Featured Post

NAIBU WAZIRI JAFO AZITAKA HALMASHAURI KUPELEKA VIJIJINI, TEKNOLOJIA NA PEMBEJEO BORA KWA WAKULIMA NA WAFUGAJI

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Suleiman Jafo akimkabidhi mshindi wa pili wa maonyesho ya nanenane kanda ya kati ambaye ni Benki Kuu ya Tanzania.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Suleiman Jafo akimkabidhi mshindi wa tatu wa maonyesho ya nanenane kanda ya kati ambaye ni Jeshi la Magereza.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Suleiman Jafo amezitaka halmashauri zote nchini kutekeleza jukumu lao la kuwapelekea wakulima wa vijijini teknolojia na pembejeo bora ili kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji mali.
Jafo ametoa rai hiyo jana wakati wa kilele cha maonyesho ya nanenane kanda ya kati inayojumuisha mikoa ya Singida na Dodoma ambapo alipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali yalioonyesha shughuli za kilimo na ufugaji pamoja na sekta binafsi zinazosaidia katika kukuza uchumi.
Amesema kauli mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu ni “Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati” hivyo basi halmashauri zinatakiwa kuhakikisha mazao ya wakulima na wafugaji yanapata soko kwa kutoa elimu ya kuchakata na kufungasha bidhaa zao katika ubora unaokubalika sokoni ili mazao hayo yawe na thamani zaidi.
Jafo amesema halmashauri zote zinapaswa kutekeleza wajibu wao kwa kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa na huduma zote za msingi kama vile miundombinu ya Barabara, Umeme na Maji ili kuwavutia wawekezaji na hivyo kumsaidia mkulima na mfugaji kufikia uchumi wa kati.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Ole Nasha ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa kuendelea kuwezesha shughuli za kilimo nchini huku akitoa angalizo la kutowasahau wakulima wasio na uwezo.
Ole Nasha amesema Benki hiyo isitoe mikopo kwa wakulima wakubwa na wenye uwezo tu bali isisahau jukumu la kuwafikia wakulima wasio na uwezo ili waweze kupata mikopo na kuweza kulima kisasa kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Wakati huo huo Naibu waziri Jafo ametoa Wito kwa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kuamua kuufanya Mkoa wa Dodoma hasa Viwanja vya Nzuguni kuwa Kituo cha Kudumu cha Maonesho ya nanenane kitaifa kutokana na Kijiografia kuwa katikati na Makao Makuu ya nchi na hivyo kuwa rahisi kwa Kanda zote nchini na hata nchi za jirani kuja kushiriki Maonesho ya Nane Nane.
Jafo amesema hayo akiunga mkono kauli iliyotolewa na Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba aliyesema Serikali inafikiria kuachana na utaratibu wa kuhamisha  hamisha Maonesho ya kitaifa ya Nane Nane kwenye Kanda mbalimbali na badala yake kuwa na kituo kimoja cha Kitaifa kama ilivyo kwa maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanavyofanyika Dar es Salaam pekee.
Jafo amesema Uwanja wa Nane Nane Nzuguni unahitaji kufanyiwa uwekezaji na uendelezaji wa miundombinu yake kama barabara, umeme na maji na kuboreshwa huduma mbalimbali na kuzitaka Mamlaka za Serikali za Mikoa ya Dodoma na Singida kuweka mkakati wa kuendeleza miundombinu hiyo kwa kuwa baada ya uwekezaji mkubwa uwanja huo utarejesha mapato mengi.
Ameongeza kuwa Serikali za Mikoa ya Singida na Dodoma inaweza kufanikisha ukarabati huo kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Taasisi kama Benki ya Uwekezaji TIB na Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB.
Washindi wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati yaliyoanza tangu Agosti Mosi ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lililoibuka kuwa Mshindi wa jumla wa Maonesho ya Mwaka huu, likifuatiwa na Benki Kuu ya Tanzania ikiwa mshindi wa pili na Mshindi wa tatu akiwa ni Jeshi la Magereza.

Comments