Featured Post

WAIRAQW-3: WAGANGA HUWAVUTA VIGOLI KWA ULOZI

Akinamama wa Kiiragw wakiwa wenye mkutano.


Na Innocent Nganyagwa
LEO tunakutana kwa mara nyingine kwenye safu yetu ya mambo ya kijadi ambapo tunamalizia ziara iliyotuchukua takriban awamu tatu kuwatembelea ndugu zetu Wairaqw.
Basi nawakaribisheni tukamilishe tathmini ya kabila hili la Kikushi, watu ambao kwa asili wanatokea mahali palipofahamika kama Messopotamia hapo zamani (kwa sasa ni Iraq).

Kama ulikuwa nami tangu tulipoanza kuwatembelea hawa Wairaqw, nadhani utakuwa umefaidika kwa kufahamu mambo mengi yanayowahusu ndugu zetu hawa.
Tumeona mambo yao kadhaa, ambapo jana tuliona baadhi ya nyimbo zao za sherehe za harusi, maombi na shukurani kwa Mungu kwa mafanikio ya mavuno ya mazao. Pia tuliona juu ya ufundi wao wa kujitengeneza mavazi yao ya asili, zana za kivita na kilimo na ujuzi wa kuhifadhi nafaka kwenye maghala yao ya asili bila kuharibiwa na wadudu.
Kati ya mambo tuliyoyaona ambayo ya kuvutia, ni kufahamu kuwa wanaoitwa Wambulu kwa asili ni Wairaqw waliotengwa.
Maana jina hilo la Wambulu mara nyingi husababisha mhemko wa hisia kali kidogo baina ya jamii hizo mbili zenye asili moja.
Tulifahamishana kuwa Mbulu ambayo kwa sasa ni wilaya, ni jina la Muiraqw wa kwanza kufiwa na mkewe katika mazingira ya kutatanisha. Hivyo basi alihisiwa kuwa na mkosi na ilibidi atengwe, huyu ndiye alienda kuanzisha mji wa Mbulu. Baadaye alifuatiwa na Wairaqw wengine, waliofiwa na wake na waume zao katika hali za kutatanisha pia.
Niliwatahadharisheni kuwa jina hilo la Mbulu inawezekana linatokana na matamshi ya kimazoea tu, lakini pengine kuna jina la matamshi yao ya asili ya Kiiraqw, maana ndugu zetu hawa lugha yao ya Kimessopatamia, ni tofauti sana na lugha za wengine tulizozizoea.
Jina halisi la huyo mtengwa wa kwanza aliyekwenda kuanzisha mji wa Mbulu, kitu kilichosababisha watokee watu wanaojiita Wambulu ni Imboru.
Kwa hiyo, usishangae ukikutana na wenyeji halisi wa huko wakakutajia mji huo kwa jina hilo, pia usishangae nikisema mji wa Mbulu wakati wewe unapafahamu sehemu hiyo kama wilaya. Licha ya wilaya kuwa na mji wake lakini pia kwa lugha yetu ya kijadi ya safu hii, huwa tunatumia matamshi yenye kutupa tafsiri muafaka kijadi.
Mathalan, tukisema nchi ya Wairaqw tunamaanisha eneo linakopatikana zaidi kabila hilo.
Kwa msingi huo huo, hata makabila mengi yamepata majina kutokana na sifa tanzu za jamii zake za awali.
Mathalan, Wahehe tulianza kuitwa hivyo karne ya 18 tulipokuwa chini ya utawala wa Munyigumba.
Huyu ni baba yake Mkwawa aliyeziunganisha jamii za kwetu huko Lilinga (Iringa), katika mapigano dhidi ya maadui wa himaya yetu.
Maneno ya morali wa kivita tunapowavamia maadui tukipiga kelele, ndiyo yalitupa jina la kabila letu.
Kama ulikuwa hufahamu basi napenda nikufahamishe kuwa mimi ni Mhehe, ninayejivunia mno asili yangu.
Ni sawa na Waluguru ambao kiongozi wao wa mwisho aliyewafikisha ilipo nchi ya Uluguru hivi sasa, alikuwa Luguru, yaani mwenye ulemavu wa mguu. Luguru ni Kiguru kwa tafsiri ya Kiswahili, kwa hiyo kuwaita ‘Wa-luguru’ ni sawa na kusema wale wafuasi wa yule mtu mwenye kilema cha mguu.
Au Wameru, jina ambalo kimsingi lilitokana na watu wa kabila hilo kukwea Mlima Meru kukwepa mapigano.
Lakini kiini hasa ya kabila hilo ni jamii ya Varwaa, walioitwa hivyo hapo awali kabla ya kuitwa Wameru. Kurwaa kwa lugha yao ina maana ya kukwea, lakini hadi kufikia sasa kabila hilo linaundwa na mchanganyiko wa jamii za hao Warwaa wenyewe wanaotokea uwanda wa Milima Usambara, Wachagga wa Kimachame, Wapare na Wapalanjo.
Kwa hiyo nadhani unanielewa vyema kuhusu Wambulu, japo tofauti yao na haya makabila mengine yaliyopata sifa za majina tofauti na jamii zao za awali, ni kwamba wao mambo yao mengi bado ni ya Kiiraqw. Hivyo, inakuwa vigumu hasa kuchukuliwa kama kabila kamili, japo kwa huku mijini kuna baadhi yao hujitambulisha kama Wambulu. Lakini ukweli ni kuwa wao ni wale wale Wairaqw kutokea Mbulu, mji wa mtengwa wa Kiiraqw.
Naam, baada ya kueleweshana vyema juu ya jambo hilo, tuendelee na simulizi ya leo kuhusu hawa Wairaqw.
Kama tulivyoona jana juu ya nyimbo zao za harusi, basi nikufahamishe kidogo juu ya ndoa zao.
Ndugu zetu hawa wana ndoa za aina kama tatu hivi, ambapo aina ya kwanza ni kwa familia mbili za wanandoa kukutana na kupanga kuwaozesha vijana wao sanjari na kiwango cha mahari na utaratibu wa sherehe husika.
Aina nyingine ya ndoa ni ile inayotokea kwa binti ‘kutekwa’ na kijana aliyempenda, tuliwahi kuona aina hii ya kuoana kwenye baadhi ya makabila tuliyoyatembelea siku zilizopita.
Utekaji huu wa kumvizia msichana njiani unaofanywa na marafiki wa mtekaji kwa maagizo yake, mara nyingi haukufanywa na watu wa kawaida. Maana kama unavyoona, ni kuridhisha matakwa ya upande mmoja zaidi hata kama yule binti kimsingi hajampenda huyo anayemteka.
Uoaji huo mara nyingi ulitumiwa na watu waliohofiwa kwenye jamii zao, mathalan wanaweza kuwa viongozi wa madaraja mbalimbali au waganga.
Binti anayesombwa kwenye ndoa ya aina hii akishajamiiana tu na yule aliyeagiza asombwe, basi hachukuliwi tena kuwa na hadhi ya msichana bali ni mwanamke. Maana hadhi yake inakuwa imeshavushwa daraja kwa mbinu hiyo, nadhani unanielewa nikikueleza hivyo.
Lakini ndoa hizi za kutekana baadaye ziliachwa na watu wengi, waliobaki kuendelea na mchezo huo ni waganga wa mvua.
Na hata hao hawakutumia nguvu bali kwa kutumia uwezo wao wa uganga, kwa kufanya ulozi wa kumwagia matone ya mafuta au kumgusa binti kigoli na mafuta hayo. Naye humfuata kwa hiari yake, kutokana na nguvu ya ulozi wa ile dawa ya kijadi iliyochanganywa kwenye mafuta hayo.
Lakini ndoa iliyo tofauti zaidi, ni ile ambayo familia isiyo na mtoto wa kiume inapomnunua binti na kukodi wanaume wa kujamiiana naye ili azae watoto.
Ndoa hiyo ambayo kwa jina jingine hujulikana kama ‘ndoa ya kivuli’ hutumika zaidi na familia ambazo licha ya kutokuwa na mtoto wa kiume, lakini pia labda baba ameshafariki dunia.
Familia husika hufanya hivyo ili kujiongezea uzao, maana watoto watakaozaliwa si wa wale wanaume wanaojamiiana na yule binti kwa kuwa wao wameshalipwa ujira wao kwa kazi hiyo.
Kama hujawahi kusikia mambo kama hayo unaweza kushangaa, lakini makabila mengi yanayotokana na mbari ya Kikushi au mbari tanzu zenye mchanganyiko wa Kikushi yana kawaida hiyo.
Wakati tutakapowatembelea Wamaasai kwenye safu yetu, nitawaeleza juu ya tabia yao ya kumkirimu mgeni mke alale naye. Japokuwa ni kwa hiyari ya mke mwenyewe atayeambiwa na mumewe afanye hivyo, maana kwa kawaida wao huoa wake wengi.
Basi endapo kwa ule usiku mmoja yule mgeni aliyekaribishwa, mke akijaamiana naye na kumpa ujauzito, mtoto si wake bali wa yule mwenyeji aliyemkirimu mkewe alale naye.
Ni moja ya mastaajabu ya kijadi, lakini hizo ni baadhi ya mila za baadhi ya makabila ambazo nyingi zimeanza kutoweka kutokana na hali halisi ya sasa.
Lakini kama ilivyo kwa makabila mengi, mambo haya ambayo labda wanaharakati wa sasa wa haki za akina mama wanaweza kushangazwa nayo, kwa Wairaqw ni mambo ya kawaida yaliyozoeleka kwenye kabila lao tangu zamani.
Kwa hiyo, hata kama mwanamke anapata matatizo kwenye ndoa yake kama vile kupigwa, wao huchukulia kuwa mume anaonesha ukuu wake kwenye kaya.
Kama mume huyo ataadhibiwa basi zaidi atatozwa faini tu, ila mwanamke atakayepigwa akikimbilia kwa wazazi wake na kudai talaka atachekwa na familia yake.
Familia hiyo itamtaka arudi kwa mumewe, maana ni kawaida kwa mume kuonesha nguvu ya mamlaka yake kwenye familia. Lakini yule mume hata kama utaratibu unamruhusu kumuadhibu mkewe kwa kumpiga, anapaswa kuwa mwangalifu sana kwa kutompiga kichwani. Kama akimpiga mkwe kichwani na kumjeruhi kiasi cha kumtoa damu, basi atatozwa faini ya kulipa ng’ombe wengi.
Ndugu zetu hawa wana mfumo wao wa uongozi kwa ngazi mbalimbali, kuanzia kifamilia, kiukoo na jamii nzima ya kabila lao.
Kiongozi mkuu wa jamii ni ‘Kahamusmo’ ambaye husaidiwa na ‘Yaabusmo’ hayo ni majina ya hadhi za vyeo vyao.
Mfumo wao huwezesha kila kiongozi kutimiza wajibu wake ipasavyo kwa ngazi yake, bila maingiliano yoyote yanayoweza kukwaza mfumo wenye ushirikiano unaoeleweka.
Ukiondoa hao viongozi, watu wengine muhimu ni waganga wa jadi ambao wana hadhi inayokubalika kwenye kabila hilo.
Nadhani bado unakumbuka uwezo wao wa uganga, kama tulivyosimulia kiongozi wao Haymu Now Hatype alivyohamisha ziwa Manyara ambalo wenyewe huliita ‘Tlawta Mooya’ ili kupata nchi ya kuishi na kulima.
Wairaqw huwafunza watoto wao maadili mema ya kijamii tangu wakiwa wadogo, ambapo binti hufunzwa na mama yake hadi pale anapokaribia kuishi na mume.
Mafunzo hayo ni jinsi pia atakavyoitunza familia yake, kama ambavyo kijana wa kiume pia hufundishwa na baba yake hadi anapoanzisha familia yake mwenyewe kwa kuoa.
Katika mafunzo hayo kuna mambo ambayo ni lazima kwa jinsia husika ya mtoto kuyafahamu, mathalan mtoto wa kiume lazima ajue kuchunga.
Ndugu zetu hawa wenye mfumo wao wa kuamua kesi kwa makosa yaliyotendeka, ambapo wazee ndiyo wanahusika na jukumu hilo.
Lakini katika kusikiliza matatizo hayo huzingatia jinsia, kama mkosaji ni mwanamke, basi shauri lake lilisikilizwa kwanza na wazee wa kike. Kisha baada ya kupata mustakabali wa uamuzi wao, hukaa pamoja na wazee wa kiume kwa uamuzi wa mwisho.
Lakini si lazima mtuhumiwa akikutwa na hatia shauri linaposikilizwa na baraza la wazee wa jinsia yake uamuzi ukabaki hivyo linapokaa baraza zima la jinsia mbili.
Japokuwa mara nyingi huwa hivyo lakini maana ya kuanza kupeleka shauri kwa wazee wa jinsia husika ya mtuhumiwa, ni kutokana na ule mfumo wa wajibu wa malezi ya mtoto kijinsia.
Kwa hiyo, haya mambo ya mahakama na rufani yapo tangu zama hizo za kijadi, ni mifumo iliyokopwa na kuwekwa kisasa kwenye maisha yetu ya siku hizi.
Kama mtuhumiwa wa hizo kesi zao za kijadi za Kiiraqw akikutwa na makosa ya kutozwa faini, hulipishwa faini hiyo ambayo huitwa ‘dohho’ kwa lugha yao.
Lakini kama ikitokea mtuhumiwa akakutwa na hatia lakini bado hakubali kukiri makosa yake, basi adhabu yake ni kutengwa kabisa na jamii yote.
Kwa kesi ambazo ushahidi wake hauko wazi sana, wahusika wote yaani mlalamikaji na mlalamikiwa huapishwa kuwa watakayoyasema ni ukweli.
Kama ni ya uongo, basi atakayedanganya atapata laana kutokana na kiapo alichokula.
Mambo unayoyashuhudia sasa ya kuapishana mahakamani yasikushangaze, hayakuanza jana wala leo bali yalikuwapo tangu zamani.
Tena kwa wakati huo ukidanganya unaweza kusalimika kwenye maamuzi ya shauri husika, lakini ile laana hakika itakushukia!
Basi kama unavyoona werevu wa ndugu zetu hawa kwenye mambo yao mengi, basi hata kwa tiba za kijadi ni mahodari sana. Hutumia dawa za mitishamba za mizizi ambayo husagwa au kuchemshwa mizima kama ilivyo, kisha mgonjwa hupewa anywe ili kujitibia.
Haya, simulizi za ndugu zetu hawa zinanoga lakini pia nafasi yetu nayo imetuishia. Sina budi kukamilisha mambo ya Wairaqw licha ya kwamba kuna mengi yanayowahusu ambayo hatukuyagusia.
Tunalazimika kupeana fursa ya kuwafikia Wajadi wengine pia wanaosubiri kutimizwa maombi ya simulizi za makabila yao, ili nao wajitambue kijadi.
Tuweke miadi ya kukutana tena kesho ili kuwafikia Wajadi wengine.


Makala haya yamehaririwa na yalichapishwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Tanzania Daima Aprili 18, 2009.

Comments