Featured Post

LILIAN INTERNET: SASA NAFUGA SUNGURA NA KUKU, KARIBUNI MNIUNGE MKONO!


Lilian Joseph Tungaraza, maarufu Lilian Internet, akiwa  anamtazama mtoto wa sungura mwenye miezi miwili katika shamba lake lililoko Bunju jijini Dar es Salaam. PICHA ZOTE NA DANIEL MBEGA/MAENDELEOVIJIJINI BLOG.



Lilian akiwa amembeba jogoo wa jamii ya Kuchi ambao ni miongoni mwa kuku wa kkienyeji anaowafuga.





Lilian akiangalia kuku wake aina ya Saso ambao ni maalum kwa uzalishaji wa mayai ya utotoleshaji.
Hapa anaangalia mazao mbalimbali kwenye shamba lake.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
TAKRIBAN kilometa mbili kutoka kituo cha Mianzini, Bunju A kwenye barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo katika eneo la Mkanada utakutana na manzari ya pekee kutokana na miti ya matunda iliyostawi vyema.
MaendeleoVijijini ilishuhudia kwamba, mingi kati ya miti hiyo ni mipapai, ambayo licha ya ufupi wake, lakini tayari imeanza kuzaa katika upande mmoja wa eneo hili lenye ukubwa wa takriban ekari mbili.
Nyumba kubwa ambayo bado haijaezekwa itakulaki sawia huku pembeni kukiwa na nyumba nyingine chini ya miti yenye kivuli.
Hapa nakaribishwa na dada ambaye amevalia gauni la kumbwaya – wenyewe wanaita ‘Dela’ – la rangi ya manjano.
Tangu nimemfahamu dada huyu takriban miaka 20 iliyopita akiwa na bendi za Diamond Sound ‘Wana Dar es Salaam Ikibinda Nkoi’ na African Stars ‘Twanga Pepeta’, ndiyo kwanza namuona akiwa amevalia vazi la aina hii, na kwa hakika ndiyo mara ya kwanza kumkuta katika mazingira kama haya maana siku zote nimekuwa nikimuona jukwaani akinengua kwa ustadi wa juu kiasi cha kujipatia umaarufu mkubwa.
“Naitwa Lilian Joseph Tungara, mashabiki wangu wamezowea kuniita Lilian Internet,” ndivyo anavyojitambulisha kwangu huku akitabasamu.
Ingawa kuna kivuli, lakini ananikaribisha moja kwa moja nyuma ya nyumba ambako anasema alikuwa na shughuli za kufanya – na ndizo zilizonipeleka huko.
Ninalakiwa na kelele nyingi za kuku walio katika mabanda matatu tofauti, lakini kwanza ananipeleka kwa banda dogo la pembeni na kufungua mlango mmoja mdogo.
“Hili ni banda langu la sungura, nawapenda sana, na ninataka kufuga kibiashara zaidi,” anasema huku akimtoa sungura mmoja mdogo na kumshika kwa makini ili asimuumize.
“Muziki ni fani yangu, upo kwenye damu, ninaupenda na siwezi kuuacha kwa sababu ndio ulionifanya nijulikane, lakini hapa ndiyo maisha yangu – ujasiriamali. Nimeamua kujikita katika ujasiriamali, hasa katika sekta ya kilimo na mifugo, kwa sababu naamini ndiyo pekee inayoweza kunipa tija.
“Hapa nimepata uzoefu – japo naendelea kujifunza – na kwa kutumia shughuli hizi ninafanya biashara pia. Malengo yangu ni kuona kwamba hapa panakuwa shamba darasa  ili niweze kuwafundisha na wengine, ingawa mimi mwenyewe bado naendelea kujifunza,” anasema kwa furaha.

Kwanini sungura?
Anasema kwamba ameamua kufuga sungura kwa sababu anaamini ni biashara ambayo inaweza kuwa na tija siku za usoni.
“Ujue sungura ni mnyama rahisi wa kufuga kwani hana gharama kubwa sana, huhitaji kuwa na mamilioni ndipo uanzishe mradi kama huu, tena sungura akitunzwa vyema inavyostahili haugui kwa urahisi na pia lishe yake ni rahisi kupatikana.
“Kama unavyoona hapa, nawalisha nyasi, mboga kama vile sukuma wiki, spinachi, kabichi, karoti, mchunga, bado sijaanza kuwanunulia pellets na wanaendelea vizuri kabisa,” anafafanua.
Anasema kwamba, kwa kuwalisha vyakula hivyo vibichi sungura wanakojoa mara kwa mara, na mkojo wake ni mali unaweza kumpatia kipato kikubwa hapo baadaye kwa sababu unatumika katika maabara na viwandani kwa utengenezaji wa mbolea (follier fertilizer) na dawa za kuulia wadudu kwenye mazao.
Anaongeza kwamba, sungura hapati magonjwa ya mara kwa mara tofauti na wanyama wengine, lakini ikiwa tu utadumisha usafi na kuwapatia lishe bora.
“Nyama ya sungura ni tamu na inalingana na nyama ya kuku. Hii ni nyama nyeupe ambayo haina lehemu (cholesterol) na hiyvo wataalam wa lishe bora huhimiza matumizi ya nyama ya sungura kwani ni bora kwa afya,” anasema.
Hata hivyo, anasema anahitaji kuongeza idadi ya sungura na kupanua mradi wake kabla hajaanza kufikiria kuhusu faida zaidi.
“Kwa sasa ninao sungura 20, wangekuwa wengi, lakini wengine walikufa wangali watoto kutokana na changamoto ambazo nilikuwa sijajua namna ya kukabiliana nazo,” anasema.

… Ni sungura tu au?
Anasema hafugi sungura peke yake, bali anafuga kuku aina ya Saso ambao ni maalum kwa kutaga mayai ya kutotolesha, kuku wa kienyeji pamoja na njiwa.
“Ninao kuku karibu 500 wa aina ya Saso ambao wamefikisha miezi minne sasa, bado mwezi mmoja tu waanze kutaga. Nataka kuweka mashine ya kutotolesha mayai ili niwe ninauza vifaranga,” anasema.
Lilian, ambaye licha ya kustaafu kucheza shoo mwaka 2016 bado anaendelea na muziki akiwa amegeukia Bongo Fleva, anasema anao kuku wa kienyeji wapatao 80 sasa wa aina mbalimbali, wakiwemo Kuchi.
Aidha, anasema kwamba, anakusudia kuongeza zaidi kuku wa kienyeji na kuwazalisha hadi walau wafikie 5,000 ndipo aanze kuwauza.
“Nataka wafanyabiashara wa kuku wawe wanakuja hapa kununua badala ya kwenda mikoani, naamini hata ndani ya Jiji kama hili tunaweza kuzalisha wanyama kwa biashara kwa maeneo tuliyonayo,” anasema.
Ukiacha mifugo hiyo, Lilian ambaye ni mama wa watoto wawili – Amrock mwenye miaka saba na Bilgis mwenye miaka minne – anasema ndani ya eneo lake hilo lenye ukubwa wa takriban ekari mbili, anaendesha kilimo cha bustani pamoja na miti ya matunda.
“Nalima kabichi, spinachi, Chinese, pilipili hoho, bilinganya, nyanya chungu, mahindi pamoja na mananasi, migomba, mipera, michungwa na nimepanda mipapai 200 ya kisasa ambayo imeanza kuzaa ikiwa na miezi mitatu tu,” anasema.

Muumini wa kilimo hai…
Anabainisha kwamba, mazao yote ya shambani hatumii mbolea za kemikali, bali kinyesi cha mifugo yake pekee, kwani yeye ni muumini wa bidhaa za kilimo hai.
“Nikitoa kinyesi cha kuku na sungura napeleka kwenye mazao yangu ya bustani, lakini bado mazao hayo ya shamba pia yanawafaa wanyama wangu kama sungura na kuku wa kienyeji,” anasema.
Anaongeza kwamba, hakuna kinachotupwa kati ya mazao ya shamba na mifugo. “Taka za mifugo ni mbolea, mabaki ya mazao ni chakula cha wanyama!”

Kwanini ujasiriamali?
Lilian anasema kwamba, kwa maisha ya sasa ni lazima kuwa na mipango mbalimbali ya maendeleo badala ya kutegemea kazi moja.
Anasema, japokuwa anaendelea na muziki akipiga Bongo Fleva, lakini ujasiriamali ni ndoto yake ya muda mrefu na kwamba alishindwa kuifanya kwa kuwa muda mwingi aliutumia jukwaani, tofauti na sasa ambapo amekuwa na muda wa kutosha unaomruhusu kufanya shughuli nyingine.
“Muda mwingi nilikuwa stejini na bendi, wakati mwingine nilitakiwa kusafiri nje ya nchi, sikupata nafasi kama niliyonayo sasa… ukitaka kufanikiwa kwenye ujasiriamali ni lazima mwenyewe uwepo hata kama unao wasaidizi, na kadiri unavyokuwepo nawe unajifunza na kujua changamoto zilizopo na namna ya kukabiliana nazo,” anasema.
Anawashauri wanamuziki wenzake, hususan akinadada, kuwa na mipango mbadala ya maendeleo kwa kuwa hata shughuli hizo za muziki zina ukomo wake.
“Niko tayari kuwasaidia mawazo vijana na wasichana wanaotaka kujifunza ujasiriamali, nataka kuwajenga kifikra, kila mmoja anaweza na tunaweza kubadili uchumi wetu binafsi na taifa kwa ujumla,” anasisitiza.

Lakini mbali na hilo, malengo yake ni kuchakata bidhaa zinazotokana na mazao ya mifugo na kilimo ili kuongeza mnyororo wa thamani.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656 331974.

Comments