WAKULIMA WAASWA KUJENGA UHUSIANO MZURI NA WAFANYABIASHARA

Na Mathias Canal, Lindi
Baada ya kuimarisha umoja na ushirikiano wa wakulima wenyewe ni vema wakulima wakajenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara ili kutokutoa mianya kwa madalali ambao mara nyingi wamekuwa wakilalamikiwa kuwa wananunua mazao ya wakulima kwa bei ya chini huku wao wakiyauza kwa bei ya juu.

Hayo yameelezwa na baadhi ya wadau wa kilimo waliozuru katika sherehe za maonesho ya Wakulima Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.

Wamesema kuwa Ni vema kukatengenezwa mfumo mzuri utakaowasaidia wakulima kupata taarifa sahihi za masoko na bei halisi ya bidhaa kupitia umoja wao, kuliko kuendelea kusherehekea kila mwaka wakati wakulima bado wanateseka na bei kandamizi za madalali.

Suala hili linaenda sambamba na kaulimbiu ya sherehe za Nane Nane mwaka huu ambayo ni “Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati”  
Juma Msembi ni moja ya washiriki wa Maonesho ya Nanenane anasema serikali inapaswa kuzidi kuwa kiunganishi kizuri kati ya wakulima na soko, ili wakulima wasikate tamaa katika kuzalisha chakula kingi.

Anasema kuwa anaamini Sherehe hizi zitakuwa chachu ya kujadili na kutathmini maendeleo ya sekta ya kilimo na changamoto zinazowakabili wakulima na kuangalia namna ya kuzitatua.

Katika Maonesho haya wakulima watajifunza mbinu bora za kisasa za kilimo zitakazowawezesha kupata mazao mengi na kuinua kipato chao.

Msembi anatoa wito kwa wakulima na mashirika kujitokeza katika maonesho hayo kwa sababu watapata fursa ya kujifunza mambo mengi na kubadilishana uzoefu na wataalamu mbalimbali wa kilimo.

MWISHO