Featured Post

MAKAMU WA RAIS AZINDUA JUKWAA LA KUWAENDELEZA WANAWAKE AFRIKA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa Sherehe za Uzinduzi wa Jukwaa la Kuwaendeleza  Wanawake  Afrika iliyofanyika kwenye hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema jukumu kubwa la nchi za Afrika ni kuhakikisha zinaweka mazingira wezeshi ya kuwaendeleza wanawake katika nyanja zote.
Samia ameyasema hayo leo kwenye Uzinduzi wa Jukwaa la Kuwawezesha na Kuwaendeleza  Wanawake Afrika lililoandaliwa na Asasi ya Graca Machel na kufanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es salaam.

Makamu wa Rais alisema pamoja na kuwepo kwa jitihada mbalimbali za kuwaendeleza wanawake bado mazingira hayampi nafasi mwanamke haswa yule anayeishi kijijini.
Aidha, aliainisha baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na sheria na sera zilizopo ambazo bado zinawanyima wanawake fursa ya kumiliki ardhi pamoja na haki ya kurithi hata kama haki hizo zipo kisheria.
"Hii inatokana na utekelezaji mbaya wa sheria, unaosababishwa na uwepo wa  mianya ya ubaguzi kwenye kwenye sheria hizo jambo ambalo linakinzana na mfumo rasmi wa kisheria zilizowekwa," alisema Makamu wa Rais.
Aidha alisema “Inasikitisha kuona kuwa ni zaidi ya miaka 20 baada ya Ulingo wa Beijing; kukamilika kwa utekelezaji wa Malengo ya Milenia; pamoja na kuanza kwa utekelezaji wa Malengo mapya ya Maendeleo Endelevu ambapo kuna lengo la pekee linalosimamia masuala ya usawa na kuwawezesha wanawake na watoto wa kike, bado kuna baadhi wanawake miongoni mwetu ambao wapo kwenye lindi la umasikini, wanafanya kazi kwenye mazingira magumu; kupata kipato tofauti na wanaume kwa kazi sawa; kutokuwa na sauti ya kufanya maamuzi kwenye maisha yao wala maamuzi ya kisiasa; kutokuwa na fursa ya kumiliki na haki ya kurithi ardhi, kukosa huduma za mikopo, afya na elimu; Ingawa wamezingirwa na fursa tofauti na mazingira wezeshi bado wanawake wengi wa Afrika hawachukuliwi kuwa sawa na wenzao wa kiume mbele ya sheria.
 Alimalizia kwa kusema kuwa muda umefika sasa kwa wanawake kuwa mfano, Kuungana na kuinuana ilikuweza kumkomboa mwanamke wa Kiafrika na kuhakikisha hamna anayebaki nyuma kwenye fursa za maendeleo. 



Comments