Featured Post

VYANZO VINGI LAKINI NJOMBE NA IRINGA MAJI TABU

Mto Ruaha Mkuu ambao ni mto wa pili kwa urefu nchini Tanzania ukiwa na urefu wa kilometa 475.


Na Lilian Mkusa, Iringa
LICHA ya kuwa na vyanzo vingi vya maji katika Mikoa ya Iringa na Njombe bado maji ni tatizo katika maeneo mengi.

Katika vituo vingi vya afya na zahanati kumekuwa na changamoto za kukosekana kwa huduma muhimu ili kuhakikisha utoaji wa huduma za afya na matibabu unaendana na mazingira safi yatakayo hakikisha kuwa mgonjwa haondoki akiwa na maradhi mengine.
Huduma za msingi kama vile maji huhakikisha kwamba pamoja na kuwa mgonjwa amekwenda kutibiwa aina fulani ya maradhi, anahitaji huduma nyingine kama binadamu wa kawaida na pia ni vitu vya muhimu kuambatana na huduma bora ya afya.
Kutokuwepo kwa rasilimali hii muhimu katika zahanati kumekwamisha utolewaji wa huduma kwa wajawazito, mfano hutakiwa kubeba maji lita tano kwa ajili ya kuwasaidia wakati wa kujifungua, hali ambayo ni hatari kwa sababu maji hayo kwanza hayatoshi lakini pia si salama maana haijulikani wapi yamechotwa.
Vijijini kuna uhaba mkubwa wa miundombinu ya kutosha ya maji.
Upatikanaji wa maji siyo wa uhakika na wananchi wengi hutegemea maji ya visima na hata madimbwi au vijito na chemchemi ambazo nyingi huwa si salama kwa matumizi ya binadamu.
Kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu ya kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa maji safi, wananchi wa maeneo ya vijijini hulazimika kutumia vyanzo vya maji vinavyowazunguka bila kujali usalama wa maji hayo na hivyo kuweka afya zao katika hatari.
“Tunalazimika kubeba mashuka na kwenda kuyafulia nyumbani, tena tunayafua mtoni ambako tunatembea hadi kilometa 9, kwa hali anayokuwa nayo mjamzito akitoka kujifungua ni hatari kutembea umbali huo,” anasema Selina Mwemile, mkazi wa Kijiji cha Lundamatwe wilaya ya Kilolo.
Zahanati hazina mabafu hali ambayo huwalazimu wajawazito na wagonjwa wengine kuoga chooni ambako hali ya usafi si nzuri. Kutokana na hali hiyo wengi huoga vichakani mahali ambapo si salama hasa kwa hali wanazokuwa nazo.
 “Wakati mwingine mtu anaona ajisaidie kichakani na sio katika vyoo vya zahanati maana hali ni mbaya sababu tunakutana watu wa tabia tofauti, sasa kama wote tukijisaidia vichakani hali itakuwaje?” anasema Maria Nyenza mkazi wa Kijiji cha Idegenda.
Pamoja na hayo, bado hakuna utaratibu wa kuwepo kwa maji safi na salama ya kunywa katika zahanati, wakati mwingine mgonjwa hutakiwa kumeza dawa papo hapo lakini badala yake huambiwa akameze nyumbani au akatafute maji popote ambapo hujikuta akinywa maji yasiyo safi na salama.
Kitapu kipo lakini maji hayatoki.
Bado hakuna mfumo bora wa kuvuna maji katika sehemu hizi za kutoa huduma ilhali kulikuwa na umuhimu wa kutoa elimu juu ya suala hilo pamoja na vifaa maalumu vya kuhifadhi maji hayo ya mvua. Bomba zilizoharibika hazifanyiwi matengenezo na badala yake zimekuwa mapambo wakati zingeweza kutengenezwa na maji yakapatikana. Kwa ujumla hakuna ufuatiliaji yakinifu wa masuala ya maji.
“Yalishaletwa hadi mabomba hapa na yakaunganishwa kabisa lakini ghafla tu tukaona yanatolewa sasa sijui tatizo lilikuwa nini na mpaka leo kimya tumeshafuatilia tumechoka,” anasema Rashid Kihombo mkazi wa kijiji cha Lihagule wilaya ya Ludewa.
Kuna umuhimu mkubwa wa kuwekwa miundombinu ya uhakika ya upatikanaji wa maji hasa katika maeneo ya vijijini kwenye vituo vya utoaji wa huduma za afya ili kuwahakikishia wakazi wa maeneo ya vijijini uhakika na ustawi wa afya zao kupitia huduma ya uhakika ya maji safi na salama.


Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. +255 656 331974.

Comments