Featured Post

NYAYO ZA CHIFU MKWAWA: KUTOKA MWINDAJI WA ETHIOPIA HADI CHIFU MKUU WA WAHEHE - 2

Malugala Mwamuyinga (kulia) akimsimulia mmiliki wa blogu hii, Bw. Daniel Mbega, historia ya ukoo wa Chifu Mkwawa.

Na Daniel Mbega, Iringa
MAANDIKO kadhaa yamekuwepo kuhusiana na historia ya Wahehe na hasa ukoo wa Mtwa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa, lakini yote hayo hayakunizuia kuisaka historia hiyo.

‘Jicho halishibi kuona na Sikio halikinai kusikia!’ hivyo nikaamua kufunga safari hadi Lungemba, yaliko makaburi ya Mtwa Munyigumba na ndugu wengine wa ukoo huo, yapata kilometa 62 kutoka Iringa Mjini.
Wapo walioandika kwamba chimbuko la Mtwa Mkwawa ni Ungazija, lakini simulizi ninazokutana nazo hapa ni tofauti, maana zinatoka katika vinywa vya wanaukoo wa Muyinga, ambao nao wameipata ama kurithishwa kutoka kizazi na kizazi kutokana na simulizi za mababu zao.
Wale waliopata kuandika kwamba asili ya akina Mkwawa ni Ungazija wanaeleza kuwa mtawala wa Ngazija aliyeitwa Yusuf Hassan ambaye alikuwa Mwarabu, alizaa watoto wawili wa kiume, Hassan ‘Mbunsungulu’ na Ahmad.
Wanasema kwamba Mufwimi alikuwa mmoja wa watoto watatu wa Mbunsungulu aliozaa na mwanamke wa Kikaguru.
Ndugu zake wengine walikuwa Ngulusavangi na Ngwila, kwa maelezo yaliyo kwenye baadhi ya maandishi ambayo yanatoweka kutokana na Watanzania kukosa utamaduni wa kutembea, kujifunza na kudadisi.
Rungemba ni kijiji ambacho hakijasikika sana katika historia kama lilivyo jina la Mkwawa, lakini hapa ndipo kwa kiasi kikubwa lilipo chimbuko la Chifu huyo wa kabila la Wahehe na ndipo lilipo kaburi la Mtwa Munyigumba.
Ignas Pangiligosi Muyinga, maarufu kama Malugila Mwamuyinga (67), ambaye ni kitukuu wa Msengele Kilekamagana, mdogo wake Mkwawa, anaona fahari kuisimulia historia ya ukoo huo maarufu.
“Shina la ukoo wetu linaanzia kwa mtu aliyeitwa Mufwimi (yaani Mwindaji), ambaye mababu zetu walitusimulia kwamba alitokea Ethiopia,” Malugala anaanza kueleza. “Mufwimi alipita akiwinda kutoka Ethiopia, Kenya kabla ya kuingia Tanganyika na kujikuta yupo Usagara na hatimaye eneo la Nguluhe-Dabaga akipitia Ikombagulu, himaya ya Chifu Mwamduda. Wengi walimfananisha na mtu wa kabila la Wakamba kutoka Kenya kutokana na umbile lake kubwa.”
Wakati huo eneo ambalo sasa linaitwa Iringa lilikuwa na makabila mbalimbali. Walikuwepo ‘Wahafiwa’ katika Bonde la Milima Welu, Luvango, Wutinde, Lugulu, Makongati, Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalang’ombe, Ibanagosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe na Isanzala.
‘Vanyategeta’ wao waliishi Udzungwa, Kitelewasi na Lundamatwe ya sasa, ambao walikuwa wahunzi hodari.
‘Vanyakilwa’ walilowea Mufindi wakitokea Kilwa; ‘Vasavila’ waliishi milima ya Welu huko Makungu (Kihanga ya sasa), Magubike na Malangali; na ‘Vadongwe’ waliishi kando ya milima ya Uhambingeto, Ipogolo, Nyabula na Luhota.
Mufwimi alikuwa mwindaji mkubwa wa nyati ambapo aliichoma nyama yake kwa kuipaka chumvi ambayo ilikuwa haifahamiki kwa wakazi wa himaya hiyo, alimpelekea zawadi ya nyama-choma Chifu Mwamduda aliyeipenda mno kwa ladha yake.
Alipendwa na kukaribishwa na Mwamduda kuishi kwake, lakini akaanzisha mapenzi ya siri na Semduda, binti wa Chifu huyo, ambaye alikuwa amewakataa wachumba wengi. Binti huyo akapata ujauzito. Mufwimi akaogopa kwa kuona amefanya kosa kubwa ambalo pengine adhabu yake ingekuwa ni kifo chake.
Jioni moja akamwita Semduda na kumweleza kwamba yeye anaondoka, lakini akampa maagizo, ikiwa atajifungua mtoto wa kike amwite Mng’anzagala na akiwa wa kiume amwite Muyinga Mufwimi (maana yake ni Mhangaikaji Mwindaji).
Mufwimi alitoroka kwa hofu ya kuuawa na Mwamududa. Akaendelea kuwinda huko na huko hadi Itamba alikouawa na nyati. Hakuna ajuaye lilipo kaburi lake.
Lakini kumbe mtawala huyo alifurahi kusikia bintiye ana mimba ya Mufwimi, maana alijua sasa angekubali kuolewa.
Hata hivyo, wapi angempata Mufwimi ambaye tayari alikwishatoweka? Hili lilimhuzunisha Chifu Mwamduda.
JUMAPILI IJAYO: Uchifu waingia rasmi.


Imetayarishwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656 331974.

Comments