Featured Post

JACKSON ISSA NUNDU: MKALI WA SAUTI ALIYETAMBA BAVY NATIONAL HADI MARQUIS DU ZAIRE

Jacques Issa Nundu (kulia) akiwa na Abubakar Kassongo Mpinda enzi ya uhai wao.


Jacques Issa Nundu (alizaliwa Julai 23, 1954 Uvira, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) alikuwa mwanamuziki raia wa Congo aliyejizolea umaarufu mkubwa akiwa nchini Tanzania ambako aliishi hadi mauti yalipomfika Jumamosi Oktoba 25, 2014 na kuzikwa mjini Moshi, Kilimanjaro.
 
Maisha yake ya awali
Jacques (Jackson) Issa Nundu alizaliwa katika Kijiji cha Nundu huko Uvira katika Jimbo la Kivu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo akiwa mtoto wa Chifu Sadi Issa Nundu. 
Ndiyo maana hata wakati akiwa nchini Tanzania alikuwa akiitwa Prince Jacques Issa Nundu.
Issa Nundu alijaaliwa sauti nzuri na alikuwa mtunzi na mwimbaji mahiri ingawa taaluma aliyoisomea ilikuwa ni ufamasia ambapo alipata kufanya kazi katika Hospitali ya Uvira kama Mfamasia. 
Akiwa katika hospitali hiyo alikuwa akifanya kazi asubuhi hadi mchana, ambapo usiku alikuwa akienda kupiga muziki katika bendi ya Bavy National akiwa na mpiga solo Dekula Kahanga Vumbi ambako alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na sauti yake murua.
Wakati huo alikuwa na uwezo wa kukariri kisha kuimba nyimbo za wanamuziki wakongwe mbalimbali zikiwemo za akina Dk. Nico Kasanda wa African Jazz.
Issa Nundu aliitumikia bendi ya Bavy National kati yam waka 1981 hadi 1983 ambapo aliondoka Uvira na kwenda Tanzania akiongozana na mtunzi na mwimbaji Kyanga Songa ambaye pamoja na kila mmoja kujiunga na bendi tofauti, lakini walikutana tena katika bendi ya Marquis du Zaire mwaka 1986 kabla Issa Nundu hajahamia MK. Group mwaka 1990.
Akiwa jijini Dar es Salaam, Issa Nundu alipigia bendi za Orchestra Makassy, Orchestra Super Matimila,  Maquis du  Zaire, MK. Group, Bana Marquis,  Super Kamanyola ya jijini Mwanza na La Capitale ‘Wazee Sugu’ ambayo aliitumikia hadi alipoanza kuugua na mauti kumkuta.
Alipokuwa katika bendi ya Makassy alikutana na waimbaji mahiri akiwemo Mbombo wa Mbomboka, Mzee Kitenzogu Makassy na Maliki Star na wengine wengi.
Wakati alipojiunga na Marquis du Zaire, wakati huo ikipiga katika ukumbi wa White House-Ubungo, alikuwa na miamba ya uimbaji akina Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mbuya Makonga ‘Adios’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, mapacha Kassalo Kyanga na Kyanga Songa, Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’, Mbombo wa Mbomboka, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Tshimanga Kalala Assosa, Masiya Radi ‘Dikubakuba’, Rahma Shaari, Anna Mwaole na Mary Mwanjelwa.
Akiwa Marquis aliimba peke yake wimbo wa Sikutegemea, ambao aliuimba kwa sauti yenye simanzi mno. 
Lakini pia alitunga wimbo wa Marusu uliorekodiwa studio za Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) mwaka 1989, ambapo solo limekung’utwa na Dekula Kahanga Vumbi.
Alipokwenda katika bendi ya MK Group iliyokuwa ikipiga muziki katika Hoteli ya New Africa, Issa Nundu alikutana na waimbaji mahiri akiwemo kiongozi wa bendi hiyo Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’, Kapaya Vivi na wengine wengi.
Nundu alijiunga na Bana Marquis iliyokuwa inaongozwa na Tshimanga Kalala Assosa mwaka 1994 akiwa pamoja na Anna Mwaole na Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’. Baadaye yeye na Mukumbule Lulembo ‘Parashi’ na Anna Mwaole walikwenda jijini Mwanza na kujiunga na bendi ya Super Kamanyola.

Mauti
Issa Nundu alifariki alfajiri ya Jumamosi Oktoba 25, 2014 katika Hospitali ya KCMC mjini Moshi alikokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na tatizo la kusinyaa kwa ubongo.
Mwanamuziki huyo aliamua kurudi kwao Congo lakini alipofika Kigoma alizidiwa na kulazwa huko kabla ya kuhamishiwa KCMC Moshi kwa matibabu zaidi. Alizikwa Jumanne Oktoba 28, 2014 mjini Moshi ambapo baba yake Said Issa Nundu alihudhuria mazishi hayo. Aliacha mjane na watoto kadhaa.


Comments