Featured Post

WANYAKYUSA: MAJINA YA WATOTO HUMTUKUZA MUNGU

Akinamama wa Kinyakyusa wakiwa wamevaa nguo za asili.


Na Innocent Nganyagwa
NDUGU zangu, leo nawakaribisheni kwenye safu yetu hii ambapo tunawatembelea Wanyakyusa wanaopatikana kwenye nchi yenye neema ya vyakula mbalimbali kama maparachichi, ndizi na matunda mengine matamu.
Wanyakyusa wanapatikana kwenye eneo pana sana.
Ndugu zetu hawa ambao kwa majina mengine huitwa pia Wasokile, Wangonde au Wankonde, jamii zao zinapatikana kuanzia maeneo ya kaskazini mwa nchi jirani ya Malawi hadi kusini mwa nchi yetu huko Mbeya.
Ndugu zetu hawa ambao huzungumza lugha yao ya Kinyakyusa ambayo ni sehemu ya lugha za Kibantu, eneo la nchi yao ndilo linalowapa majina tofauti na tulivyozoea kuwaita.
Tumezoea kuwaita Wanyakyusa, lakini kutokana na nchi yao yenye milima na mabonde inayoanzia Malawi na kupitia Ziwa Nyasa kuwagawanya kwenye pande mbili, hiyo ilisababisha wawe na majina kadhaa.
Wale wanaoishi kuanzia mto wa Rukuru kaskazini, Karonga, huko Malawi, hufahamika kama Wangonde au Wankonde.
Lakini watu hao hao wa jamii hiyo hiyo moja walio upande wa pili wa nchi ya Unyakyusa, yaani maeneo ya Mbeya, hasa katika wilaya za Rungwe na Kyela, ndiyo hufahamika zaidi kama Wanyakyusa.
Lugha ya ndugu zetu hawa ni Kibantu, japo ina miundo tofauti ndani yake, yaani haina ule mfumo wa moja kwa moja kwa lugha hiyo hiyo moja.
Lugha yao inatofautiana kimatamshi na hata silabi zake, na lugha nyingine za Kibantu za jamii wanazopakana nazo.
Ukikuta Wanyakyusa wanaoongea lugha yao kama inavyopaswa, utadhani kama aina fulani ya wimbo au shairi kwa jinsi matamshi yao yanavyotoka.
Japo kwa sasa kuna Wanyakyusa wengi ambao huongea lugha yao kwa kunyoosha matamshi ya silabi, kana kwamba wanaongea Kiswahili.
Maingiliano ya jamii na lugha huathiri lugha nyingi za kijadi na kuzibadili.
Japo si wengi wenu mnaofahamu hivyo, maana hata salamu na baadhi ya majina hubadilika na yakishatumika kwa muda mrefu hukubalika kwa mazoea na kuonekana ya kawaida.
Tukirudi kwenye jamii za Wanyakyusa, hapo zamani wakati wakiwa huko ‘Nyasaland’ kwenye eneo la kandoni mwa Mto Songwe, walifahamika zaidi kama Wangonde.
Lakini upande wa pili wa mto huo walishaanza kuitwa Wanyakyusa, ila utamaduni na lugha zao zilikuwa zinalandana kwa kiasi kikubwa, hali iliyowachanganya hata wageni (wakoloni) waliokuwa wanatawala pande hizo mbili.
Huu upande wa pili ulikuwa chini ya Wajerumani, walioamua kupaita Konde kutokana na kule kufanana kwa watu wa upande huo na ule wa kwanza, uliokuwa chini ya Waingereza.
Lakini kitu kimoja kitakachokushangaza kuhusu ndugu zetu hawa, ni kwamba ukirudi nyuma zaidi kwenye chanzo chao utagundua kuwa wanatokana na Malkia mwenye asili ya Kinubi, aliyeitwa Nyanseba.
Malkia huyu alipinduliwa na mpiganaji mmoja na kundi lake la wafugaji wazururaji, kisha wakahamisha utawala kutoka kikeni kwenda kiumeni kwa maana ya Wafalme badala ya Malkia.
Lakini hiyo haikusaidia kufuta nguvu na uwakilishi wa kikeni, ndani ya jamii za baadaye zilizozalisha kabila la Wanyakyusa.
Mfumo wao wa utoaji majina ya watoto katika ujadi wao wa zamani, ni kwamba mtoto wa kiume huchukua jina la ukoo wa mama na wa kike la ukoo wa baba, hiyo ilifanyika ili kuendelea kulinda ile hadhi ya kikeni kwa vizazi vya baadaye.
Pia kuna mambo mengine kuhusiana na majina ya Wanyakyusa, ngoja nikutaarifu kitu kinachoweza kukuchekesha kidogo.
Kama ni mgeni kwenye nchi yao ya Unyakyusa, unaweza kustaajabishwa na utopevu na ufuasi mkubwa wa imani za kidini.
Hata ukipanda mabasi yanayoelekea mkoani Mbeya, basi burudani ya nyimbo itakayotawala ndani ya vyombo hivyo vya usafiri iwe kwa sauti au taswira, ni nyimbo za kidini.
Endapo mhudumu wa basi atajaribu kuweka aina nyingine ya burudani, basi huenda akakumbwa na malalamiko ya abiria wanaosafiri.
Lakini kama ukifikiri kuwa utopevu huo wa imani umeanza siku za karibuni, utakuwa umekosea sana.
Ukitaka kuthibitisha utopevu wao wa kiimani, basi tazama maana ya majina mengi kati ya yale wanayopewa watoto wa Kinyakyusa.
Ngoja nikutajie baadhi ya majina hayo na maana zake kwenye mabano, Ambidwile (Mungu ameshawishi), Ambilikile (Mungu ameniita), Ambokile (Mungu ameniokoa), Ambonisye (Mungu ameniponya), Andalwisye (Mungu ameniongoza), Andondile (Mungu amenihitaji) na Andongwisye (Mungu ameniongoza).
Mengine ni Andwele (Mungu amenileta), Tuponile (Tumeokolewa) na Tusajigwe (Tumebarikiwa).
Majina yote hayo ni ya kiume isipokuwa kwa hili la mwisho, ambalo mara nyingi kwa ufupisho huitwa Tusa. Wasichana wengi wa Kinyakyusa wenye jina hilo huitwa hivyo.
Tukirudi kwenye zile jamii zao za awali zilizogawanywa na mito na majina, wale walioitwa Wangonde waliokuwa kusini walitangulia kimaendeleo.
Hawa waliokuwa upande wa pili waliojulikana zaidi kama Wanyakyusa, kwanza waliishi kwenye vijiji vidogo vidogo huku wakiwa na tawala nyingi ndogo ndogo za Kichifu, zilizotawanyika kwenye eneo lao.
Lakini licha ya kuwa na tawala nyingi ndogo ndogo, waliweza kuwashinda maadui waliowashambulia kwa nia ya kuwatawala, maadui hao walitoka kwenye makabila ya Wasangu na Wangoni.
Katika eneo la nchi yao lenye uwanda wa milima, Wanyakyusa waliwahi kuwa na muingiliano wa kijamii na Wakinga waliosambaa upande wa magharibi wa nchi yao wakiwa wahamiaji.
Magharibi mwa nchi ya Ukinga, ndipo nchi ya Unyakyusa ilipopakana nao.
Mchanganyiko wa jamii hizo mbili ndiyo uliozalisha baadhi ya kanuni na mila, zilizowahusu machifu wa awali wa Kinyaksyusa hasa kwa zile himaya nyingi ndogo ndogo nilizozitaja hapo awali.
Watawala hao waliishi katika hali ya kujitenga, walikuwa na nguvu za kimiujiza lakini pia walidhibitiwa upeo wa mamlaka yao na mabaraza ya utawala.
Kama mtawala akizeeka sana au akiumwa mno, ili kuepusha himaya anayotawala isikumbwe na mkosi utakaosababisha kukosekana kwa mvua na mavuno bora, basi aliuawa kwa kunyongwa na hao wajumbe wa baraza lake.
Nitakuja kuwaeleza mauaji kama hayo ya Machifu wakati nitakapowasimulia mambo ya ndugu zetu Wanyamwezi na mfumo wao wa utawala.
Mfumo huo unalandana sana na mfumo huu na hii haishangazi, maana Wanyamwezi nao ni Wabantu kama hawa Wanyakyusa tunaowazungumzia leo.
Kama ambavyo huwa tunaainisha mara nyingi kwenye safu yetu, kwamba makabila au jamii zitokanazo na mbari moja hulandana kwa mambo mengi.
Basi tukiendelea na mambo ya wale Machifu wao, ni kwamba kwenye baraza lao la utawala walikuwa na washauri lakini hawakupaswa kuwa na undugu wowote na Chifu, ili iwe rahisi kwao kumdhibiti.
Licha ya huu mfumo wao wa utawala, lakini pia Wanyakyusa waliishi kwenye jamii yenye mafungu ya madaraja ya umri.
Japo mengi ya mafungu hayo ya jamii yalitokana na koo tofauti tofauti si koo zenye undugu.
Ukiuangalia mfumo wao kwa juu juu, unaweza kuhisi kama walikuwa na jamii dhaifu.
Lakini ukweli ni kuwa jamii yao iliweza kujilinda vyema, ndiyo maana hawakuwahi hata kufanywa watumwa japo kwenye maeneo ya Konde na Karonga kulikuwa na utumwa.
Nikukumbushe tena kuwa utumwa si lazima uwe ule wa wageni dhidi ya wenyeji kama Waraabu walivyowafanyia babu zetu.
Zamani kulikuwa na utumwa hata ndani ya jamii na makabila mbalimbali, kiasi kwamba kuna baadhi ya jamii zilivikwa sifa ya utwana.
Tukiendelea na ndugu zetu Wanyakyusa, wao ni wakulima mahodari wa mazao ya aina mbalimbali kwa zamu za misimu yake.
Baadhi ya mazao hayo ni maharagwe, ufuta, mtama, viazi vya aina mbalimbali, huku migomba ya ndizi ikichukua sehemu kubwa ya kilimo chao.
Zamani kulima kutokana na mfumo wao wa jadi lilikuwa ni jukumu la baba na wanawe wa kiume, au tuseme kuwa kulima ilikuwa ni shughuli ya wanaume.
Mazao hayo hutumika kwa chakula, kutengenezea pombe na hata kukirimiana pamoja na kuuzwa.
Kwa kuwa kilimo kilikuwa jambo la msingi, umri haukuwa sababu ya kukwepa jukumu hilo hata kama mtu akizeeka, labda pawepo sababu nyingine itakayomfanya ashindwe kabisa kulima.
Kutokana na kujizoesha sana kilimo na neema ya kupata vyakula vinavyotokana na mavuno, ilikuwa vigumu sana kwa Wanyakyusa kuhama au kuondoka eneo lao la asili linalowapatia neema hiyo ya vyakula walivyovizowea.
Na kilimo kilikuwa muhimu sana kwao, basi kila msimu wa mvua unapoanza walikusanyika kwa Chifu wao aliyeiita mvua.
Waliamini kuwa hata kama msimu wa mvua umewadia, lakini ili ianze kunyesha ni lazima ikaribishwe kwa kuitwa na Chifu.
Mathalan, wakazi wote wa himaya ya Chifu Kyungu walikusanyika Chikungu kwa Chifu wao, kwenye tambiko la mvua.
Watu hao hawakutakiwa kuwasha moto majumbani mwao asubuhi hiyo ya tambiko la kuita mvua.
Wote walipaswa kusubiri ule moto unaowashwa kwenye tambiko ili ugawanywe nao wawashe moto kutokana na moto huo.
Haya ndugu zangu, bado mengi ya kuzungumzia kuhusu ndugu zetu hawa, lakini kwa leo tuishie hapa katika awamu hii ya kwanza baada ya kuwapigia hodi.
Tutaendelea tena na simulizi za Wanyakyusa kesho.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Juni 20, 2009.

Comments