneo hilo, ndipo madini ya chuma yalipoanza kutumika kutengenezea silaha.
Kwa hiyo, licha ya sasa Wabantu kuonekana ni wapole kulinganisha na watu wa mbari nyingine, lakini ni wao ambao awali walikuwa wapiganaji hodari kutokana na zana hizo mpya, kwa wakati huo.
Hizo ni zama za kati ya zile za mawe na chuma, ambapo kwa walioweza kutumia zana za chuma walikuwa na nguvu kubwa ya kushinda kivita.
Kwa hiyo haishangazi kwamba, wao walikuwa katikati ya makabila mengi, huku wakiwa kabila dogo, lakini hawakuweza kugubikwa.
Kwa hiyo, ushawishi ni moja kati ya mambo ambayo yaliwezesha makabila ya mbari nyingine. Kuyaiga yale ya mbari zenye nguvu kama ambavyo tohara ilivyoigwa na baadhi ya makabila jirani na Wanyisanzu.
Wabantu wengi kwa asili hutahiri, tofauti na jamii za mbari nyingine.
Katika eneo lao wanalopatikana huko Kirumi, kuna michoro, japo wenyewe wanadai kutohusika nayo, lakini kwenye mapango ya mawe inakopatikana michoro hiyo, ndipo ilikuwa sehemu ya kujificha ya shujaa wa Kirumi ambaye anasemekana alikuwa Mnyisanzu. Huyo aliitwa Nyakidarama, mmoja kati ya watu maarufu kwenye historia ya kabila hilo.
Lakini, kwa kuwa kwenye eneo lao kuna makabila mengine pia yaliyojihusisha na michoro ya mapangoni, si ajabu kuwa hata miongoni mwao kuna ambao wanasema kuwa michoro hiyo haihusiani na kabila lao. Wanyiramba pia, ambao ni majirani zao, nao wanafahamika sana pia kwa michoro hiyo.
Pia kuzungukana kwenye eneo moja kwa makabila yanayotokea mbari tofauti, ndiko ambako mara nyingi husababisha taswira tata kama ambavyo tutaona kwa Wakamba.
Wabantu kwa asili, lakini wana taswira za makabila ya Kihamitiki. Wanyisanzu wana makundi ya koo zipatazo takriban 12, ambazo koo hizo zote huzijichukulia kuwa ndugu.
Koo hizo huzalisha koo nyingine thelathini, hawa wote huunganishwa kwa kizazi cha kikeni, japo wana muelemeo wa kiumeni.
Nadhani naeleweka, tuliwahi kuona makabila yenye mfumo huo, pia kuna ile hali ya kutambuana kindugu kwa tofauti ya mbinu za utambulisho, ambao niliwahi kuzigusia hapa kwenye safu yetu.
Tuone baadhi ya hizo koo zao na koo tanzu zitokanazo na hizo, kuna Anyampanda wa Kirumi (Anyanzoka – au Wanyanzoka), Anyampanda wa Kinyakambi (Iyindi, Muhai au Mpilimaigulu), Anyampanda wa Anega, Anyampanda wa lgomano, Anyampanda wa Ikela, Anyampanda wa Itiili, Anyampanda wa Ikunguli, Anyampanda wa Matongo, Anyampanda wa Kinyingogo, Anyampanda wa Nyonyela, Anyampanda wa Magemelo, Anyambilu wa Gudali, Anyambilu wa Kinyankunde na Anyambilu wa Azigo.
Nyingine ni Anyambilu wa Mumba, Anyambilu wa Anyankuni, Anyankali wa Ilumba (au Iyaniko), Anyankali wa Ipilinga, Anyansuli wa Kingwele (au Mukoolo), Anyansuli wa Mukilampili (Itimbwa au Ng’wamalaga), Anyambeu, Anyambeu, Anyang’walu, Anyambwa, Anyisungu, Anyambala, Asamba, Anyakumi na Anyikili.
Nchi ya Ihanzu, yaani mahali wanakopatikana ndugu zetu hawa, kuna misimu miwili tu, ‘kitika’ wakati wa mvua na ‘kipasu’ wakati wa ukame. Misimu hii miwili imejigawanya katika takriban nusu mwaka kila mmoja, mvua ziko kati ya Novemba na Aprili hadi Mei.
Kipindi kinachofuata kati ya Juni na Oktoba ni ukame, hakuna mvua, mabadilishano ya vipindi vya ukame na mvua, ndiyo yanayosababisha kilimo kuwa kigumu kwenye eneo hilo. Mara nyingine mvua huweza kuja kwa wingi usiotarajiwa, na kuziondoa mbegu zilizopandwa.
Haiwezekani kulima bustani wala kilimo cha sehemu nyevu, maana kwa asili hakuna mito inayotiririka kwa mwaka mzima. Lakini wao kwa mbinu zao, wameweza kudumu na kuishi kwenye eneo lao la asili lenye hali kama hiyo niliyoitaja.
Kesho tutaona kwa uchache, baadhi ya mambo yao yaliyobakia.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Januari 10, 2009.

Comments