Featured Post

WANYIRAMBA: WALIKWEPA VITA WAKAISHIA KUPIGANA

Nyumba za asili za Wanyiramba.


Na Innocent Nganyagwa
NDUGU zangu, leo tunawaangalia ndugu zetu Waniramba au maarufu kama Wanyiramba. Ndugu zetu hawa wanapatikana mkoani Singida, hasa huko Iramba, ambako wako kwa wingi. Wanyiramba ni Wabantu ambao kwa asili wanatokea pembezoni mwa himaya ya Bahima, magharibi mwa Ziwa Victoria kwenye mpaka wa Rwanda na Uganda.

Kutoka huko, jamii zao za awali ziliingia mkoani Mara miaka 200 iliyopita na kuacha urithi wa majina yao, yanayofanana na yale yaliyoko kwenye makazi yao ya sasa.
Wanyiramba walifika Iramba kutokana na kukimbia vita huko walikotokea, walishapigana na Wakurya na kuwa watani baadaye.
Katika msafara wao wakagawanyika makundi mawili, kundi moja likaelekea kaskazini mashariki, kundi lingine likaenda kusini magharibi.
Kundi la pili lililoelekea kwenye Bonde la Mto Sibiti liligawanyika tena katika makundi madogo mawili, wengine wakaenda kusini mwa Ziwa Kitangiri na wengine wakaenda Karatu.
Wale walioenda kaskazini mashariki, walisogea hadi kwenye uwanda wa milima ya Usambara na Upare. Wakalazimika kugeuza mwelekeo na kwenda kusini magharibi, kupitia eneo la katikati la Kondoa.
Wakaenda hadi pembezoni mwa mpaka na Mkoa wa Iringa, lakini wakalazimika kubadili tena mwelekeo na kwenda kaskazini.
Kilichowafanya wageuze kwa mara nyingine ni kukumbana na wababe wengine wa kivita, Wahehe.
Walikuwa radhi kuzurura ili kutafuta amani, kuliko kupigana na jamii za kibabe.
Kutoka hapo waliingilia kusini na kupitia kwenye eneo la Ukimbu, wakaishi kwa muda maeneo ya Ushora na Usure huko Ukimbu.
Kisha wakaelekea kaskazini zaidi, walikokutana tena na wenzao walioachana nao awali pale Kitangiri.
Lakini pia historia yao nyingine inasema, walitokea mashariki huko Usambara mpakani na Upare wakaelekea kusini na kuishi kwa muda maeneo ya Mkoa wa Morogoro.
Wana kumbukumbu ya makazi hayo kwenye nyimbo zao, kwa kuimba majina kama ‘Munangulu’ lililotokana na kukaa kwa muda huko Uluguruni.
Wakaingilia Ugogoni na kujaribu kwenda tena kusini, iliposhindikana wakaenda kusini magharibi.
Wakapitia Itigi na kukaa Tyumba huko Ukimbu, kutoka hapo wakageuza na kwenda kaskazini zaidi kupitia misitu ya Tyumba na kwenda kuishi kwenye Msitu wa Kungu.
Safari zao hazikuishia hapo, walielekea kaskazini zaidi na kulowea huko Mwalu, kusini mwa Ushora, kisha baadaye wakaenda Mangula.
Muda wote huo walipokuwa wakizurura, hawakuwa na machifu bali viongozi wa muda waliotokana na matukio.
Hadi walipofika uwanda wa Iramba, walikuwa wamegawanyika katika makundi ya koo mbalimbali.
Kila kundi la ukoo likalowea mahali lilipoona panafaa, japokuwa makundi mengine kutokana na kuwa madogo mno, hayana kumbukumbu zinazoonesha mahali yalikofikia awali.
Mengi ya makundi hayo yalilowea eneo la Kisilili, yalipo makazi ya Chifu na mpakani na vilima vya Kinakumi, kaskazini mwa Kiomboi na vilima vya Sekenke.
Baadhi ya koo hizo za Wanyiramba zilizolowea maeneo hayo ni Wanambwa (mbwa) waliolowea Nsimba huko Kisilili, na Wanisungu (upepo) waliolowea Pazu.
Koo nyingine ni Wanankali (jua na chui) waliolowea Kulu, ambayo maana yake ni Ufalme, Wanakumi (nge), waliolowea kwenye miamba ya Nsamile, Wanampanda (kondoo), walilowea ‘Nzuki’ ambayo kwa Kiswahili ni nyuki, kutokana na eneo hilo kuwa na wadudu hao kwa wingi.
Koo nyingine ni Wanambala (kuku), waliolowea Mukiloga kusini mwa Kisilili. Pia kuna Wanishanga (kuku), waliolowea eneo lililopewa jina la kiongozi wao hapo Kisilili.
Koo nyingine zilizosalia ni Wanangili (nungu) waliolowea Kimaguwe, eneo la kati ya Kiomboi na Ruruma, Wanalilya (kilio) waliolowea Mangola karibu na miamba ya Nkuu.
Kuna makundi mengine yaliyolowea hapo Iramba lakini hayakuja kwa ile misafara ya kuzurura.
Hao ni Wanakili (simba) waliotoka magharibi na kulowea Mwagala, Wanambala nao pia walitokea magharibi, kama Wammbeu (mbegu) ambao nao walitoka magharibi.
Hao Wammbeu ndiyo ambao wanashikilia Uchifu wa sasa wa Wanyiramba. Kundi la mwisho ambalo ni dogo kabisa ni Wazigo (Zigua), waliotokea magharibi mwa eneo la Wazigua.
Ndugu zangu, tutambue kuwa majina yaliyo kwenye mabano ni alama za majina yanayotumika kutambulisha koo hizo.
Kama ambavyo tulivyoona hapo mwanzoni, ndugu zetu hawa hapo awali hawakuwa na machifu. Lakini baadaye walikuwa na mfumo huo wa uongozi, baadhi ya machifu muhimu wa kabila hilo wanaokumbukwa ni Makala, Shango, Mizuzu, Kitandu, Nganguli, Leme, Mulumba na dada zake Nsili na Shamba.
Wengine ambao hawakuwa na nguvu sana ni Gelema, Magili, Kimalangombe, Nzoe, Shila na Kingu Kingu. Huyu wa mwisho alipokewa utawala na Mazila, ambaye naye baadaye alipokewa na mwanaye Lutheri baada ya kufariki.
Kama nilivyowafahamisha mambo ya ndugu zetu hawa yanataka kuyafukua kweli kweli, maana yamejificha.
Kutokana na hali hiyo, hata simulizi za machifu wao ni adimu kiasi kupatikana, ila wapo wawili ambao kuna kumbukumbu nzuri ya simulizi zao.
Hao ni mtu na mwanaye, Mizuzu na Kitandu, ambapo Mizuzu alikuwa akipata dawa za kijadi kutoka kwa mmoja wa machifu wa Unyamwezini wa wakati huo.
Huyo chifu wa Kinyamwezi aliitwa Limampindi, yaani mtu alimaye jioni. Yule Mizuzu kila mwaka alikwenda kwa Limampindi, kujifunza ufundi wa dawa za kutengeneza mvua na za kulinda watu wake.
Kila mara katika safari hizo alikuwa akiambatana na mwanaye Kitandu, na walipofika huko, wakati Mizuzu akipata mafunzo Kitandu alikwenda kwa mtoto wa Limampindi kumsaidia kuchunga.
Lakini yule Mizuzu akaona kama ametosheka na mafunzo, hivyo basi muda mwingi aliutumia kunywa pombe na mwenyeji wake.
Lakini yule mtoto wa Limampindi ambaye alikuwa rafiki wa Kitandu, yaani mtoto wa Mizuzu, alizifahamu vyema dawa za baba yake na alimfundisha Kitandu walipokuwa wanachunga.
Kitandu akaondokea kuzijua vyema sana dawa zile kuliko baba yake. Kuna siku Mizuzu na Kitandu walipokuwa wanarudi kutoka huko Unyamwezini, mvua kubwa sana ilinyesha.
Kuna mto waliopaswa kuuvuka ambao ulijaa sana kutokana na mvua hiyo, Kitandu alipotaka kujua kutoka kwa babake watavukaje hakuwa na jibu.
Mizuzu alisema kuwa watasubiri mpaka kina cha maji kipungue. Kitandu alipingana na jambo lile, akabainisha kuwa watachelewa.
Akachukua mkuki wake na kuchoma kwenye yale maji, yakagawanyika pande mbili na kuacha njia, wakavuka.
Najua ndugu yangu unaweza kushangaa, maana mambo haya ya kugawanya maji na kupita katikati yake, wengi wenu mmeyasikia kwenye maandiko ya imani za kigeni.
Lakini nataka nikuhakikishie kuwa, mambo kama haya yalikuwepo hata kwenye jadi zetu, mengine bado yapo hata sasa unaposoma simulizi hii ya Wanyiramba.
Binafsi kutokana na kupenda kuwa mdadisi, mara kadhaa nikitajiwa eneo lenye maajabu ya aina hiyo, basi huwa najitahidi kufika ili nishuhudie mwenyewe.
Kule kwetu Iringa nimeshawahi kwenda kutembelea maeneo mawili matatu, ambayo bado yana mambo hayo ya maajabu ya kijadi hata sasa.
Basi kama Kitandu kugawanya mto ni maajabu kwako, soma haya mengine yanayofuata.
Ni mambo tu ya nguvu za kijadi, kama tutavyoona tutakapowatembelea Wazigua na Wasambaa.
Yule Kitandu na babake walipovuka mto walikabiliwa na msitu, na kwa mbali mbele yao kulikuwa na Wamaasai wanawaelekea.
Kama ilivyokuwa mwanzoni, Mizuzu hakuwa na ufumbuzi, Kitandu akaonesha ubingwa wake wa dawa za kijadi.
Alichukua udongo na kuufinyanga katika umbo la pembe ya ndovu, akapuliza pembe ile ya bandia.
Baada ya kufanya hivyo walichokiona mbele yao si Wamaasai tena, bali msafara wa wanyama wa msituni waliopita kwenda mwelekeo mwingine siyo ule waliokuwa wao, yaani walipishana nao.
Tangu hapo Mizuzu hakupendezewa na uwezo huo wa mwanaye, maana ulikuwa ni tishio kwa Uchifu wake.
Lakini hakukumbuka kuwa, wakati yeye anaendekeza pombe, Kitandu alitumia muda wake vyema kujifunza dawa kwa mtoto wa Limampindi.
Alianza kumfanyia hila mwanaye huyo, kwanza alimlaani ili apotelee msituni, ikashindikana.
Akajaribu kumlaani ili apotee wakati wa usiku, ikashindikana pia, alipoona mambo hayamwendei vyema akajaribu hila nyingine.
Siku moja akaamua kumtumia nyoka amgonge na kumuua, lakini Kitandu naye alimtuma mwanaye aliyeitwa Makala akaleta aina ya nzige wanaoitwa ‘malimbo’ hawa walimuuma yule nyoka aliyeitwa ‘nkungishaka’ mpaka akakimbia.
Mvutano huo haukumalizika vyema, kwani Kitundu alimvunja mguu babake huko msituni, kisha baadaye akamkata kichwa. Halafu akajenga kibanda kidogo na kukiweka kichwa hicho, ambacho kiliitwa ‘turnbika’ ambapo chumba kilichowekwa kichwa hicho kiliitwa ‘kikungu’.
Sehemu hiyo ya kibanda ikawa ndiyo ya kuabudia, hata mwaka wao mpya uliotegemea hesabu za mzunguko wa mbalamwezi, ulihesabiwa kuanzia wakati ambao kibanda hicho kilijengwa.
Kwa wakati huo, koo iliyotawala ilitoa kiapo cha kutooana na Wanangili kutokana na matukio hayo ya Kitandu na babake Mizuzu.
Tukiachana na simulizi hiyo ndogo ya Kitandu na babake, ni kwamba kusongamana kwa Wanyiramba kutokana na kuzaliana kuliwafanya baadhi yao wajisogeze Kiomboi, Kinisungu, Ulemo na Kinampanda.
Katika maeneo hayo kuna sehemu ndogo ndogo zinazofahamika kwa wakazi wenyewe tu waliolowea hapo.
Mathalan, Wanisungu waliishi kwenye maeneo yaliyo ndani ya Kisungu, hawa walikuwa wanapenda sana kupigana dhidi ya koo nyingine.
Najua utashangaa, kwamba watu waliozunguka mwendo mrefu kukimbia vita wakaishia kupigana wenyewe kwa wenyewe.
Labda ni kwa kuwa walifahamiana vyema nguvu zao, kulinganisha na wale wababe wa makabila mengine. Baadaye walikwenda kuishi Ng’iti wakitokea Mpanzu.
Wanambala waliishi katika eneo dogo la Monele huko Uwanza. Hawa walipigwa na wale Wanisungu ikabidi wakimbilie Mukinga.
Wanisungu kwa muda huo walimtegemea sana nabii wao Kwanwaga, basi Wanishanga nao walipokuja kusini mwa Uwanza kutoka Kisilili, Wanisungu waliwapiga na kuwafukuza. Wakakimbilia upande wa mashariki, eneo lililokuwa mbuga na kulowea nchi ya aliyekuwa Chifu Mtali.
Waliofuata kuonja kipigo cha Wanisungu ni Wanangili, ikabidi wakimbilie tena nchi ya Wakimbu na kuishi Usule. Lakini ukoo uliokataa kupigwa kirahisi ni Wanankali, hawa walipigana mno na Wanisungu.
Wakati huo Wanisungu walikuwa wanaongozwa na jemedari wa vita aliyeitwa Shuluwa, mapambano hayo yalivuma kwa miaka mingi.
Damu nyingi sana ilimwagika kutokana na mapigano hayo, sehemu ambayo mapambano yalikuwa makali ni Ruruma.
Eneo hilo lilikuwa na mto mdogo uliojaa damu kutokana na mapigano hayo, koo hizo za Wanankali na Wanisungu ziliendelea kupigana mpaka Wajerumani walipokuja kutawala.
Waniramba, ambao kiini cha makazi yao ni kwenye maeneo ya Iramba inayojumuisha maeneo ya Kisinungu, Ulemo, Kinambwa, Kisilili, Kinikili au Kiomboi, ambako Kinyiramba halisi kinazungumzwa.
Tofauti ndogo ndogo za matamshi ya lugha hiyo kwa Wanyiramba wa Iambi, Isanzu na Ushora, zinatokana na kutangamana na kuingiliana na makabila mengine.
Ndugu zangu, kuna mengi bado tunayoweza kuyachambua kuhusu ndugu zetu hawa, lakini la mwisho kwa sasa ni kumbukumbu ya yule Chifu Kitandu.
Kwenye Kijiji cha Kisana kaskazini mwa Ruruma, wilayani Iramba, kuna kaburi lake karibu na shule ya Msingi ya Kisana huko Kinakumi.
Kaburi hilo limezungukwa na miti iliyopandwa pembezoni mwake, ili kuliwekea alama kwa ukumbusho wa Wanyiramba wote.
Pamoja na Wanyiramba wengi kupatikana huko Iramba, lakini wapo ambao kuna nyakati walikwenda Usukumani kufanya kazi za kuvuna pamba.
Wengine wamelowea Arusha wakijihusisha na shughuli za uvunaji miwa, huko wanapatikana kwa wingi Arusha Chini pembezoni mwa mto Usa.
Ndugu zangu, kwa leo tukomee hapa, tukutane tena kesho tutakapolitembelea kabila lingine kati ya makabila yetu hapa nchini.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Februari 07, 2009.

Comments