Featured Post

WANAFUNZI BORA SASA KUPEWA UDHAMINI BADALA YA MIKOPO

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Simon Msanjila.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
SERIKALI inafikiria kuwapatia udhamini (scholarships) wanafunzi wanaoshika nafasi 10 bora katika masomo ya sayansi badala ya mikopo ili kuhamasisha wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Hayo yameelezwa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Simon Msanjila, wakati wa sherehe za kuwatunuku wanafunzi waliofanya vizuri katika maonyesho ya Wanasayansi Chipukizi yaliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa ya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Profesa Msanjila amesema kwamba, amevutiwa na namna Shirika la Wanasayansi Chipukizi nchini Tanzania (YST) kwa kushirikiana na wadhamini mbalimbali wa maonyesho hayo, wanavyowazawadi washindi tuzo za udhamini, jambo ambalo ni zuri na linawapa motisha wanafunzi kubuni kazi bora zaidi.
“Tunawapongeza wadhamini wote, na serikali inafikiria kwamba ni vyema wanafunzi bora wakapatiwa ufadhili wa masomo badala ya mikopo kama ilivyo sasa,” alisema.
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, kwa mfumo wa sasa, wanafunzi wanaoshika nafasi 10 bora kitaifa, hata wale wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi, wamekuwa wakipanga foleni kuomba mikopo kama wengine.
Lakini ikiwa serikali itaamua kutumia mfumo huo wa kuwatunuku  ufadhili wa moja kwa moja wa masomo yao ya elimu ya juu, itawasaidia kuwamotisha na kuchochea hamasa kwa wanafunzi wengine kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao, hususan ya sayansi.
Katika maonyesho ya Wanasayansi Chipukizi kila mwaka wanafunzi wanne washindi wa tuzo mbalimbali hupatiwa udhamini wa masomo ambapo mpaka sasa zaidi ya wanafunzi 20 wamekwishanufaika na ufadhili huo katika kozi za sayansi za elimu ya juu tangu maonyesho hayo yalipoanzishwa na YST mwaka 2011.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, ufadhili huo unajumuisha gharama zote za ada, pesa za kujikimu, mafunzo ya vitendo na vifaa vya kujifunzia ikiwemo kompyuta mpakato (Laptop).
Kwa upande mwingine, Profesa Msanjila amesema, katika kutekeleza azma ya kuifanya Tanzania ya Viwanda pamoja na kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2017-2022) na Dira ya Taifa ya Maendeleo (2000-2025) inayotaka kuona Tanzania ya uchumi wa kati, serikali inaunga mkono jitihada za ubunifu katika sayansi na teknolojia.
“Fedha zipo, na kwa bahati nzuri Wizara ya Elimu ni miongoni mwa wizara zilizopatiwa bajeti nono kwa mwaka 2017/2018, hivyo kazi za ubunifu ni muhimu kuendelezwa,” amesema.
Ameongeza kusema kwamba, ni vizuri uwepo utaratibu mzuri wa kufuatilia kazi bora za ubunifu zinazoshinda kwenye maonyesho ya YST ili kuziendeleza.
Lakini MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, kwa upande mmoja tayari serikali imeanza kutekeleza suala la ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa kike wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi, utaratibu ambao umeanza kutumika katika mwaka 2017/2018.
Utaratibu huo ni kupitia Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere unaosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambao ulitangaza mapema kutoa nafasi za udhamini (scholarships) ili kuongeza hamasa na ufaulu kwa wanafunzi wa kike hapa nchini katika masomo ya Hisabati na Sayansi.
Taarifa kamili hii hapa:



Kwa ujumla, maonyesho ya YST yameweza kuleta hamasa kubwa kwa wanafunzi kupenda masomo ya sayansi, huku viongozi mbalimbali wa kiserikali wakivutiwa na ubunifu unaofanywa na vijana hao katika sayansi na teknolojia.
Katika kilele cha maonyesho ya mwaka 2016, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, aliwataka wanafunzi kupenda masomo ya sayansi ambayo yanatoa fursa nyingi kwa sasa katika ulimwengu wa teknolojia.
Aidha, katika mwaka 2015,  Rais mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi ammbaye alikuwa mgeni rasmi katika maonyesho hayo, aliwataka walimu katika shule za msingi na sekondari kutumia lugha ya Kiswahili kufundisha sayansi, kwani lugha hiyo inaeleweka vizuri.
“Kiswahili ni lugha inayoeleweka vizuri, si kwa wanafunzi tu, bali hata kwa watu wengine, hivyo ni vyema walimu wakaweka mkazo katika kuitumia kwenye masomo ya sayansi,” MaendeleoVijijini ilimkariri akisema wakati huo.
“Nimepita kwenye maonyesho haya, baadhi ya wanafunzi walikuwa wananiuliza ‘tukueleze kwa Kiswahili au kwa Kiingereza’, nikasema tumieni lugha yoyote tu. Wengine wamenieleza Kiingereza na wengine Kiswahili.
“Lakini nataka niwaambie, walionieleza kwa Kiswahili, pamoja na utafiti wao kuwa katika lugha ya Kiingereza, walifafanua vizuri sana na nikasema ‘aah, kumbe Kiswahili kinaweza kutumika kufundisha vizuri sayansi,” alisema.
Aliongeza kusema kwamba, yeye wakati anaingia darasa la tano, mwalimu wake wa sayansi alikuwa rais wa Scotland, lakini alimfundisha sayansi kwa Kiswahili na ndio msingi wake mkubwa wa kulifahamu vyema somo la sayansi.

Comments