DKT NCHIMBI: WATENDAJI WATAIFISHWE MALI ZAO KUFIDIA MILIONI 15 ZA WANANCHI WALIZOIBA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza na madiwani na watendaji katika baraza maalumu la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Manyoni la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.

Watendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Manyoni wakifuatilia kwa umakini hoja zikijadiliwa katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Manyoni wakifuatilia kwa umakini hoja zikijadiliwa katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Miraji Mtaturu akizungumza katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Mkaguzi wa ndani na Mweka hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni wakipitia hoja zilizowasilishwa katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ameagiza na kutoa mwezi mmoja mali za watendaji 21 wa vijiji katika halmashauri ya Wilaya ya Manyoni zitaifishwe na kuuzwa ili kufidia fedha walizotumia za chakula cha njaa katika kipindi cha mwaka 2012.

Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali ambapo kulikuwa na hoja ya watendaji wa vijiji 30 waliokusanya kwa wananchi shilingi milioni 15,268,700 kwa ajili ya chakula cha njaa na hawakuziwasilisha katika halmashauri hiyo.

Amesema kitendo hicho ni wizi na hakistahili kuvumiliwa licha ya watendaji tisa kurejesha kiasi cha shilingi milioni 3,277,000 na hivyo kusalia watendaji 21 wanaodaiwa shilingi milioni 11,991,700 walizokusanya.

“Huu ni wizi na hatutauvumilia, hao watendaji wa vijiji hakikisheni wanarudisha fedha za serikali, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi, anzisheni utaratibu wa mahakama tembezi muwafuate huko waliko, kamateni mbuzi, kuku, uzeni tupate hiyo fedha na zoezi hilo lifanyike ndani ya mwezi wa nane” ameagiza Dkt Nchimbi.

Ameongeza kwa kusema kuwa, “watendaji hawa nasikia wengine wameshaandikiwa barua za onyo zaidi ya mara tatu, kwanini wanaendelea kuwa watumishi wa umma?, kwanini wasikae pembeni tupate watanzania wengine wazalendo wazibe nafasi hizo?. Hawa hawafai kuwa watumishi wa umma, ila hakikisheni kwanza fedha inarudi ndipo hatu nyingine zichukuliwe”.

Dkt. Nchimbi amesema hoja nyingi katika halmashauri hiyo zimetokana na uzembe wa watumishi pamoja na kutegemea taarifa za makaratasi badala ya kutembelea maeneo husika kujionea hali halisi ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za serikali mpaka ngazi ya vijiji na mitaa.

Aidha amemtaka mwanasheria wa halmashauri na mkaguzi wa ndani kuisaidia halmashauri kuepuka kuwa na hoja nyingi zinazoepukika kwa kutoa ushauri sahihi na kwa wakati, huku akiwasisitiza watumishi wote kubadilika, kuacha uzemba na kufanya kazi kwa mazoea bali waendane na kasi ya serikali ya awamu ya tano.

Kwa upande wake Mkaguzi wa Nje wa Hesabu za Serikali Anna Kakunguru amewataka viongozi kuhakikisha wanasimamia ili hoja zifungwe kabla ya watendaji waliosababisha hoja hizo kustaafu, kuhama au kuachishwa kazi ili kuepuka hasara.

Kakunguru amesema imekuwa ikichukua muda mrefu kwa halmashauri kufuta hoja jambo linalosababisha waliotengeneza hoja hizo kutopatikana na kuzijibu ili halmashauri isibaki na hoja nyingi.

Ameongeza kuwa uwepo wa hoja za serikali ni kiashiria kuwa kuna sehemu katika utendaji wa halmshauri kuna mapungufu au umelegalega na hivyo halmashauri inapaswa kushirikiana na Mkaguzi wa nje na ndani ili kurekebisha na kuzuia kabisa udhaifu huo.

Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Miraji Mtaturu amesema atahakikishika kufikia tarehe 30 Agosti watendaji 21 watakuwa wamerejesha fedha walizochukua za wananchi huku akiagiza apatiwe orodha ya watendaji hao ili aweze kuwashughulikia vizuri.

Mtaturu ameongeza kuwa atasimamia kikamilifu ili mahakama tembezi itakayoanzishwa iweze kutekeleza agizo hilo na kurejesha fedha hizo na endapo watatokea watendaji watakaokaidi kutoa ushirikiano atawachukulia hatua zaidi za kisheria.

Ameongeza kwa kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manyoni kuweka utaratibu wa kukutana na watendaji wake mara mbili kwa mwezi ili wajadili namna ya kufuta hoja zilizojitokeza pamoja na kupeana maelekezo ya namna ya kuepuka kutengeneza hoja nyingine.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singda Dkt Rehema Nchimbi amewashauri madiwani wa halmashauri hiyo kutenga ekari tano kwa ajili ya kilimo cha korosho katika kata zao ili kuongeza kipato kwa wananchi wao, kutunza mazingira na kufikia lengo la kuwa wazalishaji wakubwa wa korosho nchini.

Dkt Nchimbi pia ameshauri madiwani hao na watendaji kutofanya mzaha na waliovamia misitu ya hifadhi kwakuwa wanahatarisha usalama wa raia kutokana na wanyama kutoka katika hifadhi na kuvamia makazi ya watu.

Amesema “Tusifanye mzaha kwa hili, na hakuna siasa hapa, sio kwamba tunawajali wanyama kuliko wananchi hapana, watu wameingia katika maeneo ya hifadhi wamesababisha wanyama watoke huko na kuja kuvamia watu, mpaka sasa wananchi saba wameshafariki, tuwe wakali kweli kwa wavamizi hawa”.

Halmashauri ya Manyoni imepata imepata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali na hoja zilizojadiliwa katika baraza hilo maalumu ni 74 ambazo zilikuwa hazijafungwa kwa kipindi cha mwaka 2012/13 mpaka 2015/16.