Featured Post

KILOLO ‘WALIA’ KWA KUGAWA ARDHI BURE

Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto, akiwa katika Kijiji cha Mhanga, Kata ya Kimala, akionyesha Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro inayopakana na Wilaya Kilolo.


Na Daniel Mbega, Kilolo
WANANCHI wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wanalia hawana ardhi. Na wataikosa kwa miaka 100 ijayo, au pengine milele, kwani hata vizazi vyao havitakuwa na kumbukumbu kama wazazi wao waliwahi kumiliki ardhi.

Kwa sasa hawana hata ardhi ya akiba, inapotokea kuna mradi wa jamii, hata wa kujenga zahanati, lazima serikali za vijiji zinunue eneo kwa wananchi wengine wenye ziada.
Si kwamba hawakuwa na ardhi, walikuwa nayo. Lakini ile ardhi ambayo mababu zao, akiwemo Chifu Mkwavinyika Munyigumba, waliipigania isitwaliwe na wakeng’e (Wazungu), sasa wameiuza kwa wawekezaji wa Kampuni ya New Forests kutoka Uingereza, kwa bei ya karibu na bure.
Kilio chao hakiwezi kusikika, kwani waligawa ardhi hiyo kwa hiari wala hawakushikiwa bakora. Ufukara na ujinga wa kutojua thamani ya ardhi ndivyo vilivyowaponza, jambo ambalo hata viongozi wao wanakiri.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, zaidi ya hekta 8,000 (takriban ekari 20,000) zimetwaliwa na New Forests Company (NFC) kwa ajili ya kupanda miti aina ya Misindano na Mikaratusi.
Ilikuwa hivi: Kampuni ya New Forests ilikuwa na fedha za kuwekeza … wananchi walikuwa na ardhi. Wawili hao wakaingia ‘mkataba’ lakini wananchi wamepoteza – wamemeza chambo, ndoano imewakaba.
Vijiji vingi katika Kata za Idete, Ukwega na Dabaga ambako kampuni hiyo imewekeza havina tena ardhi ya ziada kwa kizazi cha sasa na hata kijacho. Wawekezaji hao wamepata hatimiliki kwa karne nzima, miaka 99. Kizazi cha sasa hakitakuwepo na kijacho hakitajua pa kuanzia.
“Ujinga na umaskini ndio umewafanya wananchi wauze ardhi, hawakupewa elimu kuhusu thamani ya ardhi, walipoona fedha, na baada ya kushawishiwa na viongozi wa serikali za vijiji, wakaamua kuuza kwa bei ya kutupa. Hekta moja waliuza kwa kati ya Shs. 50,000 na 100,000 tu,” alisema Mejusi Mgeveke, Diwani wa zamani wa Kata ya Kimala wakati alipoongea na mtandao wa MaendeleoVijijini.
NFC iliomba kibali cha uwekezaji Tanzania kupanda hekta 20,000 za miti. Mpaka sasa imepata jumla ya hekta 8,000 tu wilayani Kilolo, bado inaendelea kutafuta ardhi katika maeneo hayo ya Nyanda za Juu Kusini na safari hii wanaelekea Wilaya ya Mufindi na mkoani Njombe.
Maeneo ambako NFC imepata ardhi ni katika vijiji vya Lukosi ambako kuna hekta 2,270.4 (Shamba Namba 972), Kising’a hekta 3,851.53 (Shamba Namba 973), Ipalamwa hekta 62.4 (Shamba Namba 974), Ndengisivili hekta 121.5 (Shamba Namba 975), Ukwega hekta 94.6 (Shamba Namba 976), Isele hekta 1,215 (mpango wa mwaka 2013), Idete hekta 50 na eneo jingine bado ‘wanalifukuzia’ katika Kijiji cha Makungu kwenye Kata ya Ukwega.
Tangu imeanza uwekezaji wa kilimo hicho cha miti kwa ajili ya matumizi ya viwandani mwaka 2010, kampuni hiyo kutoka Uingereza imetumia kiasi cha Dola 110 milioni (takriban Shs. 176 milioni).
Kampuni imekwishapatiwa hatimiliki kwa mashamba ya Lukosi na Ukwega kwa muda wa miaka 99. Bado inasubiri hatimiliki kwa mashamba yaliyobaki.
Lengo lake jingine ni kuvuna hewa ya ukaa (Carbon Dioxide), ambayo kwa muda sasa imekuwa ikihitajika katika nchi nyingi za Ulaya Magharibi katika harakati za Umoja wa Mataifa kupunguza joto kutokana na ufyekaji wa misitu pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
Lakini wakati taarifa za NFC zinasema kwamba mpaka sasa wamepata takriban hekta 8,000, Diwani wa Kata ya Kimala, Mejusi Mgeveke, anasema eneo lililochukuliwa na wawekezaji hao ni hekta 13,000 (ekari 33,500) likihusisha vijiji vyote vilivyotajwa.

Taratibu zilizotumika
Uchunguzi uliofanywa na MaendeleoVijijini umebaini kwamba, utaratibu uliotumika kupata ardhi hiyo haukuwa wazi katika maeneo mengi.
“Walipokuja wawekezaji kuomba ardhi miaka mitano iliyopita wananchi walielezwa kwenye mikutano ya hadhara, wakaridhia, wataalamu wakaja kupima na kuthaminiwa. Wananchi wakalipwa fidia,” alisema Aridi Sanga, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Magome katika Kata ya Dabaga.
Maelezo yake yaliungwa mkono na Diwani wa zamani wa Kata hiyo, Amin Tengelakwi, ambaye anasema wakati walipokuja NFC katika maeneo hayo wananchi walishirikishwa na wakaridhia wenyewe kutoa maeneo hayo.
“Ardhi iliyotolewa ipo eneo la Wotamasiwa, ambalo ni la kijiji na la watu binafsi, lakini kwa miaka mingi lilikuwa halitumiwi.
“Waliokuwa wakipanda miti kwenye maeneo hayo ilikuwa ikiungua tu kwa vile wanajijiji wa Kiwalamo walikuwa wakianzisha moto wakati wa kuandaa mashamba, hivyo serikali ikaona ni vyema wakampatia mwekezaji,” alisema Tengelakwi na kuongeza kwamba fidia iliyotolewa na mwekezaji ilikuwa Shs. 100,000 kwa hekta.
Tengelakwi alisema, uhusiano baina ya wananchi na mwekezaji ni mzuri. “… amesaidia kujenga nyumba ya mganga katika zahanati ya Magome na ameahidi kujenga vyumba viwili vya madarasa na matundu manne ya vyoo kwenye Shule ya Msingi Kidabaga.”
Lakini si diwani huyo wala mtendaji anayejua wapi mihutasari ya mikutano hiyo ya wananchi ilipo hasa baada ya uongozi wa zamani wa Kata na Kijiji cha Kidabaga kutimuliwa mwaka 2012 kutokana na kutumia mabavu kuwachapa viboko wananchi.
Katika vijiji vya Kimala, Idete, Magome, Kising’a, Makungu na Ipalamwa, hakuna kumbukumbu zozote za kuonyesha mihutasari ya vikao hivyo wala makubaliano baina ya vijiji na wawekezaji zaidi ya makubaliano ya mdomo kwamba wawekezaji wangetoa misaada kwa huduma za jamii.
Tofauti na wawekezaji wengine wa kilimo cha miti ambao wameandikishana na wanavijiji kwamba watatoa asilimia 10 ya mapato yao kusaidia shughuli za maendeleo, NFC yenyewe haikufanya hivyo.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Idete, Anderson Kitule, alisema hakuna mikataba yoyote ya maandishi baina ya wananchi na mwekezaji, hivyo hawajui hata nini ambacho wanajamii wanaouzunguka mradi watanufaika na uwekezaji huo.
“Tumejengewa tu bweni la wasichana katika shule ya sekondari ya Madege na wawekezaji hawa ambao pia wamejenga matundu ya vyoo na kutoa vitanda, magodoro, mablanketi kwa ajili ya bweni hilo,” alisema.
Bruno Hakimu Kauku, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Idete, ambayo vijiji vyake vya Kiwalamo na Idete vimetoa ardhi kwa mwekezaji, anasema hakuna nyaraka zozote kuonyesha mchakato mzima wa utoaji ardhi katika kata hiyo.

Malipo ya fidia
Utaratibu wa malipo ya fidia kwa wananchi nao haukuwiana na thamani halisi ya ardhi na wala haukuwiana kutoka eneo moja na lingine. Mahali pengine fidia ilikuwa Shs. 100,000, lakini kwingine wakalipwa 25,000 kwa hekta.
“Wawekezaji walipokuja walichukua ardhi kubwa, fidia ilikuwa ndogo, lakini kutokana na uelewa mdogo tulikwenda hivyo hivyo,” alisema Mgeveke, Diwani wa Kata ya Kimala.
Kwa sasa, anasema, wananchi wameshtuka, wametambua thamani ya ardhi, lakini hawana ardhi ya ziada.
Atilio Msigala, Mwenyekiti wa aliyepita wa Kijiji cha Kising’a katika Kata ya Ukwega, anasema malipo ya fidia kwa wananchi waliotoa ardhi yalikuwa madogo na yalichelewa tangu ardhi yao ilipofanyiwa tathmini mwaka 2005.
“Kijiji hakina eneo, wananchi ndio waliowapa ardhi NFC, lakini fidia ilikuwa ndogo, ardhi ilithaminishwa mwaka 2005 kwa kiasi cha Shs. 25,000 kwa hekta, malipo ya kwanza yalitolewa mwaka 2010, na yale ya mwisho yalitolewa mwaka 2011 ambapo hekta moja ililipwa kwa Shs. 40,000,” alisema Msigala.
Kijiji cha Kising’a kina eneo la hekta za mraba 8,884.58 na zilizotolewa kwa mwekezaji ni hekta 3,851.53, ingawa mwenyekiti huyo anasema eneo lililotolewa ni hekta 4,500 ikiwa ni zaidi ya nusu ya eneo la kijiji.
Diwani wa Kata ya Ukwega, Israel Mwilafi, ambaye ukoo wake walitoa hekta 400 (sawa na ekari 1,000), alisema walau wao ‘walilipwa vizuri’ mwaka 2011 kwa Shs. 40,000 kwa ekari moja.
“Sisi tulilipwa vizuri, ilikuwa Shs. 40,000 katika awamu ya pili tofauti na wale wa kwanza ambao walilipwa Shs. 25,000,” alisema.

NFC wanasemaje?
Uongozi wa NFC tawi la Tanzania, ulisema kwamba wao walifuata taratibu zote zinazotakiwa kupata ardhi ambapo walifika kwenye serikali za vijiji na kupeleka maombi yao, mikutano ikafanyika na mihutasari ikawasilishwa kwenye Kata, Halmashauri ya Wilaya na baadaye Wizara ya Ardhi ambako wamepata hatimiliki na bado wanasubiri nyingine.
“Hatujapora ardhi, taratibu zote zilifuatwa baada ya kupewa kibali cha uwekezaji. Bila taratibu hizi katu serikali haiwezi kutoa hatimiliki. Sisi hapa tunayo mihutasari yote, kama vijiji havina basi ni juu yao wenyewe,” alifafanua mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo.
Hata hivyo, alikiri kwamba hakuna makubaliano ya kimaandishi kuhusiana na kile ambacho wananchi wanastahili kukipata kama gawiwo kutokana na faida watakayoingiza hapo baadaye.
Na katika kuendelea kuwa karibu na wananchi, kampuni hiyo inachangia huduma za jamii kama kujenga zahanati katika vijijini mbalimbali, ikiwemo Kiwalamo ambako wamekamilisha ujenzi wa zahanati iliyogharibu Shs. 44.7 milioni.
Jengo mojawapo la zahanati katika Kijiji cha Kiwalamo, Kata ya Idete wilayani Kilolo lililojengwa na kampuni ya New Forests.

Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Abraham Nyantori, anasema kimsingi wawekezaji wanatakiwa kupitia kwenye serikali za vijiji katika uombaji wa ardhi na wananchi washirikishwe kikamilifu ili kuridhia.
“Kwa kuwashirikisha wananchi maana yake tutakuwa tumeondoa migogoro ya ardhi,” anafafanua na kuongeza kwamba ni vyema fidia nayo walau ikalingana na thamani ya ardhi.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. +255 656 331974.



Comments