Featured Post

LILIAN INTERNET: SIKUTAKA MPAKA NIPIGIWE KELELE NA MASHABIKI “TOKA STEJINI!”

Lilian Joseph Tungaraza almaarufu Lilian Internet enzi zake wakati akishambulia jukwaa.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
USIKU wa Jumamosi, Agosti 27, 2016 ndio ulikuwa wa mwisho kwa Lilian Joseph Tungaraza, maarufu kama Lilian Internet, kufanya kazi ya unenguaji katika bendi wakati alipostaafu rasmi kuitumikia bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’.
Ni siku ambayo bendi hiyo kongwe nchini ilifanya onyesho maalum la kumuaga mnenguaji wake huyo aliyeitumikia bendi hiyo kwa takriban miaka 14 tangu alipojiunga nayo mwaka 2001 akitokea Diamond Sound ‘Wana Dar es Salaam Ikibinda Nkoi’ ambayo ilikuwa imesambaratika, bendi aliyoanzia maisha ya muziki tangu mwaka 1996 pale New Silent Club, Mwenge.
Onyesho hilo la kumuaga, ambalo lilifanyika katika ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni (ambao sasa umebomolewa), ambalo aliliandaa mwenyewe na kuomba bendi yake imsindikize lilifana na lilidhihirisha jinsi mwanadada huyo alivyo mahiri katika uchezaji, lakini pia alivyo mbunifu.
Ni mbunifu kwa kuwa Lilian alifanya kitu ambacho hakijawahi kufanywa na mnenguaji yeyote hapo kabla – kufanya onyesho la kuagana rasmi na unenguaji ilikuwa ni zaidi ya akili ya kawaida.
Hapa Lilian (kulia) enzi zake akiwa na mcheza shoo mwenzake enzi hizo, Aisha Mohamed Mbegu maarufu Aisha Mdinda (sasa marehemu) wakilishambulia jukwaa la Twanga Pepeta. 
Katika mahojiano na MaendeleoVijijini Blogyaliyofanyika shambani kwake Bunju, jijini Dar es Salaam, Lilian alisema kwamba aliamua kuachana na unenguaji kwa sababu hakutaka kusubiri mpaka apigiwe kelele na mashabiki atoke jukwaani.
“Sikutaka mpaka mashabiki wapige kelele za “Tokaa! Tokaa!” kwa sababu ya kushindwa kumudu jukwaa kutokana na umri… kwa kifupi, nilitaka mimi ndiye niuache muziki, siyo muziki uniache.
“Unajua unaweza kufika wakati umri ukawa kikwazo, akili inaweza kuwa tayari kufanya jambo fulani jukwaani, lakini mwili ukagoma, sasa usingoje mpaka ufikie hatua hiyo, maana hapo ndipo mashabiki watakapokupigia kelele utoke jukwaani,” anasema.

Aliuacha muziki?
Lilian (37) ambaye ni mama wa watoto wawili – Amrock (7) na Bilgis (4) – anasema hakuacha kabisa muziki, aliamua kuachana na unenguaji na kugeukia uimbaji kama mwanamuziki binafsi huku akijikita kwenye Bongo Fleva.
Katika kipindi cha mwaka mmoja, tayari amekwishatoa nyimbo nne ambazo ni Wangu Moyo aliomshirikisha Barnaba, na nyimbo nyingine tatu – Nishawazima, Navimba na Together – amekamua peke yake na kuonyesha kipaji cha hali ya juu katika uimbaji kiasi cha kutishia baadhi ya waimbaji wa kike ambao wamekuwepo kwenye game kwa muda mrefu.
Nyimbo zote hizo zimerekodiwa kupitia lebo yake mwenyewe na mumewe, Sheri Buhiregabo, ya LS Entertainment.
Waliodhani kwenye wimbo wa Wangu Moyo alibebwa tu na Barnaba walikosea, kwani ukisikiliza nyimbo kama Nishawazima na Navimba utaamini kwamba Lilian ni zaidi ya yule aliyekuwa akinengua stejini – kwa kifupi ni habari nyingine kabisa katika Bongo Fleva.
“Ni ukiritimba tu ndio unaofanya nyimbo zangu zisipigwe sana kwenye vituo vya redio na runinga, baadhi ya vituo vya redio watangazaji wao wamewahi kuniambia wazi kwamba hawawezi kupiga nyimbo zangu kwa sababu mimi ‘sina skendo’, yaani msanii akiwa na skendo kama kufumaniwa au kutembea uchi, au hata kuwa na uhusiano na msanii mwingine, ndiyo anapewa kipaumbele,” anasema kwa masikitiko.
Lakini anasema kwamba, yeye anajiheshimu na katu hawezi kufanya mambo ya kipuuzi kama hayo eti tu kwa sababu ya kutafuta umaarufu.
“Umaarufu nilikwishaupata miaka mingi, nafanya muziki kwa sababu uko kwenye damu, ni taaluma na inafaa kuheshimiwa, kwanza nikiingia kwenye makashfa kama hayo hata jamii itanishangaa na kunidharau – japo sikatai kwamba binadamu anakosea, lakini siwezi kuigiza kashfa,” anasema.
Aidha, anasema kwamba, katika studio moja aliwasikia watangazaji akisema kwamba, yeye ni mwimbaji mahiri, lakini kama watapiga nyimbo zake ‘atawaharibia wasanii wao’.
“Nilipeleka single yangu, lakini baadaye nikiwa naondoka nikawasikia wakisema wenyewe kwa wenyewe, kweli mimi najua kuimba, lakini kama watakimpa promo nitawazima, madai ambayo hayana msingi kwa sababu kila mmoja anaimba tofauti na ushindani unapokuwepo ndipo maendeleo yanakuwepo kwa kuongeza ubinifu.
“Sikujua kama kumbe kuna baadhi ya vituo vya redio na runinga vina ‘wasanii wao’,” anasema kwa kusikitika.

Hakati tamaa
Pamoja na changamoto hizo, Lilian anasema kwamba kamwe hawezi kukata tamaa, kwa kuwa ana malengo makubwa kwenye muziki, ikiwa ni pamoja na kuanzisha taasisi ya kuwasaidia wasanii wengine hapo baadaye.
“Nafikiria kuanzisha taasisi ya kuwasaidia wasanii, hasa chipukizi, hivyo siwezi kukatishwa tamaa na changamoto hizi ambazo kwa kweli zinarudisha nyuma maendeleo,” anasema.

Lilian akiwa kwenye banda lake la kuku shambani kwake Bunju.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656 331974.

Comments