Featured Post

DAKTARI AKISAFIRI, ZAHANATI INAFUNGWA DODOMA

Zahanati ya Kijiji cha Malolo yenye mtumishi mmoja tu.

Na Daniel Mbega, Mpwapwa
WAKAZI wa Kijiji cha Malolo wilayani Mpwapwa wanapata changamoto kubwa ya huduma za afya ambapo zahanati pekee iliyopo hufungwa kila wakati Mganga Mfawidhi anaposafiri.
Uchunguzi wa MaendeleoVijijini umeonyesha kwamba, zahanati hiyo ina mtumishi mmoja tu, Elias Mlwande, ambaye ndiye mganga mfawidhi, na kutokana na kukosekana kwa watumishi, hulazimika kuifunga kila wakati anaposafiri, kuugua ama kuwa na dharura nyingine za kijamii.
MaendeleoVijijini ilizuru kijijini hapo hivi karibuni ambapo ilishuhudia nyumba ya mganga huyo mfawidhi pamoja na zahanati vikiwa vimetiwa kufuli baada ya kuwa safarini kwa siku tatu kwenda makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, takriban kilometa 150 kutoka kijijini hapo.
"Ni siku ya tatu sasa hakuna huduma, haya ni mateso makubwa," anasema Grace Machidya, mkazi wa kijiji hicho ambaye alikutwa akihangaika kutafuta usafiri wa bodaboda ili impeleke katika zahanati ya Al Jazeera iliyoko Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo katika Mkoa wa Iringa, umbali wa takriban kilometa 25 kutoka kijijini hapo, ili kumwahisha mwanaye wa miaka miwili aliye mgonjwa.
Mwanaye huyo ana homa kali na pia anaharisha na msaada ambao alitarajia kuupata katika zahanati ya Kijiji cha Malolo hapo baada ya kukuta imefungwa kwa siku ya tatu sasa kutokana na ofisa afya kusafiri.
“Ningejua ningekwenda tu moja kwa moja, kwa sababu tumezowea kutibiwa nje ya kijiji, zahanati gani kila siku imefungwa hakuna huduma?” anasema kwa masikitiko.
Lakini anasema, hata kama zahanati hiyo ingekuwa wazi, huenda mwanaye asingeweza kupata huduma kwa sababu hata dawa za malaria tu, ugonjwa unaoua watoto wengi nchini Tanzania, ni shida kupatikana.
Hawezi kutumia usafiri wa gari kwa sababu huduma hiyo haipo, hivyo njia pekee ni kutafuta bodaboda ambayo ataikodi kwa Shs. 10,000 ili imfikishe huko zahanati.
"Hii ni mara ya pili nakuja hapa, mara ya kwanza nilikuja wiki tatu zilizopita, zahanati ilikuwa imefungwa ambapo niliambiwa mganga alikuwa amefuata dawa wilayani, mjini Mpwapwa, sikupata huduma nikalazimika kwenda Ruaha Mbuyuni. Leo nimeambiwa kwamba amepeleka ripoti ya utendaji huko Halmashauri,” anasema.
Hata hivyo, anasema ni gharama kubwa kwenda Ruaha, kwani si kila mtu atakayekuwa na uwezo wa kukodi bodaboda kwa Shs. 20,000 kwa maana ya kwenda na kurudi, achilia mbali uhakika na usalama wa usafiri huo ulivyo, hasa unapokuwa na mgonjwa mahtuti.
Jengo jipya la zahanati katika Kijiji cha Malolo.
Ikiwa mpakani kabisa mwa mikoa ya Dodoma, Iringa na Morogoro, zahanati hiyo ya Malolo ndiyo pekee kwa wananchi wa kijiji hicho chenye wakazi 2,600 kutoka katika vitongoji sita, na iko umbali wa kilometa 155 kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, ambapo siyo tu usafiri hakuna kutoka hapo, bali njia yenyewe imejaa makorongo pamoja na mawe yakiambatana na milima.
Mwandishi wa makala haya alishuhudia zahanati hiyo ikiwa imefungwa, ambapo baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Malolo walisema, hiyo ilikuwa siku ya tatu tangu mganga mfawidhi wa zahanati hiyo, Elias Mlwande, aliposafiri.
“Hapa ni kawaida, wakati mwingine inaweza kufungwa hadi wiki mbili, tumeshazowea kwenda kutibiwa huko Morogoro na Iringa ambako ni karibu na kuna usafiri na huduma za uhakika kuliko hapa kijijini au kwenda Mpwapwa,” anasema Julius Mapalilo, mkazi wa kijiji hicho.
Mapalilo anasema, wakati mwingine hulazimika kuvuka mto kwenda Kijiji cha Malolo ya wilayani Kilosa ama kwenda zahanati ya Al Jazeera Ruaha Mbuyuni au Hospitali ya Misheni ya Mtandika wilayani Kilolo mkoani Iringa.
“Siyo ajabu, tunakwenda pia Hospitali ya Misheni Ilula au Hospitali ya Mtakatifu Kizito ya Mikumi, ambayo ni ya misheni pia. Huko kuna huduma nzuri na usafiri ni wa uhakika,” anaongeza Mapalilo.
Uchunguzi umebaini pia kwamba, ni vigumu kufanya kazi katika kijiji hicho kutokana na changamoto ya miundombinu, hususan usafiri, licha ya kwamba kama kuna mgonjwa mahututi gari la wagonjwa linaweza kuitwa kutoka Mpwapwa.
Hakuna maduka ya dawa ya binafsi kijijini hapo na mtu pekee anayehudumu kwenye zahanati ni ofisa afya, ambaye kwa sasa ni Bwana Mlwande.
Bosco Paulo Mwaluga, Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ambaye pia ndiye mtendaji wa Kijiji cha Malolo, anasema zahanati hiyo haina mtumishi mwingine zaidi ya ofisa afya.
"Tunajua kwamba mazingira ni magumu ya kufanyia kazi. Licha ya miundombinu ya mawasiliano ukiwemo usafiri, lakini pia kuna uhaba mkubwa wa dawa," anasema Mwaluga, ambaye anathibitisha kwamba ofisa afya huyo ana siku ya tatu tangu alipoondoka kwenda Halmashauri Mpwapwa kupeleka ripoti ya kila mwezi.
Mwaluga anasema, amekuwa akipokea taarifa ya bwana mganga kila anapotuma orodha ya dawa na vifaa tiba vinavyohitajika kutoka ofisi ya afya ya wilaya, lakini mara nyingi dawa hizo huchelewa na wakati mwingine si zote zinazoombwa ambazo hupelekwa.
"Hili ni tatizo sugu hasa kwa watoto ambao, kwa mujibu wa ripoti ya ofisa afya, ndio wanaongoza kwenye orodha ya wagonjwa,” anasema ofisa mtendaji huyo.
Anaeleza kwamba, kutokana na uhaba wa watumishi wa afya, zahanati hiyo hufungwa hata kwa wiki mbili ikitokea bwana mganga anahudhuria mafunzo au hata akipatwa na dharura binafsi.
Imeelezwa kwamba, tangu ilipofungiliwa, zahanati hiyo haijawahi kuwa na watumishi zaidi ya mmoja, huku changamoto ya nyumba za watumishi nayo ikiwa kubwa.
Mwaluga anasema kwamba, zahanati hiyo iliwahi kufungwa kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu baada ya kukosekana kwa nyumba ya watumishi hadi wananchi walipoamua kujitolea kujenga nyumba moja ambayo ndiyo anayoishi Bwana Mlwande.
Nyumba ya Mganga Mfawidhi ikiwa imetiwa kufuli.
“Nilipohamia hapa mwaka 2011 hali ilikuwa mbaya, nikalazimika kutafuta nyumba kwa msamaria mwema mmoja mkazi wa Ruaha Mbuyuni ambayo tulimpatia ofisa afya aliyekuwepo, Nyamboga, lakini mwenye nyumba alisema alitakiwa kukaa kwa muda hadi kiangazi kwani yeye aliitumia nyumba hiyo kama ghala la kuhifadhia vitunguu vyake,” anasema Mwaluga.
Hata hivyo, ilipofika Juni 2011, mwenye nyumba aliitaka kwa kuwa tayari alikuwa amekwishavuna vitunguu na kutaka kuvihifadhi, hali iliyompa wakati mgumu ofisa afya ambaye alilazimika kujihamisha mwenyewe.
“Ni hapo ndipo Mkurugenzi aligoma kutoa mtumishi mwingine wa afya mpaka nyumba ijengwe na aje aikague, tukajenga na alipokuja kuikagua ndipo akatuletea mtumishi wa sasa, Mlwande,” anasema.
Lakini Mwaluga anasema, kukoseka kwa watumishi, hususan wauguzi wa kike, kumekuwa changamoto kubwa ambapo jamii imekuwa na mtazamo hasi kuhusu huduma nyingine za afya, hususan suala la afya ya uzazi pamoja na mahudhurio ya kliniki ya wajawazito.
Anasema kwamba, utumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango ni duni na kwamba baadhi ya wanaume wanawazuia wake zao wajawazito kwenda kliniki kwa kuwa tu mtumishi aliyepo ni mwanamume.
“Ni mtazamo hasi tu, wanasema hawawezi kuwaruhusu wake zao ‘wakapekuliwa’ na mwanamume mwenzao,” anasema akirejea maelezo ya wananchi wanaowakata wake zao kuhudhuria kliniki.
Licha ya kuwa na changamoto ya uhaba wa wauguzi, Mwaluga anasema kwamba, serikali ya kijiji imeweza kuwahamasisha wananchi wake kujenga zahanati bora ambayo uongozi wa Kata unaona inafaa kuwa Kituo cha Afya pindi itakapokamilika.
Anasema jengo hilo ambalo linakaribia kumailika limetumia matofali 24,000 ya kuchoma, ambapo kila kitongoji kati ya sita kilichangia matofali 4,000, tripu tano za mchanga na tripu tano za mawe.
“Mdadu mwingine amechangia tripu 10 za mchanga wakati wafugaji katika umoja wao wamechangia Shs. 5 milioni kufanikisha ujenzi huo,” anasema Mwaluga.
Aidha, anasema kwamba, halmashauri ya kijiji iliamua kuuza ekari 50 za kijiji kwa Shs. 100,000 kila moja ambapo Shs. 5 milioni zilizopatikana zitasaidia katika shughuli za ujenzi.
“Halmashauri ilitupatia Shs. 10 milioni kwa ajili ya ukarabati wa jengo la zahanati, lakini tukaona kwamba itakuwa ni upotevu mkubwa wa fedha kukarabati jengo ambalo limezeeka, hivyo tukaamua kujenga linguine, fedha hizo zipo katika akaunti na zitatumika kwa shughuli nyingine.
“Kwa vile huku misitu ni mikubwa na miti ya mbao inapatikana ya kutosha, tutakapokuwa tayari tutakwenda kuomba kibali maalum idara ya misitu ili tuwalipe watu watupasulie mbao za kupaulia,” anaongeza ofisa mtendaji huyo.
Mwaluga anasema kwamba, mara watakapokamlisha ujenzi, wataanza kujenga nyumba za watumishi ili halmashauri iweze kuwapatia watumishi wengine wa kutosha kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Wataalam wa afya wanasema kwamba, uhaba wa wauguzi na wafamasia ni miongoni mwa sababu zinazowanyima wananchi haki ya matibabu nchini Tanzania, huku serikali ya awamu ya tano ikiwa imezuia ajira zote.
Inaelezwa kwamba, hata kama Bohari Kuu ya Dawa (MSD) itakuwa na akiba ya kutosha ya dawa muhimu, hospitali za wilaya zinakosa dawa nyingi muhimu kutokana na ukosefu wa watumishi ambao wanaweza kuandaa orodha ya mahitaji, jambo ambalo linaathiri upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na zahanati za vijijini.
Takwimu rasimu za watumishi wa idara ya afya zinaonyesha kwamba, hadi Desemba 2014, kulikuwa na watumishi 69,864 nchi nzima.
Mkoa wa Dodoma wenye watu 2,187,955 una jumla ya watumishi wa afya 2,861.

Comments