Featured Post

WILAYA YA NEWALA MKOANI MTWARA INAKABILIWA NA UHABA MKUBWA WA MAOFISA UGANI NA MIFUGO

Mwezeshaji kutoka Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (OFAB), Dk. Emmarold Mneney (kulia), akitoa mafunzo ya siku moja ya kilimo chenye tija  kwa wakulima wa Mkoa wa Mtwara  kwenye Maonyesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Ngongo mkoani Lindi jana.


Mkulima Lukia Hassan Nalamba kutoka Kata ya Nanyamba akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo kwenye mafunzo hayo.
Wakulima wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Mkulima Mohamed Ismail kutoka Kijiji cha Mnyambe wilayani Newala akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mkulima Shazili Mpangalika kutoka Kijiji cha Mikumbi wilayani Newala akizungumzia changamoto ya wakulima kuhamia maeneo mengine kufuata bei kubwa ya mazao.
Wakulima kutoka Wilaya ya Nanyumbu wakiwa kwenye 
semina hiyo.
Mratibu wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Philbert Nyinondi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA), akizungumza na wakulima hao
Mafunzo yakitolewa.


Na Dotto Mwaibale, Lindi

HALMASHAURI ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maofisa ugani na mifugo jambo linalochangia kuporomoka kwa kilimo wilayani humo.

Hayo yalielezwa na mkulima wa wilaya hiyo,  Mohamed Ismail katika mafunzo ya siku moja kwa wakulima wa Mkoa wa Mtwara yenye lengo la kuwasaidia kulima kilimo chenye manufaa yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia kwa mwezeshaji kutoka Jukwaa la Bioteknolojia kwa maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk. Hamalord Mneney katika maonyesho ya kitaifa ya wakulima Nanenane yanayoendelea Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi jana.

"Tunachangamoto kubwa ya uhaba wa maofisa ugani na mifugo hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kutokuwepo kwa ufanisi wa kazi na kushindwa kuwafikia wakulima hivyo kuzorotesha shughuli za kilimo na mifugo kwa ujumla" alisema Ismail.

Alisema katika kata moja yenye vijiji sita ni ofisa ugani mmoja tu ndiye anayehudumia wakulima katika vijiji hivyo tena bila ya kuwa na usafiri wa uhakika hivyo  kumfanya ashindwe kuwafikia wakulima kuwapa mafunzo na kujua changamoto walizonazo.

Alisema kutokana na uhaba wa maofisa kilimo na mifugo imesababisha ofisa ugani kujikuta akifanya kazi mbili ya ugani na mifugo na ofisa mifugo naye akifanya kazi ya ugani na ambayo hakuisomea.

"Tunaiomba serikali kuliangalia jambo ili kwa karibu zaidi kwani bila ya kufanya hivyo Tanzania ya kuelekea uchumi wa viwanda katika wilaya hiyo itakuwa ni ndoto" alisema Ismail.

Mkulima Shezili Mpangalika kutoka katika wilaya hiyo alisema kilimo cha kuhamahama kinachosababishwa na kuporomoka kwa bei ya zao la mbaazi kimechangia kuwepo kwa mimba za utotoni kwa wanafunzi na wavulana kuacha masomo kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi wa wazazi na walezi wao wanaokimbia nyumba zao kwenda maeneo mengine kufanya kilimo chenye tija.

Alisema katika wilaya hiyo wakulima wengi wamekuwa wakikimbia kutokana na bei ya mbaazi kushuka kutoka shilingi 500 hadi kufikia 400 na hivyo kuhamua kwenda wilayani Kilwa kulima ufuta ambao bei yake ni kati ya shilingi 2000 hadi 2500.

"Wazazi wanapoondoka na kwenda Kilwa ukaa huko kwa zaidi ya miezi sita na huwaacha watoto wao bila ya kuwa na uangalizi maalumu wakilelewa na babu na bibi zao tena bila ya kuwa na chakula hivyo kujikuta wakijiingiza katika vitendo vya ngono isiyo salama na kupata mimba huku wavulana wakiacha shule na kushinda kijijini wakizurura.

Wakulima hao walizitaja changamoto walizonazo ni mazao yao kushambuliwa na wadudu waharibifu, ukame, kukosekana kwa elimu ya kilimo,pembejeo, mvua kutonyesha kwa wakati na zao la mhogo kushambuliwa na ugonjwa wa batobato na michirizi kahawia na kuwa changamoto hizo zinalingana na wilaya zingine za mkoa wa Mtwara

Mwezeshaji kutoka Jukwaa la Bioteknolojia kwa maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk. Hamalord Mneney aliwataka wakulima hao kuacha kilimo cha mazoea na kufanya kilimo cha Kisayansi kutokana na hali ya sasa ya tabia nchi.

"Wakulima mnapaswa kubadilika na kuacha kulima kilimo cha zamani hivi sasa hali imebadilika hivyo mnatakiwa kufanya kilimo cha Sayansi na Teknolojia chenye tija na kufuata maelekezo ya wataalamu na kuachana na kilimo cha zamani" alisema Dk. Mneney.

Mratibu wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Philbert Nyinondi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA), aliwataka wakulima hao kujiongeza zaidi na kubadili matumizi ya simu zao kwa kuzitumia  kutafuta masoko na kuwasiliana na wenzao kuelezana changamoto walizonazo kwenye kilimo badala ya kutumia kwa matumizi yasiyo na tija.

Wakulima walionufaika na mafunzo hayo ni kutoka Wilaya za Mtwara mjini, Vijijini, Nanyamba, Tandahimba, Newala, Masasi na Nanyumbu.

Comments