Featured Post

WAKIMBU-2: WALIPORWA HIMAYA KWA KULA MABOGA


Na Innocent Nganyagwa
KARIBUNI kwa mara nyingine tena kwenye safu yetu ambapo bado tuko kwenye eneo la makabila yanayotofautiana na mengine kati ya makabila kadhaa tuliyowahi kuyatembelea awali kwenye safu hii.
Leo tunaingia katika sehemu ya pili ya simulizi za Wakimbu, kabila ambalo liko kwenye eneo lililomega mikoa sita kwa sasa, lakini halikugubikwa na makabila makubwa ya mikoa ambayo maeneo yake yamemegwa.

Hiyo ndiyo tofauti ya kimsingi niliyoitaja awali, ya makabila yanayopatikana eneo hilo na yale mengine tuliyowahi kuyatembelea.
Labda nikukumbushe ndugu kama hukuwa nasi kabla hatujawapigia hodi Wakimbu, tuliwatembelea Wanyiramba ambao nao wako kwenye eneo hilo hilo. Bado hatujawatembelea Wanyisanzu kwenye eneo hilo.
Ni makabila yenye muingiliano wa namna fulani, maana tutakapokuwa kwa Wanyisanzu tutakumbana na fungamano za Kinyiramba na za Kikimbu.
Kufika kwa Wanyiramba tukakumbana na fungamano za Kikimbu na hata baada ya kuingia kwa Wakimbu, tumekumbana na fungamano nyingine japo hizi za sasa zinatokana na maeneo waliyoyamega ili kuwa na nchi ya Ukimbu.
Fungamano hizo ni za Kisangu na Kibungu, makabila yaliyoko maeneo mkabala na mpaka wa eneo la Wakimbu ambayo tutayaona baadaye.
Basi sasa tuendelee kutathmini mambo ya hawa ndugu zetu Wakimbu, nikukumbushe kuwa ndugu zetu hawa wako kwenye eneo lililo katikati ya mikoa ya Singida, Tabora, Iringa, Katavi, Songwe na Mbeya.
Eneo hilo linaanzia Sikonge, kupitia Uyuyi mashariki mwa Tabora, Igaluli (Igalula), Tura, Kizengi hadi Singida magharibi na Manyoni.
Kwa upande wa mikoa ya Songwe, Mbeya na Iringa, eneo lao linaanzia Idodi, Pawaga, Mbarali, Chunya hadi huko Mpanda mkoani Katavi.
Tuliona kuwa walikuja eneo hilo kwa mafungu, wakitokea kaskazini zaidi mwa nchi yetu.
Kundi lao la kwanza kuingia hapo ni Wanyisamba, walioingia kutokea upande wa Unyangwila, yaani Ugogoni.
Wakaanzisha himaya ya Wikangulu chini ya uongozi wa Mbela, aliyewagawia nduguze pia maeneo ya kuweka himaya zao.
Nduguye Magulunjega alianzisha himaya ya Mwendo huko Lukwati, wa pili alianzisha himaya ya Mweli katika eneo lenye vilima virefu la Igululilu, himaya ya tatu ilikuwa ya Ilasi.
Himaya hizo zilizokuwa ndani ya eneo pana la Ukimbu litokalo Chunya hadi Sindiga kwa upande mmoja, pia Iringa hadi Mpanda kwa upande wa pili, zilizaa himaya nyingine.
Mweli alianzisha himaya ya Kasekela, himaya ya Mwendo ikasababisha himaya nyingine ya Isote na Ilasi alianzisha himaya nyingine ya Nkila.
Himaya nyingi kati ya hizo ziligawiwa kwa maridhiano, hata wageni wa jamii na makabila mengine walimegewa sehemu za pembezoni.
Hiyo ilisaidia kuhifadhi ukubwa wa eneo la Ukimbu, ambalo hata hivyo awali lilipatikana kwa vita.
Wakati Wanyisamba wanaingia mahali hapo waliwakuta Wapantama, watu waoga na wafupi wenye maumbo madogo.
Waliwapiga na kuwanyang’anya eneo na kuhodhi mamlaka kwa kujitwalia ardhi, ndipo walipoanzisha himaya zilizotawaliwa na machifu wao.
Wakalazimika kubadili mfumo wa kurithiana madaraka ya uchifu, ambapo awali watoto ndiyo walirithi.
Lakini kutokana na watoto hao kuuawa kwa kijicho, wakaamua kurithisha watoto wa dada wa machifu. Hapo ndipo Wakimbu ambalo ni kabila la kiumeni, lilipokuwa na mifumo miwili ya kiukoo.
Koo za kawaida zilikuwa za kiumeni, lakini koo za kichifu zilikuwa za kikeni kwa majina ya utambuzi wa koo hizo.
Tulitoa mifano kadhaa ya makabila mengine, ili kubainisha mfumo wa koo za kikeni na kiumeni. Tuliwataja Waluguru, Wazaramo, Wakurya na Wahehe.
Hapo ndipo tulipoishia jana kwenye ziara yetu kwa ndugu zetu Wakimbu.
Sasa basi tukiendelea kutoka hapo ni kwamba, kuna himaya nyingine za wale Wanyisamba, kundi la awali la Wakimbu, ambazo zilitokana na misigano na si kwa amani na maridhiano kama zile tulizoziona pale awali.
Hizo ni pamoja na Ikokolo, Ipito na Ilamba, msigano ulianza baada ya mtu mmoja kutoka maeneo ya Uyumbu aliyejulikana kama Kuti, ambaye alikuwa mfanyabiashara alipopita kwa nia ya kwenda kwenye biashara zake huko Mwera Lindi.
Usishangae, maana wengi wetu tunadhani kuwa kutokana na vyombo vya usafiri kuwa vingi kwa sasa duniani, basi tunasafiri umbali mrefu kuliko watu wa zamani.
Lakini ukweli uko tofauti, zamani watu walisafiri na kutembea kwa maili nyingi hata kama iliwachukua siku nyingi. Siku tukipata fursa hapa kwenye safu yetu, nitawadokeza jinsi ambavyyo vizazi vya Kiajemi na Kishirazi vilivyoko Mashariki ya Kati na Arabuni, vilivyotoka Yemen na pembezoni mwa Afrika.
Kisha watu wa jamii hizo wakaenda sehemu za Iran na Iraq, pamoja na Aussian ambako kwa sasa kunajulikana kama Saudia.
Kutoka kule wakazunguka na kwenda Ngazija na baadaye kuja tena pwani ya Afrika Mashariki, wakakamilisha mzunguko wao kwa kufika tena pembezoni mwa Afrika, huko Benadir, Barawa, Somalia.
Ni historia ya kina, ndiyo maana makabila kama Wairaqw wanatokea Iraq, kule kwa Saddam ambako zamani kulijulikana kama Messopotamia.
Wahehe ni mchanganyiko wa Wahabeshi, Wangazija na Wabantu, wakati Wadigo ni Wagiliama, jamii ya Wasomalia wa pembezoni karibu na Kenya.
Tuachane na hayo kwa sasa, tuendelee na hawa Wakimbu kwanza.
Basi katika safari mojawapo, Kuti alipofika Igululilu katika sehemu iitwayo Mbaraga, aliweka kambi ya muda mrefu.
Kwa bahati mbaya akafariki, lakini hakuweza kuzikwa mahali pale alipofia maana alikuwa ni kiongozi wa kigeni.
Wafuasi wake walipotaka kumzika, Chifu wa pale aliwakatalia, wakakaidi maagizo yake na kumzika, yule Chifu akaghadhabika na kuanzisha vita ya kuwaondoa.
Lakini alishindwa, hao wafuasi wa Kuti wakajiimarisha na baadaye wakaenda kujieleza kwa chifu wa himaya ya Wikangulu, ambaye alikuwa Mbela.
Walienda kwake kwa kuwa ukumbuke kwamba hiyo ndiyo himaya kuu iliyozalisha zile nyingine.
Yeye aliwaruhusu wabakie na kuishi mahali pale. Basi kutokana nao ndipo zikazaliwa zile himaya nyingine za Ipoto, Ikokolo na Ilamba.
Sasa turejee kwenye yale makundi ya Wakimbu, maana mpaka hapa tulipofikia tumeona kundi moja tu la Wanyisamba, ambalo kimsingi ndilo lilianza kuingia nchi ya Ukimbu.
Lakini kwa ujumla kulikuwa na makundi manne, kundi lingine ni Wanyitumba waliokuwa na eneo lao la Kipembawe ndani ya nchi hiyo ya Ukimbu.
Hawa waliingia eneo hilo kwa kufuatana na Wanyisamba, walipishana kidogo tu muda wa kufika hapo.
Hao nao walianzisha himaya zao za Igunda, Ilumwe na Nyamnyam. Lakini zamani kabla ya hapo walijulikana kama Wanyampanda, isipokuwa walinyang’anywa himaya kwa hila.
Kwenye karne ya 18, wafanyabiashara kutoka Usagara waliiteka Kipembawe kwa kisingizo kidogo sana. Walipokuja eneo hilo walibeba mbegu za maboga wakawapa wenyeji, kisha wakawafundisha namna ya kupanda maboga hayo.
Lakini waliwapa sharti kuwa maboga yakikomaa wale, lakini wabakize mbegu ili watakaporudi kutoka safari zao za kibiashara wazikute mbegu zao.
Tuseme ni kama waliwaazima tu, lakini wale wenyeji wakanogewa na kula yale maboga kabla hayajakomaa vizuri pamoja na zile mbegu zake, bila kuzibakisha.
Wasagara waliporudi hawakukuta mbegu kama walivyokubaliana, wakadai wapewe nchi kama fidia.
Kutokana na kuwa na silaha bora, mtawala wa Wanyitumba aliisalimisha himaya yake kwa Wasagara waliohodhi mamlaka.
Kuanzia muda huo wakajitambulisha kama Wanyitumba (yaani watu kutoka huko Usagara) na wakaeneza utawala wao hadi Iswangala, huko maeneo ya Sikonge na ndani ya eneo hilo ndipo zile himaya za Igunda, Ilumwe na Nyamnyam zilikuwemo.
Kundi lililofuatia kati ya yale manne ni la Wanyangwila, ambalo Chifu wake alikuwa Mkugansi (Mkuga Nsi – mvumbuzi wa nchi), yaani kwa tafsiri ya jina lake ni ‘Mtu aliyevumbua au kuokota nchi’.
Huyu alikuwa kwenye himaya ya Unyangwila ambayo baadaye ilizaa himaya za Ngulu, Unyanyembe, Kisalusalu, Kihwele, Itumba na Kipili.
Watu wa maeneo hayo wote ni Wakimbu-Wanyangwila. Najua kuna majina mawili ya himaya zao yatakutatiza kidogo.
Nitakufafanulia, Wanyanyembe ambao wengi tunawafahamu kama Wanyamwezi kwa asili ni Wakimbu.
Kabla hata ya Uhuru wa Tanganyika kulikuwa na shirikisho la Ukimbu, ambalo Mwenyekiti wake alikuwa Chifu Haruna Lugusha wa Sikonge.
Huyo alifariki mwaka 2007, akiwa na umri wa zaidi ya miaka 80.
Hiyo ina maana kuwa, kwenye hilo shirikisho lao himaya kama hizo za Unyanyembe na nyingine zilizotokana na vita, au urithi wa uchifu kwa watoto wa machifu zilikuwemo ndani ya shirikisho hilo.
Mathalan, aliyeanzisha himaya ya Unyanyembe na Itetemwa, aliitwa Swetu, mtu ambaye alisigana na kupigana na nduguze.
Ile himaya nyingine ya Kihwele, ambayo najua Wanyalukolo wengi watashtuka kusikia ilikuwa Ukimbu, ufafanuzi wake ni rahisi hasa ukizingatia jiografia ya Uhehe na Ukimbu.
Nadhani tunaelewana, na kwa kumalizia kutathmini makundi yao kuna kundi dogo la mwisho la Wanyikungu ambalo nalo lilitokana na Wanyangwila.
Hawa eneo lao linaishia hadi kwenye msitu wa Wanyiramba, huko Tarafa ya Ndago, mkoani Singida.
Watoto wa Ikugansi, Mnyangwila mwinda tembo pamoja na Wanyangwila wenzie, walipigana kwa sababu ya biashara ya ndovu.
Kisha walihamia Usumbwa na kuanzisha himaya za Uyogo na Ukuni, walifanya hivyo ili wapate uhuru zaidi wa kuwinda tembo.
Lakini kwa asili wametokea Ukungu kwa Wanyikungu, ambao kimsingi ni Wanyangwila, kundi dogo na la mwisho kati ya makundi yanayounda kabila la Wakimbu.
Simulizi zinanoga lakini nafasi yetu inatubana.
Kwa kuwa yamebakia mambo machache yanayowahusu hawa Wakimbu, yanayojumuisha imani zao, matambiko na rasilimali walizozitegemea kiuchumi, basi tutamalizia simulizi zao wakati mwingine kwa kutazama mambo hayo.
Kama ilivyo kawaida ya miadi yetu, nakusihi usikose kuungana nami kesho ili tutopee zaidi kwenye kina cha ujadi.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Februari 28, 2009.

Comments