Featured Post

KAMUGISHA: TANZANIA YA VIWANDA ITAFANIKIWA TUKICHANGIA MAENDELEO YA SAYANSI KAMA TUNAVYOCHANGIA HARUSI


Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa Shirika la Young Scientist Tanzania (YST), Gosbert Kamugisha, akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu Maonyesho ya Sita ya Wanasayansi Chipukizi yanayotaraji kuanza Agosti 8 mpaka 9, 2017 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Royal Dutch Shell Afrika Mashariki ambaye pia ni Mkurugenzi wa BG Tanzania, ambayo ni kampuni tanzu ya Shell, Marc den Hartog.


Mkurugenzi Mtendaji wa Shell Afrika Mashariki na BG Tanzania, Marc den Hartog, akizungumza na wanahabari kuhusu udhamini wa kampuni yake katika Maonyesho ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania ambayo yanalenga kuandaa kizazi cha magwiji wa sayansi nchini.
Muasisi Mwenza na Mkurugenzi wa Ushauri wa Masuala ya Sayansi wa Shirika la YST, Joseph Clowry, akizungumzia mafanikio ya tasisi hiyo ndani ya miaka sita tangu ianze kuendesha maonyesho hayo.
Meneja Uhusiano wa Nje kutoka kampuni ya BG Tanzania, ambayo ni kampuni tanzu ya Royal Dutch Shell, Patricia Mhondo, akifafanua jambo juu ya udhamini wa kampuni hiyo katika kuwawezesha wanasayansi chipukizi nchini Tanzania.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog

MALENGO ya kuona Tanzania ya Viwanda yatafanikiwa ikiwa jamii itawekeza katika kuchangia maendeleo ya elimu ya sayansi kwa wanasayansi chipukizi ili kuwapata wataalam wengi zaidi.
Kuliko kuchangia sherehe za harusi zinazogharimu fedha nyingi kwa tukio la mara moja, ni vyema wanajamii wakachangia fedha hizo kwa watoto wao kujifunza masomo ya sayansi ambayo yataleta tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo hii na Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa Shirika la Wanasayansi Chipukizi Tanzania (Young Scientists Tanzania – YST), Dkt. Gosbert Kamugisha, wakati akizungumza na wanahabari kuhusu maonyesho ya sita ya wanasayansi hao chipukizi yanayotarajiwa kuanza Agosti 8 – 9, 2017.
“Wanajamii tunachanga fedha nyingi kwa ajili ya sherehe za harusi, lakini tunashindwa kuwekeza kwenye sayansi na teknolojia ambako ndiko uliko msingi mkubwa wa maendeleo ya taifa lolote.
“Siyo ajabu ukakuta tunachangia shilingi laki moja hadi laki tano kwa ajili ya kuburudika kwa vinywaji na vyakula kwenye sherehe ya siku moja tu, lakini watoto wetu hawa maskini wanahitaji walau hata shilingi elfu hamsini tu kuwaendeleza kwenye masomo ya sayansi. Ni vyema tubadilike ili tuweze kuifikia ndoto ya kuona Tanzania ya Viwanda,” amesema Dkt. Kamugisha.
Dkt. Kamugisha amesema kwamba, malengo ya serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda yatatimia ikiwa tu wananchi watabadili mtazamo wa kuchangia maendeleo ya sayansi na teknolojia na akawaomba wadau kuunganisha nguvu ili kuwaandaa wanasayansi chipukizi.
“Tunaweza kuanzisha viwanda vingi, lakini kama hatutakuwa na msingi imara wa wataalam wa sayansi na teknolojia itakuwa ni kazi bure,” amesema Dkt. Kamugisha na kuongeza kwamba, uwepo wa wanasayansi wengi utasaidia hapo baadaye kufanya kazi na kuviendeleza viwanda hivyo vitakavyoanzishwa kutimiza azma ya serikali.
Amesema ni muhimu kuwekeza kwa wanafunzi ambao wanaonyesha kuvutiwa na masomo ya sayansi kwani wao ndiyo watakaoendesha viwanda siku za usoni.

Maonyesho ya sita
Kuhusu maonyesho ya sita ya YST, Dkt. Kamugisha amesema mwaka huu yatashirikisha jumla ya wanafunzi 200 na walimu 100 kutoka shule 100 za sekondari za Tanzania – Bara na Visiwani.
Maonyesho hayo yanatarajiwa kufanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ambapo pia yatashuhudia wanafunzi waalikwa 850 wakihudhuria kutoka shule mbalimbali za Dar es Salaam.
Dkt. Kamugisha amesema kwamba, tangu walipoanzisha maonyesho hayo miaka sita iliyopita wameshuhudia mafanikio makubwa ambapo wanafunzi katika shule nyingi wamehamasika kupenda na kuchukua masomo ya sayansi tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma
“Ingawa bado kuna uhaba wa walimu, lakini shule nyingi ambazo zimepata kushiriki maonyesho haya zimeonekana kufanya vizuri zaidi kwenye masomo ya sayansi ikilinganishwa na shule ambazo hazijapata kushiriki,” amesema.
Ameipongeza serikali kutokana na juhudi kubwa inazozifanya hivi sasa za kupeleka vifaa mbalimbali vya maabara katika shule nyingi za sekondari na kuwapa fursa wanafunzi ya kujifunza kwa vitendo.
Hata hivyo, amesema kuwa kazi nyingi zinazoletwa kwenye maonyesho hayo siyo zile zinazoandaliwa kwenye maabara tu, bali ni za ubunifu wa wanafunzi wenyewe katika mambo mbalimbali ya kijamii na kutafuta namna ya kukabiliana na changamoto hizo.
"Maeneo yanayoguswa ni afya, kilimo, usalama wa chakula, mawasiliano, nishati na mazingira, elimu, usalama katika usafirishaji na mengine yanayogusa jamii," amesema.
Ameongeza kusema kwamba, ingawa wamekuwa wakizitembelea shule nyingi za sekondari kuwafundisha na kuwaelekeza walimu na wanafunzi namna ya kubuni kazi za kisayansi na teknolojia, lakini kwa sasa inaonekana mwamko ni mkubwa kwa shule nyingi kiasi kwamba hata maombi ya ushiriki yamevuka kiwango.
“Awali tulianza na shule sita tu na tulikuwa tunakwenda kuwaomba washiriki, lakini hivi sasa katika shule nyingi kunakuwepo na ushindani wa wanafunzi wenyewe ambapo huchaguliwa wanafunzi wawili ambao wazo lao linakuwa bora zaidi ili washiriki kwenye mashindano ya kitaifa,” amesema.

Udhamini
Kwa miaka mitano sasa mashindano hayo yamekuwa na wadhamini mbalimbali huku mdhamini mkuu akiwa kampuni ya British Gas (BG) ambayo ni kampuni tanzu ya Royal Dutch Shell.
Kufuatia udhamini huo, wanafunzi na walimu wote wanaoshiriki maonyesho hayo huwa hawachangii gharama yoyote kuanzia nauli za kuwatoa mikoani, malazi na chakula, gharama ambazo hulipwa kupitia udhamini huo.
“Tunaishukuru sana BG Tanzania kwa kufanikisha maonyesho haya na tunawaomba wadhamini wengine wajitokeze zaidi ili tuendelee kuwaandaa wanasayansi chipukizi kwa ustawi wa taifa letu,” amesema Dkt. Kamugisha.
Kwa upande wake, Mwanzilishi Mwenza wa YST, Joseph Crowry kutoka Ireland, amewaomba Watanzania kuhamasika na kuwaendeleza watoto wao katika masomo ya sayansi ili kuwajengea msingi imara.
Amepongeza jitihada za vyombo vya habari katika kuhamasisha maonyesho hayo kila mwaka, lakini akaomba jitihada hizo ziendelee zaidi ili kujenga msingi imara wa wanajamii kupenda sayansi.
“Kule Ireland tumekuwa na maonyesho kama haya kwa zaidi ya miaka 50 sasa na kwa hakika, kila maonyesho yanapofanyika jiji la Dublin husimama kila mtu akiwa na shauku ya kwenda kutazama kazi za ubunifu wa sayansi na teknolojia,” amesema Crowry.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba Ireland imepiga hatua kubwa sana katika sayansi kiasi kwamba makampuni makubwa ya teknolojia na mitandao, ikiwemo Google, yameweka makao yao makuu huko.
Mkurugenzi Mtendaji wa Royal Shell Afrika Mashariki ambaye pia ni Mkurugenzi wa BG Tanzania, Marc den Hartog, amesema kampuni hiyo imevutiwa kufadhili mashindano hayo kwa kuwa ni mradi unaolenga kuwajenga wanasayansi.

“Ni mradi mzuri mno ndiyo sababu hatuoni hasara kuwekeza fedha nyingi katika hili, tunataka tuwe na wanasayansi, wabunifu na watalaam wa teknolojia wa kutosha,” amesema.

Comments