- Get link
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- Other Apps
Rais wa Kwanza wa Bunge la Afrika, Getrude Mongela amesema wakati umefika kwa wanawake kuajiri na kufukuza.
Alitoa kauli hiyo katika sherehe za Uzinduzi wa Jukwaa la Kuwaendeleza Wanawake Afrika (WAA) iliyofanyika kwenye hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam. Jukwaa hilo linasimamiwa na Taasisi ya Graca Machel.
Mama Mongela alikuwa akijibu maswali ya waandishi kuhusiana na hisia zake baada ya uzinduzi na majadiliano ya Kitabu “Women Creating Wealth” ambazo ni simulizi la wanawake wajasiriamali katika bara la Afrika, waliofanikiwa na safari yao katika ujasiriamali.
Alisema ingawa wakati wa Mwalimu Nyerere juhudi zilifanyika kuwawezesha wanawake, kundi hilo lilibaki kufanyakazi za kufungasha au kushona, lakini kizazi cha sasa kimeendelea kiasi ya kwamba kina uwezo wa kufanya uwekezaji na kuwa waajiri.
Alisema amefurahishwa sana na maelezo ya ndani ya kitabu hasa safari mbalimbali za wanawake kuanzia vijana na wale wa kati ambao wamethubutu na kuonesha njia ya ujasiriamali bila kukata tamaa na hivyo kuwa mfano kwa wengine.
Alisema katika mahojiano hayo kuwa wanawake kwa sasa wakati umefika wa kuwa na viwanda vikubwa, kumiliki na kuwezesha mabadiliko ambayo yatachochea maendeleo binafsi, familia na hata taifa.
Anasema wanawake waliachwa nyuma kutokana na wanaume kutotambua au kutokubali uwezo wa mwanamke na sasa vijana wanaonesha kwamba wanawake wanaweza na wanathubutu.
Pamoja na kazi hizo amesema wakati umefika wa wanawake kutumia akili ili siku moja kipuri kitengenezwe na mdada na watu wajisikie fahari kwenda kukitumia.
Akizungumzia kitabu hicho Mwasisi wa mtandao wa She Inspires Her, Lisa O'Donoghue-Lindy amesema kwamba kinatoa maelezo ya safari ya wajasiriamali wa kike, dhiki zao, changamoto na namna walivyoanzisha ujasiriamali wakati mwingine wakiwa na fedha kidogo kiasi cha dola 23 katika mifuko yao.
Alisema kitabu hicho kimeandaliwa kutoka wajasiriamali mbalimbali takribani 60 wa bara la Afrika kwa lengo la kutoa hamasa kwa wajasiriamali wengine ambao wanachipukia au wale ambao wanataka kuthubutu.
Alisema kwamba maelezo yaliyomo ndani ya kitabu hicho ni binafsi mno, kwani walizungumzia ubunifu na safari ya kiuchumi waliyoianzisha wadada hao na namna waliyvoondoka katika changamoto mbalimbali. Aidha kimelenga kushawishi watoa maamuzi kutoa nafasi ya wanawake kuendelea na kuona umuhimu wao katika kuimarisha maendeleo na usawa.
Miongoni mwa watu waliomo ndani ya kitabu hicho Jacqueline Mengi, Esther Karin Mngodo, Devotha Minzi na Mtendaji wa kampuni ya uhandisi ya Mount Carmel Seline Mwenelupembe. Wapo pia wajasiriamali kutoka Kenya, Uganda na Kongo ya Kinshasa.
Akizungumza kuhusu kuwamo katika kitabu hicho Jacqueline Mengi alisema anajisikia furaha kuwa mfano wa kuwafundisha wengine, akisema kwamba anaona fahari kuwaambia wanawake wenzake kwamba kujiamini ni silaha muhimu na kwamba ukishinda nafsi ni lazima ufanikiwe.
Aliwataka wanawake kushikamana na kupeana ushirikiano katika safari hiyo.
Naye Renee Ngamau Mtangazaji wa redio kipindi cha Capital in the Morning kutoka kampuni ya Capital Group Limited alitoa hongera kwa kukazabuti kwa washiriki wote waliomo katika kitabu kwamba wamefanyakazi moja muhimu ya kuonesha wanawake kwamba ujasiri na uthubutu ni kitu cha muhimu katika kuamua maisha yao binafsi. Alisema wanawake hao wameonesha kwamba kwa hali yoyote ile mwanamke akifanya maamuzi ya kuendelea mbele ataweza.
Anasema wanawake ndio msingi mkubwa wa maendeleo kwa kuwa asilimia 90 ya pato lao hulirejesha katika familia kwa shughuli mbalimbali za kijamii.
Akielezea siri ya mafanikio yake Devotha Minzi ambaye kwa sasa ana kampuni ya ushauri kuhusu namna ya kuingia katika ujasiriamali, alisema kwamba mambo ambayo yamekuwa yakimfikirisha sana ni kuhusu namna ya wahitaji wanavyoweza kupata fedha benki na wala si benki kutoa fedha.
Minzi ambaye aliwahi kuajiriwa Benki Kuu aliacha kazi yake hiyo na kuingia katika kuwekeza katika taasisi ya fedha kabla ya kuachana nayo na kuanzisha kampuni ya ushauri.
Akizungumza katika mkutano huo alisema kwamba wakati anaingia katika ujasiriamali alitambua kwamba kuna shida ya kujiweka sawa kuchukua fedha za Benki na hivyo kuona haja ya kuwapa elimu wanawake kuhusu Benki kuwapa fedha na si kunung’unika kwamba hawapewi fedha.
Alisema ni vyema wanawake kufanyakazi zao kwa akili zaidi na kuhakikisha kwamba wamejiandaa vyema katika kuhakikisha kwamba mahitaji yao yanatekelezeka kwa kutambua mambo ambayo ni muhimu katika uwekezaji na kuwa na nguvu.
Anasema mpaka alipofika yeye amekumbana ana changamoto nyingi lakini la maana ni kuwa ana ratibu na anaangalia zaidi mahitaji na taratibu zake akiongeza kwamba kwa sasa amejikita kutoa ushauri wa kuwawezesha wanawake wenzake kukopesheka.
Alisema ni vyema watu wakabadilika kifikra na kutengeneza utaratibu ambao utawafanya benki wawape hela bila hata kuombwa.
Katika jukwaa hilo wanawake walipata nafasi pia ya kuhutubiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye aliwataka wanawake kusaidia serikali katika kuhakikisha uchumi unakua.
Comments
Post a Comment