YA PAULO MAKONDA, ‘FEDHA ZA BANGI’ NA NGUVU YA ‘MAFIA WA TANZANIA’Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
JIMBO la Colorado nchini Marekani linasemekana ndilo lenye uchumi unaokua kwa kasi zaidi kuliko majimbo mengine yote 51 yaliyobakia.
Ukuaji huo unasemekana unatokana na kitendo cha Serikali ya jimbo hilo kuhalalisha matumuizi ya bangi na mimea kama hiyo tangu Januari 2014.
Kwa sasa jimboni humo maduka ya kuuza bangi na mimea kama hiyo yanaingiza jumla ya Dola 295 milioni 295 (sawa na Shs. 649 bilioni za Tanzania) huku Serikali ikipata jumla ya Dola 51 milioni (sawa na Shs. 112.2 bilioni za Tanzania) kama kodi ya mapato.

Hata hivyo, bangi pamoja na mihadarati mingine imepigwa marufuku sehemu nyingi duniani ikiwemo Tanzania kwa sababu inahatarisha afya za watu na kuathiri nguvu kazi.
Licha ya kupigwa marufuku kimataifa, lakini bangi na dawa nyingine za kulevya zimetamalaki na biashara hiyo ndiyo inayoongoza kwa mapato makubwa kati ya biashara zote haramu duniani.
Biashara ya dawa za kulevya inafanywa na watu wakubwa wenye mitandao imara, yakiwemo makundi hatari ya kihalifu, kwani fedha zinazotokana na biashara hiyo ndizo zinazotumika kufadhili makundi ya kigaidi ulimwenguni, kuvuruga chaguzi mbalimbali kwa kuwaweka watu wanaowapenda ambao watalinda maslahi yao, zinatumika pia kuleta machafuko katika nchi zenye rasilimali ili wakati serikali zinapambana na waasi, wao watakuwa wanachota rasilimali hizo kiulaini.
Makundi haya yana nguvu za ajabu na yamepenya katika taasisi nyingi nyeti. Kwa maana hiyo, ni rahisi ‘kuwashughulikia’ wote wenye viherehere ambao wanataka kukwamisha biashara zao.
Wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda, alipotangaza rasmi operesheni ya kuwakamata vigogo wa dawa za kulevya alikuwa na nia nzuri tu ya kuendeleza mapambano yaliyokubaliwa na serikali nyingi duniani.
Lakini hakujua kwamba, alikuwa ameingia kwenye anga za miungu-watu wasioguswa (The Untouchable Godfathers), ambao kwa miaka mingi wameimarisha mtandao wao hapa Tanzania.
Orodha aliyopewa Makonda haina tofauti kubwa kama ile ambayo ilipelekwa Ikulu mwaka 2006 na kundi la viongozi wa dini ikiwataja vigogo wote wa dawa za kulevya wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wa dini.
Haina tofauti na ile ambayo imekuwa ikitajwa na wafungwa wa Kitanzania walioko Uchina na Hong Kong ambako wanatumikia adhabu mbalimbali vikiwemo vifungo vya maisha kutokana na kukamatwa na dawa za kulevya wakiwa kama ‘punda wabeba mizigo’ (drug mules).
Licha ya orodha hizo kutolewa kitambo, hakuna kiongozi yeyote mwenye dhamana aliyewahi kuthubutu kulivalia njuga suala hilo kwa utekelezaji, na kwa kadiri miaka inavyosonga mbele, orodha hiyo imeendelea kuwa ndefu ikiwataja hadi watoto wa vigogo wa serikali na wafanyabiashara tunaowaheshimu katika jamii.
Makonda, akifanya kazi kwa niaba ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, alikuwa na nia njema ya kuonyesha utendaji wa serikali katika masuala mazito ambayo yamewashinda viongozi wengi, lakini hakujua kwamba wahusika kwenye mtandao huo wana mkono mrefu na wanaweza siyo tu kumharibia kazi na maisha yake, bali kuivuruga operesheni nzima na ikakosa maana.
Leo hii Makonda anaumia kwa mashambulizi mfululizo ambayo yamefichua mambo yake binafsi yaliyofichika kwa sababu ya uthubutu wake katika kupambana na dawa za kulevya.
Hakujua kwamba, lile kundi la watu waliohisi kubanwa na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, lilikuwa limejiimarisha Tanzania tangu mwaka 1992 walipoliua Azimio la Arusha kule Zanzibar na kuleta Azimio la Zanzibar la ‘Soko Huria’ ambalo lilizaa ubepari uchwara.
Ni ubepari huo uchwara ambao katika kipindi cha miaka zaidi ya 20 tangu kuuawa kwa Azimio la Arusha tumeshuhudia matabaka mbalimbali yalivyowaathiri Watanzania. Waliokuwa viongozi enzi za Mwalimu, ambao walijiona wamebanwa, wakatumia fursa hiyo kujilimbikizia mali, wakauza kila kitu, wakaruhusu na mifumo mingine kutamalaki, japo kwa siri, na kuibariki kwamba ndiyo inayofaa.
Rushwa, ambayo katika kipindi cha Mwalimu ilikuwa msamiati mgeni (ingawa ilikuwepo kwa siri), leo hii imetawala na imeundiwa majina mengi ya kuihalalisha. Wengine wanasema ni takrima, bakhshishi, asante, mlungula, mshiko na majina mengineyo mengi.
Hii yote imetokana na kuruhusu mfumo hatari wa Mafia utamalaki, mfumo mbaya ambao kwa sasa ndio unaotumiwa hata kutuchagulia viongozi wetu, na wahusika wakuu wengi wao wamo katika biashara ya dawa za kulevya.
Hapa sizungumzii Kisiwa cha Mafia kule Pwani, nazungumzia kundi lile hatari la Mafia ‘Morte alla Francia, Italia anela!’ (Kifo kwa Mfaransa ni Kilio kwa Mtaliano), lililoibuka katika Visiwa vya Sicily, Italia katikati ya karne ya 19 na kuogopwa na wengi duniani kutokana na vitendo vyao.
Pengine vijana wengi hawalielewi vizuri kundi hili hatari, lakini niwakumbushe tu kwamba, kundi hili mojawapo ya majukumu yake ni kuwalinda mafisadi, kusafirisha silaha, kuhujumu mikataba, kutengeneza fedha bandia, usafirishaji wa dawa za kulevya, ufisadi, fedha chafu, rushwa kwenye siasa na mambo mengine haramu ikiwemo hata kuua wapinzani wao.
Ni mara ngapi tumeshuhudia mfumo mbovu katika upatikanaji wa viongozi, ufisadi uliotamalaki, rushwa iliyoota mizizi, mikataba feki na uporaji wa rasilimali zetu ikiwemo ujangili na usafirishaji wa wanyama hai. Hawa Mafia ndio wanaohusika.
Mafia, au Cosa Nostra, yaani ‘Kitu Chetu’, ndilo linaloitesa nchi hii kama tunavyoona mikataba mibovu ya madini, mafuta na gesi, utaifishaji wa ardhi yetu kwa kisingizio cha uwekezaji na mambo mengine kadha wa kadha.
Tunashuhudia kashfa za vigogo wengi wa Serikali kuficha matrilioni ya fedha nje ya nchi, tukio ambalo huko nyuma lilikuwa adimu. Wanafanya hivi kwa maslahi ya nani? Uzalendo umekwenda wapi? Ni aibu kubwa.
Chaguzi mbalimbali zimegubikwa na wimbi la rushwa na ufisadi, tunapata viongozi kwa njia haramu na baadaye tunatambua kwamba, viongozi hao wamewekwa na kambi fulani, ili baadaye watetee maslahi ya kambi hiyo na ikiwezekana kufumbia macho vitendo vya kihalifu viendelee. Haya yote yanatuthibitishia kwamba Mafia iko miongoni mwetu, ndiyo inayoweka mashinikizo ya kuwapata viongozi.
Leo hii tunachaguliwa viongozi, yaani watu wanapitishwa madirishani ili watuongoze, bila ridhaa yetu. Kinachofanyika ni kwa kundi hili kuwaandaa watu ambao lenyewe linadhani watalitumikia kwa maslahi yao.
Na limefanikiwa sana, tunaona zoezi la ubinafsishaji lilivyoua mashirika ya umma ingawa tunasadikishwa kwamba ni shinikizo la Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia, lakini dhahiri limefanywa kwa manufaa ya kundi fulani likiwahusisha na viongozi.
Tazama kashfa ya EPA ambayo tunaona kampuni nyingi za mifukoni ndizo zilizochota mabilioni ya fedha, na tunaelezwa kwamba fedha hizo ndizo zilizotumika kuwapitisha baadhi ya viongozi kupitia ‘dirishani!’
Badala ya kuwashughulikia ipasavyo ikiwemo kutaifisha mali zao, tukaona jinsi watu hao walivyoelezwa ‘kishkaji’ kwamba warejeshe wenyewe fedha hizo. Wengi hawakushtakiwa mpaka leo.
Kumbuka pia kashfa ya Tegeta Escrow ambayo iliwahusisha hadi vigogo wa Ikulu waliochota mamilioni ya fedha huku wakitumia viroba kubebea.
Huku mitaani wapo watu wengi ambao ‘wana ubia’ na viongozi wa Serikali kiasi kwamba wamekuwa kama miungu-watu. Hawaguswi, na ukiwasogelea watakwambia ‘viongozi wote wa serikali wako chini yao’!
Nyerere aliweza kuidhibiti hali hiyo alipomweka ndani yule Giriki aliyekuwa akitamba kwamba “Serikali yote iko mfukoni mwake”. Lakini kwa sasa hakuna awezaye kufanya hivyo, kwa sababu “Wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu!”
Tumeruhusu wenyewe kuwa na ‘koo’ za akina ‘Gambino’, ‘Bonanno’, ‘Piana dei Greci’ ‘Francesco Cuccia’ na wengineo, na tutaendelea kushuhudia viongozi wakipitishwa madirishani kutuletea ‘tuwathibitishe’ ikiwa wale waliopo walipitia madirishani pia.
Hii ni hatari, ndugu zangu, na siyo ajabu katika siku zijazo tukasikia viongozi wetu wanaamrishwa wasifanye hiki ama wafanye hiki na kundi kama hilo. Si tumekubali wenyewe kuwa watumwa wa Mafia!?
Nyerere alionya kuhus hali hiyo mwaka 1995 alipowaasa wanaCCM na Watanzania wote kwamba tujihadhari na fedha za bangi ambazo zilikuwa zimelenga kutumika ili ‘mtu wao’ apitishwe na CCM kuwania urais katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.
Natambua wapo wengi, hata kwenye uongozi wa Serikali hii ya Awamu ya Tano, ambao wanaendelea kumchukia Mwalimu Nyerere kwa sababu ya siasa zake. Na wanamchukia kwa mengi.
Mara kadhaa wapinzani wa falsafa za Mwalimu wamekuwa ‘wakilazimika’ kumtaja ‘Baba wa Taifa’ pale tu wanapotaka kupigiwa makofi kwenye mikutano mbalimbali, ili waonekane wamesema jambo jema, lakini mioyoni mwao wamejaa unafiki na uzandiki na wanamchukia mno.
Kwahiyo, Makonda alijua anafanya kazi ya kizalendo kabisa, lakini badala yake anaonekana amejipalia makaa kwenye kazi na maisha yake binafsi kiasi kwamba hivi sasa ana hofu kubwa moyoni.
Mafia wa Tanzania wana mtandao mrefu. Nakumbuka lile sakata la mbunge mmoja ambaye kupitia kampuni yake ya uwindaji mwaka 2009 aliomba kibali cha kuwinda pundamilia 600! Inaelezwa kwamba alikuwa amepewa mkataba wa kusafirisha nyama ya pundamilia hao kwenda Mashariki ya Kati.
Ninakumbuka jinsi kwa mwaka 2011 Jeshi la Polisi lilikamata shehena kubwa kubwa za dawa za kulevya ambapo hadi kufikia Septemba lilikuwa limekamata jumla ya kilogramu 483 za dawa za kulevya mchanganyiko aina ya heroine na cocaine.
Miongoni mwa waliokamatwa mwaka huo alikuwemo mchungaji mmoja wa Kanisa la Lord Chosen Charismatic Church lililopo Kinondoni Biafra jijini Dar es Salaam aliyekutwa na kilogramu 81 za Cocaine nyumbani kwake Kunduchi Mtongani.
Pia watu watano – Ali Mirzaei Pirbaksh, raia wa Iran; Said Mrisho, mkazi wa Tandale; Aziz Juma Kizingiti, mkazi wa Magomeni Mapipa; Abdul Mtumwa Lukongo, mkazi wa Kariakoo na Hamidu Kitwana Karim walikamatwa Septemba 6, 2011 majira ya saa 3:30 usiku eneo la Africana Mbuyuni, wilayani Kinondoni wakiwa na kilogramu 97 za heroine.
Januari 12, 2012 majira ya saa 12:00 asubuhi Polisi walimkamata Morine Amatus Liyumba pamoja na wenzake katika eneo la Mchinga II mjini Lindi wakiwa na kilogramu 210 za heroine zenye thamani ya Shs. 6.3 bilioni. Morine alitajwa kuwa binti wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, marehemu Amatus Liyumba.
Morine ambaye wakati huo alikuwa na miaka 21 tu, alikamatwa pamoja na mfanyabiashara wa magari, Ismail Adamu au kwa jina lingine, Athuman Mohamed Nyaubi, 28, raia wa Tanzania anayeishi Afrika Kusini. Mwingine aliyekamatwa ni dereva, Hemed Said, 27, mkazi wa Mtoni, Temeke, Dar es Salaam ambaye pia ni mtoto wa mwenye nyumba yaliyokutwa madawa hayo na Pendo Mohamed Cheusi, 67, mkazi wa Lindi ambaye ni mmiliki wa nyumba hiyo.
Kukamatwa kwa watu hao kulikuja miezi michache tu baada ya Umoja wa Mataifa (UN), kuonya kuwa Afrika Mashariki imekuwa ikipokea kiasi kikubwa cha dawa ya heroine kutoka Afghanistan na Iran baada ya ukanda huo kuibuka njia rahisi ya kusafirisha dawa hizo kwenda Ulaya, Amerika Kaskazini na sehemu nyingine duniani.
Ripoti hiyo Umoja wa Mataifa ilimesema, wafanyabiashara wa dawa za kulevya, kwa kukabiliwa na ugumu katika kusafirisha mizigo kupitia Asia na Mashariki ya Kati, sasa wamegeukia Afrika, hasa Afrika Mashariki kwa kuwa ni kituo kikubwa cha kusafirisha heroine kwenda Ulaya na sehemu nyingine duniani.
Kukamatwa kwa binti wa Liyumba kuliibua mambo mengi, na ilielezwa kwamba, huyo alikuwa mmoja tu kati ya watoto wengi wa vigogo ambao wamekuwa wakihusishwa kwenye biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya.
Chanzo kimoja cha habari kilipata kueleza kwamba, wasafirishaji wa dawa za kulevya wana njia nyingi za kuwakwepa askari ambapo kinachofanyika ni kwamba kuna mtu anayetumwa kwenda kuchukua mzigo ‘Pele’ (yaani Brazil) au ‘Musharaf’ (yaani Pakistan) kupitia Iran.
“Huyu akishapakia mzigo(dawa za kulevya)anapanda ndege mpaka may be Dubai au nchi za Kusini mwa Afrika kama Msumbiji au Afrika Kusini. Huyu mtu akitoka na mzigo Brazil ama Pakistan/Iran kazi yake inakwisha baada ya kushuka airport ya moja ya nchi za Kusini mwa Afrika, ambako hashuki ovyo ovyo lazima kunakuwa na mchongo wa kushukia hapo, yaani mabosi wake wanakuwa wameshaseti mambo hapo airport husika hivyo jamaa anashuka hapo salama na kuingia mjini then anachukua hoteli.
“Hapo sasa anatumwa kijana kama huyu wa Liyumba kutoka hapa Bongo na passport yake ya karatasi anasafiri kwa njia ya barabara anapita boda ya Tanzania na Msumbiji anagonga passport yake hiyo ya karatasi kama kawaida hapo boda then aningia Msumbiji, anakwenda mpaka kwenye hiyo hoteli aliyofikia yule aliyetoka shamba, hapo wanabadilisha mzigo na huyu dogo aliyetoka Bongo anauchukua mzigo then anatambaa nao kivyake kwa njia ya barabara, anapita pale boda anagonga muhuri wa kumtoa Msumbiji, huyo anaingia zake Tanzania bila kushukiwa na yeyote kwa kuwa wanajua alikwenda mara moja tena na passport ya karatasi. Basi anasafiri mpaka Dar es Salaam anakabidhi mzigo anakula milioni zake 5 kwa safari hiyo ya siku kama 3 tu! Lengo la kwenda kumpokea yule ni kuficha ile mihuri ya visa za ‘Pele’ au ‘Musharaf’ zisionekane maana visa za nchi hizo zinajulikana na watu wa dawa za kulevya... Brazil utakwenda kufanya nini kama sio madawa tu..?” kinaeleza chanzo hicho.
Tukumbuke pia jinsi tembo wetu wanavyopopolewa na majangili. Ni mara ngapi tumewasikia mawaziri na vigogo wengine wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakitajwa kuhusika kwenye mitandao hiyo? Iliwezekanaje twiga wetu wakasafirishwa kwenye ndege wakati wapo maofisa wengi kila kona, wakiwemo wanausalama?
Haitoshi, zipo kampuni ambazo zinatajwa kuwa na uswahiba na vigogo wa serikali na zimekuwa zikifanya ujangili lakini zinatazamwa tu. Hii ndiyo mitandao ya ki-Mafia ninayoisema.
Itakumbukwa kwamba, Machi 2015 Polisi mkoani Arusha walilikamata gari la Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii ya Wengert Windrose Safaris, lenye namba za usajili T 655 ARR likiwa na shehena ya magunia 11 ya dawa za kulevya aina ya bangi iliyokuwa ikisafirishwa kwenda nchi jirani ya Kenya. Kampuni hiyo ilitajwa kuwa na uswahiba na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, Lazaro Nyalandu.
Kwahiyo, Makonda anaweza kuwa na makosa yake kama binadamu, lakini nguvu kubwa iliyommaliza ni mtandao wa ki-Mafia uliotamalaki nchini ambao unajihusisha na biashara nyingi haramu na hautaki kuingiliwa.
Ukiingia kwenye anga zao watakumaliza – iwe kwa maneno au hata kukupora uhai wako.
0656331974