ZITTO KABWE: MAPATO YA SERIKALI UTATA MTUPU!


Nipo kwenye ziara ya kutembelea kat a za Jimbo la Kigoma Mjini katika utaratibu niliojiwekea wa kushauriana na wananchi kila mwaka kabla ya Bunge la Bajeti. Jambo moja kubwa ambalo nimekutana nalo ni malalamiko ya Wananchi kuhusu huduma za manispaa yetu ikiwemo kuchelewa kwa miradi ya maendeleo ikiwemo barabara za mitaa ( Kigoma ina mvua nyingi Sana kiasili kwa hiyo Mitaa huharibika mno na makorongo kujengeka katikati ya baadhi ya mitaa). 

Nimewaambia wananchi kwamba uwezo wa Mapato wa Manispaa yetu ni mdogo mno. Tulikuwa na Matarajio ya kukusanya TShs 3.4 bilioni mwaka 2016/17 baada ya kufanya mabadiliko ya tozo na ushuru mbalimbali. Hata kabla ya mwaka wa fedha kuanza Halmashauri zote nchini zikanyanganywa chanzo cha Mapato cha Kodi za Majengo (Property Taxes). Kwa Manispaa ya Kigoma Ujiji hili ni punguzo la shilingi 1.2 bilioni kutoka katika makadirio yake. Baadaye Serikali ilitangaza kwamba mapato haya yatarejeshwa kwenye Manispaa zetu, lakini mpaka sasa hakuna thumni iliyorejeshwa.

Nimewaambia wananchi kwamba hata Hizo zilizobakia shilingi 2.2 bilioni nazo tumeshindwa kuzikusanya kwa sababu Waziri wa TAMISEMI ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano hajaidhinisha sheria ndogo tulizowasilisha kwake. Kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa (Sheria namba 7 na 8 za 1982) ni lazima Waziri wa TAMISEMI aidhinishe sheria ndogo ndipo zianze kutumika. Manispaa yetu na Manispaa nyengine nchini zimeshindwa kukusanya vyanzo vipya vya mapato na tozo mpya kwa sababu Rais hajasaini Sheria ndogo na hivyo kukosesha Mapato Halmashauri zetu. Sisi Kigoma Ujiji Manispaa tumeshapoteza theluthi nyengine ya Mapato (shilingi 1bn ) kwa uchelewaji huu peke yake.

Kwa Mapato ya ndani ya Manispaa zetu nchini, mwaka 2016/17 ni mwaka uliopotea (A Year Lost) katika kipindi cha uongozi wa nchi unaopigania Sana mapato kuongezeka.

Hata Fedha za maendeleo kutoka Serikali kuu kuja kwenye Manispaa zimekuwa ni kidogo Sana. Kwa mfano Kwa Manispaa ya Kigoma Ujiji mwaka 2016/17 tulitarajia kupata shilingi 9.9 bilioni Kama ruzuku ya miradi ya Maendeleo lakini hadi Desemba 2016, tulikuwa tumepata shilingi 1.4 bilioni tu sawa na 14.14% ya Bajeti.

Katika mazingira Kama haya Manispaa haiwezi kuleta Maendeleo Kwa watu wake isipokuwa Kwa miradi ya wafadhili tu. Baadhi ya Wafadhili wanaosaidia na watakaosaidia Kigoma Ujiji ni pamoja na Benki ya Dunia na Serikali ya Ubelgiji ( miundombinu na Hifadhi ya Jamii), Serikali ya Kuwait ( Kilimo), Serikali ya Uingereza ( Elimu- EQUIP na P4R ), Serikali ya Danmark ( Mazingira ya Uwekezaji ) na Shirika la PSPF ( Uwekezaji wa The Great Lakes Gateway Market - Mwanga Sokoni).

Manispaa nayo inajitahidi kuongeza vyanzo vya mapato na kuanzisha miradi ya kukuza uzalishaji ikiwemo Mfumo wa Hifadhi ya Jamii ili kuwezesha wananchi kuweka akiba, kupata bima ya afya na kupata mikopo nafuu. Kujenga Manispaa ya Kijamaa katika dimbwi la Sera za kibepari ni changamoto kubwa tunayokumbana nayo kama ACT Wazalendo Hivi sasa. Miradi mingine ni Kilimo cha Michikichi kuzalisha Mawese na Ujenzi wa Ujiji City. Hata hivyo bado tunahitaji vyanzo vya Sasa vya Mapato ili kukuza vyanzo Hivi vipya. Naomba nashauri mambo mawili;

Ninamsihi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, airudishe TAMISEMI eneo lake la asili ambalo ni Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwezesha ufanisi wa kutoa huduma Kwa wananchi. Mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa Bajeti unaonyesha kwamba Rais ana mambo mengi Sana na majukumu makubwa mno. Vinginevyo tunakwenda kupoteza mwaka mwengine. Waziri Mkuu atakuwa na nafasi zaidi ya kusaini Sheria ndogo za Mamlaka za Serikali za Mitaa na pia kuweza kufuatilia utekelezaji wake Kwa umakini na ukaribu mkubwa.

Natumai kwamba Bajeti ya mwaka 2017/16 itarejesha kodi za majengo ( property taxes ) Kwa Manispaa na Majiji yetu nchini. Hii itawezesha Halmashauri zetu kukusanya mapato ya kutosha kuweza kutoa huduma kwa wananchi wetu.  Tuchukulie kuwa mwaka 2016/17 ulikuwa mwaka wa majaribio na 2017/18 tuanze kazi. Bila uimara wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, nchi haitakwenda. Tusijidanganye Kabisa.