Featured Post

TALIRI: TAASISI KONGWE YA UZALISHAJI NA UTAFITI WA MIFUGO BORA ILIYODHAMIRIA KUWAKOMBOA WAFUGAJI NCHINI




Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
Mpwapwa
KILOMETA mbili kutoka stendi ya mabasi Mpwapwa, upande wa kaskazini, kuna taasisi muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya mifugo nchini Tanzania, MaendeleoVijijini inaandika.
Taasisi hii ambayo kwa zaidi ya miongo 11 imepitia majina mengi, kwa sasa inaitwa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (Tanzania Livestock Research Institute – Taliri), ambayo imekuwa kitovu cha uzalishaji na utafiti wa mifugo nchini.

Yawezekana wafugaji wengi hawaijui taasisi hii, lakini kwa wale wachache ambao wanaifahamu wameweza kunufaika nayo kutokana na mifugo bora inayopatikana hapo pamoja na kuelekezwa mbinu bora za ufugaji wenye tija.
MaendeleoVijijini imetembelea mara kadhaa taasisi hiyo inayopatikana katika Latitude 60° 20’Kus na Longitude 36° - 30° 30’Mash mjini Mpwapwa katika Mkoa wa Dodoma, yapata umbali wa kilometa 430 kutoka Dar es Salaam na kilometa 112 kutoka Dodoma mjini.
Aidha, taasisi hiyo iko umbali wa kilometa 17 kutoka stesheni ya Gulwe kwenye Reli ya Kati na kilometa tano kutoka uwanja wa ndege wa Ilolo, ambako hata hivyo hakujawahi kutua ndege yoyote kwa zaidi miaka 10 sasa.
Ukifika katika taasisi hiyo utashangaa wakati utakapokutana na majengo ya mawe ambayo Dk. Eligy Mussa Shirima, Mkurugenzi Mkuu wa Taliri, anasema yalijengwa zaidi ya miaka 100 iliyopita na hayajawahi kupata ufa.
 Jengo la Utawala la Taliri-Mpwapwa ambalo lilijengwa na Wajerumani tangu mwaka 1905.
“Majengo mengi unayoyaona, likiwemo hili la utawala, yalijengwa na Wajerumani tangu mwaka 1905… humu ndani tumefanya maboresho tu kwa kuweka terazo (tiles), paa na dari nzuri, vinginevyo yako imara mno,” anasema Dk. Shirima.
Makao makuu ya Taliri yapo katika kituo hicho cha Mpwapwa ingawa yamekuwa yakihamishwa mara kwa mara.
Taasisi hiyo ilianzishwa na wakoloni wa Kijerumani mwaka 1905, kikiwa kama kituo cha utafiti wa mifugo ambapo kiliendelea mpaka baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Aidha, walijenga na josho la kuogeshea wanyama mwaka 1907, ambalo ndilo kongwe kuliko yote Afrika Mashariki.
Josho lililojengwa na Wajerumani mwaka 1907 ambalo linatumika mpaka leo.
Kabla ya kuhamia katika eneo la Kikombo kilipo hivi sasa, kituo hicho kilikuwa kimenzishwa mwaka 1903 katika Kijiji cha Godegode, takriban kilometa 20 kutoka Mpwapwa mjini.
Sababu za kuhamishia kituo hicho mjini Mpwapwa, kwa mujibu wa Dk. Eliakunda Kimbi, ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Taliri-Mpwapwa ambacho ni miongoni mwa vituo saba vya utafiti vilivyo chini ya Taliri, ni baada ya kushuhudia farasi na ng’ombe wao wengi wakifa kwa magonjwa ambayo hawakuwa wameyafahamu, hivyo kuamua kuanza utafiti.
“Baadaye ikagundulika kwamba wanyama hao walikuwa wakifa kwa ugonjwa wa Sotoka (Rinderpest), hivyo wakajenga josho la kuogeshea wanyama mwaka 1907. Josho hilo ndilo kongwe kuliko yote Afrika Mashariki,” anasema Dk. Kimbi.
MaendeleoVijijini imebaini kwamba, sababu za Wajerumani kuhamishia kituo hicho Mpwapwa, hasa katika eneo la mlimani, ni kutokana na mazingira yake tulivu ambayo yamelifanya eneo hilo kuwa tofauti na maeneo mengine ya Mkoa wa Dodoma ambao ni nusu-jangwa.
Eneo la shamba kubwa kilipo kituo lipo katika mwinuko wa meta 1,100 kutoka usawa wa bahari, wakati shamba jingine lililopo Kiboriani liko kwenye mwinuko wa meta 1,750 na shamba la chakula cha mifugo la Ilolo liko kwenye mwinuko wa meta 900 kutoka usawa wa bahari.
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, wastani wa mvua kwa mwaka kwenye eneo hilo ni 660mm na hutofautiana kutoka mwaka hadi mwaka ambapo pia kuna miaka inayokuwa na ukame wa muda mrefu. Asilimia 90 ya mvua hunyesha kati ya Desemba na Aprili, ingawa kunakuwepo na kipindi cha ukame mwezi Februari, kama ilivyo katika maeneo mengi ya mikoa ya Dodoma na Singida. Wastani wa chini wa joto ni nyuzijoto 15.5°C, na Agosti ndio mwezi wenye baridi sana (13.8°C). Wastani wa kiwango cha juu cha joto ni nyuzijoto 27.5°C, huku mwezi Novemba ukiwa na joto kali (30.2°C).
Udongo ni wa tifutifu uliochanganyika na kichanga hasa kwenye maeneo ya miteremko, wakati kwenye maeneo ya mabonde kuna udongo wa mfinyanzi. Udongo wote huo una kiwango kidogo cha naitorojeni na fosforasi ingawa madini ya potasiamu ni mengi. Udongo huu wote una kiwango cha kati ya pH 5.3 hadi 8.6 huku eneo hilo likiwa limetandwa na misitu ya miombo, mahogany, na mingineyo.
Aidha, MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, mazingira tulivu ya eneo hilo, na shughuli zilizokuwa zikifanywa na Wajerumani, vilikifanya kituo hicho kuwa miongoni mwa maeneo ambayo Waingereza waliyashambulia hasa mwaka 1916 wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, wakidhani Wajerumani walikuwa akificha silaha nzito.

Shughuli kuu za kituo wakati huo
Dk. Kimbi anasema kwamba, mnamo mwaka 1922 wakoloni Waingereza walianza kukihudumia kituo hicho na kuanzisha Maabara ya Utafiti wa Magonjwa ya Mifugo (Veterinary Pathology Laboratory).
Kuanzia mwaka 1924 hadi 1929 shughuli kuu za kituo hicho zikawa utafiti wa magonjwa ya Sotoka na Ndigana (Rinderpest and Trypanosomiasis), lakini sasa utafiti huo ukawa unafanyika kwa wanyama wote waliokuwepo kituoni hapo na maeneo ya jirani kwa vile ilionekana magonjwa hayo yalikuwa yakiwashambulia na wanyama wengine mbali ya farasi.
Zaidi ya dozi 50,000 za kuzuia Sotoka (anti-rinderpest serum) zilitolewa kila mwaka.
Makao makuu ya Idara ya Sayansi ya Mifugo na Utunzaji wa Wanyama, kama ilivyojulikana wakati huo wa ukoloni, yakahamia Mpwapwa kutoka Dar es Salaam mwaka 1929. 
Aidha, uboreshaji wa ng'ombe wa kienyeji wenye asili ya Iringa, Rungwe, Singida na Masailand ulikuwa umeanza mapema mwaka 1923.
“Kuanzia mwaka 1930 hadi 1938, utafiti wa utunzaji wa mifugo ulipata sura mpya baada ya kuletwa mtaalam wa madawa na malisho. Shughuli za uzalishaji wa mifugo zilipamba zaidi mwaka 1944 baada ya kuteuliwa mtaalam wa vijinasaba (geneticts). Taasisi Kuu ya Mifugo ikaanzishwa mwaka 1951, na wakati huo huo kituo kikaona umuhimu wa kuiendeleza sekta ya mifugo, hivyo kikaanzisha kituo cha mafunzo ambacho sasa kinajulikana kama Livestock Training Agency (LITA),” anasema.
Ni katika kipindi hicho ambapo Shaaban bin Robert (jinale la asili ni Shaaban bin Selemani), mtu mashuhuri katika historia ya Tanganyika hasa katika kuikuza lugha ya Kiswahili, alifanya kazi kituoni hapo.
MaendeleoVijijini imefika mpaka katika nyumba ambayo Shaaban Robert aliishi na ofisi aliyofanyia kazi, pamoja na kushuhudia minazi miwili kati ya mitatu ambayo aliipanda wakati huo.
Nyumba ambayo Shaaban Robert bin Selemani aliishi miaka ya 1950 wakati akifanya kazi katika Idara ya Mifugo ya Wakoloni.
Jengo ambalo lilitumiwa kama ofisi hata enzi za Shaaban Robert.
Dk. Kimbi anasema, makao makuu ya idara hiyo yalirejeshwa Dar es Salaam mwaka 1954 na kumwacha Ofisa Mkuu wa Mifugo hapo Mpwapwa ambaye alisimamia Maabara ya Utafiti, Kituo Kikuu cha Uzalishaji, na Utafiti wa Mifugo na Malisho.
Wanyama wa kufugwa waliokuwepo kituoni hapo walikuwa ng'ombe, nyati, kondoo, mbuzi, nguruwe, kuku na farasi.
Mnamo mwaka 1962 kulikuwa na mabadiliko ya muundo wa wizara na kukifanya kituo hicho kiitwe Kituo cha Majaribio ya Mifugo kikiwa kinahusika na mambo ya kilimo, utunzaji wa mifugo na uvuvi.
Mwaka 1966 Sera ya Maendeleo ya Mifugo iliyopitishwa na Bunge ikiwa inasisitiza umuhimu wa kueneza ng'ombe wenye ubora wa juu vijijini ilikifanya kituo kikazanie uzalishaji wa ng'ombe, ambapo sasa kikajulikana kama Kituo cha Uzalishaji wa Mifugo (Livestock Breeding Station). Mwishoni mwa miaka ya 1960 kituo hicho kikaitwa tena Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Mifugo kikiegemea zaidi maendeleo ya mifugo.
Kuanzia mwaka 1977 utafiti wa mafunzo na mifugo viligawanywa katika taasisi mbili tofauti, Taasisi ya Utafiti, ambayo kuanzia Julai 1981 ilijulikana kama Taasisi ya Uzalishaji na Utafiti wa Mifugo (LPRI) ikiwa chini ya Mkurugenzi na Chuo cha LITA kikawa chini ya Mkuu wa Chuo. Shirika la Utafiti wa Mifugo Tanzania (Taliro) lilianza kusimamia taasisi hiyo mwaka 1981 hadi lilipokufa mwaka 1989, na kuanzia hapo mpaka sasa taasisi hiyo pamoja na chuo viko chini ya Wizara inayoshughulikia mifugo japo imekuwa ikibadilishwa kila mara.
Hivi sasa taasisi hiyo inajishughulisha na uzalishaji wa ng'ombe aina ya Mpwapwa, Mbuzi wa Maziwa jamii ya Malya (Malya Blended Goat), Kuku wa Kienyeji, Malisho, Lishe, Matibabu ya Mifugo, na Utoaji wa Elimu kwa Wakulima na Wafugaji.
Taliri inasimamia jumla ya vituo saba vilivyoko katika agro-ikolojia tofauti nchini, ambavyo ni: Mpwapwa na Konga (Dodoma), Mabuki (Mwanza), Naliendele (Mtwara), Uyole (Mbeya), Tanga (Tanga), na West Kilimanjaro (Kilimanjaro).

Kituo cha Taliri-Mpwapwa na shughuli zake
Kimsingi, Taliri yenyewe imetokana na kituo hiki cha Mpwapwa, na ndiyo maana hata makao makuu yako hapo.
MaendeleoVijijini imeelezwa kwamba, Kituo cha Utafiti Mpwapwa kina raslimali mbalimbali, ikiwemo raslimali watu, ardhi na mifugo. Mpaka sasa kituo hicho kina watumishi 72 waliopo katika ajira ya kudumu na malipo ya uzeeni, hekta 8,556 za ardhi (zikijumuisha hekta 6,614 za shamba kuu la Kikombo, hekta 1,800 za shamba la Kiboryani na hekta 142 za shamba la Ilolo ambalo ni kwa ajili ya chakula cha mifugo), ng’ombe 853, mbuzi 309 na kuku 120.
Dk. Eliakunda Kimbi anasema, tafiti zinazofanyika hivi sasa kituoni hapo ni pamoja na: Utafiti wa ng’ombe aina ya Mpwapwa wanaofaa kwa maziwa na nyama unaolenga kuhifadhi aina hiyo ya koosafu, kuzalisha idadi ya kuwatosheleza kwa ajili ya wafugaji na kuimarisha kizazi (purity maintenance and stabilization).
Pia wanafanya utafiti wa ng’ombe bora wanaoweza kuzalisha maziwa mengi na wanaoweza kustahimili nyanda kame ambapo wanatumia vizazi vya Danish Red x Mpwapwa.
Wanatafiti ng’ombe bora wanaoweza kutoa nyama nyingi na wanaoweza kustahimili nyanda kame kwa kutumia vizazi vya Beef Master x Boran.
“Tunafanya utafiti unaolenga kuzalisha ng’ombe bora kwa kutumia viini tete (embryo transfer). Kwa kipindi cha majaribio tumeshazalisha ndama watano aina ya Bons Mara kutoka Afrika Kusini. Viini tete hivi vimepandishwa kwa ng’ombe wetu aina ya Mpwapwa Boran na Mpwapwa,” anasema Dk. Kimbi.
Dk. Kimbi anasema, wanafanya tafiti za kuhifadhi na kutathmini uwezo wa mifugo ya asili kutoka kwa wafugaji, miongoni mwa mifugo hiyo ni ng’ombe aina ya Singida White, Iringa Red na Ufipa pamoja na mbuzi aina ya Gogo White, Newala Goats, na Ujiji Goats.
MaendeleoVijijini imeelezwa pia kwamba, taasisi hiyo inafanya utafiti wa aina ya mbuzi mwenye uwezo wa uzalishaji mzuri wa nyama na maziwa (blended goats) kwenye mazingira ya wafugaji wa Tanzania ambapo kwa sasa kazi kubwa inayofanyika ni kuzalisha idadi kubwa ya kuwatosheleza wakulima na kuimarisha kizazi (purity maintenance and stabilization).
Aidha, anasema wamefanya utafiti kutathmini uwezo wa uzalishaji wa kuku wa asili kwa kuangalia aina nne za kuku hao ambao ni Kuchi, Kishingo, Horace na Sasamala.
“Tumefanya utafiti wa majani na mikunde mbalimbali kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa mbegu za malisho bora kwa wafugaji ambapo kwa sasa jumla ya aina 80 za malisho zinahifadhiwa katika hifadhi ya vinasaba vya malisho (Gene Bank) hapa kituoni,” anasema Dk. Kimbi.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, msimu wa 2015/2016 kituo hicho kilizalisha kiasi cha malisho (hay) mikate 26,108 ambayo 56% iliuzwa kwa wafugaji na 44% ilitumika kwa ajili ya mifugo ya kituo.
Dk. Kimbi amebainisha kwamba, wanafanya utafiti na uzalishaji wa nguruwe bora na kuwasambaza kwa wafugaji, lakini pia wanafanya utafiti wa vyakula mbadala vya nguruwe unaolenga kupunguza gharama za uzalishaji.
“Tunafanya utafiti wa mnyororo wa thamani wa maziwa unaolenga kuboresha ukusanyaji na usindikaji wa maziwa kwa wafugaji wa nyanda kame.
“Hapa nchini, mradi huu unafanyika katika wilaya za Chamwino na Manispaa ya Dodoma ambapo unawashirikisha wafugaji 600. Wadau wengine washiriki ni pamoja na wazalishaji wa maziwa wakubwa, kati na wadogo, wakusanyaji na wauzaji wa maziwa, wachakataji wa maziwa, walaji wa maziwa, watafiti na wagani,” anafafanua Dk. Kimbi.
Aidha, Taliri inafanya utafiti unaolenga kuongeza tija ya uzalishaji wa maziwa kwa wafugaji wadogo hadi wakubwa katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Iringa na Mbeya, mradi unaotekelezwa kwa ushirikiano baina ya Taliri-Mpwapwa, Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI), Chuo Kikuu cha New England – Australia na Chuo Kikuu cha Scotchland (SURC).
Taliri pia inafanya utafiti wa uendelezaji na uboreshaji wa kuku wastahimilivu wa mazingira ya Tanzania ambao unafanyika katika mikoa ya Simiyu, Mwanza, Singida, Dodoma, Mbeya, Njombe, Lindi, Mtwara, Morogoro na Tanga.
“Mkoani Dodoma, utafiti huu unafanyika wilaya za Chamwino na Bahi, ambapo kila wilaya mradi umewashirikisha wafugaji 160 na idadi ya kuku waliosambazwa ni 4,400,” anaongeza Dk. Kimbi.
Dk. Kimbi anasema kwamba, wanafanya utafiti unaolenga kutoa teknolojia bora ya udhibiti wa maambukizi ya minyoo kwa mifugo na wakati huo huo wanasambaza mifugo bora ya ng’ombe, mbuzi na kuku na malisho kwa wafugaji na vikundi vya wafugaji kwa ajili ya utafiti na uzalishaji.

Mikakati iliyopo
Ili kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo, Taliri imeweka mikakati ya kuendeleza miundombinu ya utafiti na huduma mbalimbali za ofisi, watumishi na mifugo.
Miundombinu hii ni pamoja na maabara, miundombinu ya mashamba ya mifugo na utafiti, ofisi, ufafiri, Tehama na kadhalika.
Kuwajengea uwezo watumishi wake ili kuwa na weledi wa kufanya utafiti kwa ufanisi.
Kubuni na kujenga uwezo wa kifedha ili kuweza kuhudumia gharama za utafiti.
Kujenga na kutathmini mifumo bora na endelevu ya kubaini mahitaji mbalimbali ya wafugaji na wadau wengineo yanayohitaji majibu ya kitafiti.
Kujenga na kutathmini mifumo bora na endelevu ya usambazaji wa matokeo ya utafiti kwa walengwa.
Kuongeza ufanisi wa usambazajji wa mifugo bora, malisho na mbegu za malisho zilizokwishafanyiwa tafiti kwa wafugaji.
Taasisi hiyo inakusudia kujenga uwezo wa vituo vyake, ikijumuisha kituo kikuu cha Mpwapwa, ili kuongeza uwezo na ufanisi wa kufanya na kusambaza matokeo ya utafiti kwa walengwa.
Hata hivyo, MaendeleoVijijini inatambua kwamba, bajeti ndogo ya Kilimo na Mifugo imekuwa ikileta changamoto kubwa katika utekelezaji wa mikakati hiyo, hivyo ni vyema serikali ikawekeza zaidi kwenye tafiti ili kuifanya sekta ya kilimo na mifugo isonge mbele.

Comments