Featured Post

SUGU ALIPOHAMASISHA 'OPERESHENI PIGA MAWE MAFISADI' AKASEMA: UKIMUONA LOWASSA FISADI - PIGA MAWE



Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
IJUMAA Mei 6, 2011 Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Osmund Mbilinyi a.k.a Sugu, alitoa kauli yenye kuhamasisha vurugu na machafuko wakati alipoanzisha ‘Operesheni Piga Mawe Mafisadi’, huku akiwataka wafuasi wa Chadema kumpiga mawe Edward Lowassa kwa kuwa ni miongoni mwa mafisadi hao, MaendeleoVijijini inaripoti.
Kauli hiyo ambayo Sugu aliitoa mbele ya maelfu ya wananchi na viongozi wakuu wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa wakati huo, Dk. Wilbrod Slaa, katika viwanja vya Kibonde Nyasi, maarufu kama CCM Ilomba, jijini Mbeya.

Akitumia muda wa dakika 7 na sekunde 39, Sugu aliwataka wafuasi wa Chadema na wananchi kuwapiga mawe viongozi wote wa CCM na Serikali ambao walitajwa kwenye ufisadi, huku akisema zama za vijana maskini kuuana wenyewe kwa wenyewe kwa kuibiana simu na cheni zimekwisha na sasa ilikuwa zamu ya kuwapiga mawe viongozi wote waliotajwa kuwa mafisadi ambao ndiyo sababu ya hali ngumu ya maisha.
Tayari Lowassa, ambaye aliitwa fisadi na kuhubiriwa nchi nzima na viongozi wote wa Chadema kwa miaka takriban saba, yupo na chama hicho na katika hatua ya kushangaza, ndiye waliyemteua kuwa mgombea urais wa chama pamoja na mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mwaka 2015.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, hakuna kiongozi yeyote wa Chadema aliyewahi kuthubutu kutengua kauli hiyo ya Sugu ambayo ilionyesha mtazamo hasi kisiasa na kijamii kwa kuwa ingeweza kuleta vurugu na machafuko na hivyo kuchafua amani nchini.
MaendeleoVijijini inakuletea neno kwa neno la hotuba hiyo ya Sugu, ambaye alikaribishwa na Benson Kigaila aliyekuwa muongoza shughuli (MC):



Salaam
OOYOO... Mizuka! Mizuka! Ndo mambo ya Chadema hayo. Mimi msela leo Mbunge siyo. Nipe wepa! Usipime! Usipime!
Leo hii sitakuwa na maneno mengi kama mnavyonijua mwanenu, nikisimama saa moja, moja na nusu tunachama nondo, na hii ni experience toka majukwaa ya Hip Hop.

Kushinda kesi
Tunasimama sana na nawapa hongera sana kwa sababu kesi waliyotufungulia CCM na Shitambala kupinga ushindi imetupiliwa mbali na Jaji wa Mahakama Kuu.
Hapa sasa wanangu tunasubiri hela ya fidia kutoka kwa CCM kwa sababu hatujafanya party toka tushinde siyo.
Kwa hiyo sasa tunasubiri hela ya fidia kutoka kwa CCM kwa sababu Makamba ndo aliwaambia wafungue zile kesi na sasa Makamba hayupo kwenye game hivyo tutaenda kuchukua mashamba yao waliyosema wanayo tufanye party tulewe siyo.

Shitambala kuondoka Chadema
Kitu cha pili napenda niwapongeze kuondoka Shitambala ndani ya Chadema. Tumelitua zigo la mavi ndugu zangu tumelitua... Niko Dodoma nawawakilisheni kwa mujibu wa mlivonituma. Wakati wa mapumziko nilikuwa nasoma gazeti Shitambala anasema katumia hela nyingi sana kuijenga Chadema Mbeya.
Katumia milioni 200 kwa ushindi wa mimi na Silinde. Siye hatujatumia hela, miye haijafika hata milioni 10 uchaguzi wangu, aache fiksi siyo.
Na zaidi yeye ndo alikuwa anapiga mzinga kwangu mimi siyo. Kila siku anapiga simu ooh eeh bwana kamanda una laki mbili hapo tuje tuongee kwa sababu kesho mkutano, nitakuwa sifanyi mkutano.
Nikamcheki nikaona huyu fiksi kwa sababu alichakachua uchaguzi uliopita, anataka achakachue na huu, na akachakachua kweli kwa sababu masela tuna machale siyo.
Matokeo yake ndugu yangu Shitambala ameenda kulivaa gamba ambalo wenzake wamelivua, ni lazima limuozee hilo hilo gamba siyo. Kwa sababu kuvua gamba nako siyo dili, tatizo la nyoka siyo gamba bali tatizo ni sumu iliyomo ndani yake.
Tutawanyonya damu yenye sumu na kuwakata ndimi zenye sumu, tutawatoa miba na kila kitu wakati tunaendelea kulisongesha kuelekea mwaka 2015 kwa kishindo zaidi.
CCM waache fiksi, wache kamba wanaanza wanatajana ooh fulani fisadi, sijui tunataka kusafisha, lakini ninashukuru kwamba wao wenyewe wamekiri kuwa ndani ya CCM kuna mafisadi na wametuwekea majina na majina hayo ni kanjanja kwani tunajua wako zaidi ya waliotajwa.

Mafisadi na shaka ya Urais wa Prof. Mwandosya 2015
Tunajua Ridhiwan Kikwete ni kamba mwizi, Rostam Aziz mwizi, tunajua Lowassa mwizi, Januari Makamba mwizi na ndiyo maana nachelea kuelewa usomi wa Prof. Mark Mwandosya.
Kwa sababu anataka kututumia sisi kuwapotosha watu. Wewe Prof. Mark Mwandosya na usomi wako wote huo unashindwa kujua kuwa CCM inakufa mpaka unajiandaa kuwa Rais kupitia CCM?
Ameshindwa kwa usomi wake wote kuelewa kwamba CCM inakufa na hapa ndipo ninapochelea kuona hawa wasomi sijui maprofesa, madaktari sijui manani wanakuja wanaacha taaluma na vyuo, wanafunzi wanaandamana wao wapo tu kuchakachua tu kwenye siasa.
Kule kwao anasema zimetumika milioni 700 mradi wa maji wakati zimetumika milioni 35 halafu anabaki anasema “Mimi ndiyo Rais nitakayewakilisha Nyanda za Juu Kusini”. Hakuna kitu kama hicho Mwandosya.
Mwandosya siyo tena mtoto wa dhahabu wa Mbeya. Watoto wa dhahabu mkoani Mbeya tupo hao, wawili mimi Sugu na mwanangu Silinde pale tumefunga. Wengine watoto wa dhahabu kutoka Mbeya tutawaletea mwaka 2015 jimbo la Rungwe Mashariki, Magharibi, Chunya na majimbo yote tisa yaliyobaki ili tuendelee kuisukuma Mbeya yetu jamani.

Opereshini Piga Mawe
Ndugu zangu, sisi hatudanganyiki tena. Ndugu zangu, mimi nasema hivi, najua masela wangu wa Sido mko hapa kwa wingi sana wa Uyole mpo hapa kwa wingi sana, nasema hivi tumechoka. Imefikia mwisho kuuana wenyewe kwa wenyewe. Tunaibiana simu, cheni tunapigana kibiriti, tunakufa bila kuangalia ni sababu gani vijana wanajiingiza wizi wa simu.
Ni kwa sababu ya maisha magumu waliyonayo toka kwa mafisadi ndiyo maana tunaishia kuwa wezi. Hawatupi elimu, sasa mimi nasema hivi, sisi tupo wengi wao wapo wachache.
Kuanzia leo ndani ya Jiji la Mbeya na nchi nzima natangaza ‘Operesheni Piga Mawe’. Tusipigane mawe tena sisi kwa sisi maskini tunauana wakati tatizo tunalijua. Akipita Ridhiwan Kikwete fisadi, piga mawe!… Akipita Lawassa fisadi, piga mawe!… Akipita Januari Makamba fisadi, piga mawe!
Na hii si wao tu, bali na wote wanaowasaidia. Kwa sababu siku zote tunasema anayemsaidia gaidi naye ni gaidi. Kwa hiyo hii ni kwa wasanii wote wanaoisaidia CCM, piga mawe na kutoingia kwenye shoo zao wanapokuja kwenye maeneo yetu.
Nyosha mikono ili tukubaliane kwa pamoja siyo na tunakokwenda. Hata vyombo vya habari vinavyotumika kama jukwaa la CCM navyo tunavipiga mawe kwa namna ya kutovisikiliza….piga mawe, piga mawe, piga mawe!! - MWISHO WA HOTUBA YAKE.


OPERESHENI GIANT NDOSYA NA TWANGA KOTEKOTE
Mbali ya ‘Operesheni Piga Mawe’, lakini Sugu na makada wengine wa Chadema mkoani Mbeya walianzisha operesheni ya ‘Giant Ndosya’ kwa dhamira kuu ya kumpinga Profesa Mwandosya na kuhakikisha harudi tena jimboni mwaka 2015 huku wakiendelea na ‘Operesheni ya Twanga Kotekote’.
Sugu alimtaka Profesa Mwandosya kutumia muda wake wa uongozi uliosalia kwa ajili ya kujiandaa na kustaafu kwa kuwa ndoto zake za kutaka urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haziwezi kutimia huku akisema ni vigumu tena kwake kuendelea kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki.
Sugu aliyasema hayo wakati akihutubia wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa ‘Chadema Twanga Kotekote’ ulofanyika katika Kijiji cha Kandete, eneo la Mwakaleli, Jimbo la Rungwe Mashariki ambalo lilikuwa linashikiliwa na Prof. Mwandosya.
Mkutano huo ulikuwa moja ya mikutano mingi iliyoendelea kufanyika katika jimbo hilo, ikiwa na jina la ‘Operesheni Giant Ndosya’, kama maanndalizi ya kumng’oa Prof. Mwandosya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Sugu alisema Prof. Mwandosya hajalitendea haki jimbo lake kwa kuwa wananchi hao wamempa ridhaa ya kuwaongoza kwa zaidi ya miaka 15, tena akiwa na wadhifa mkubwa serikalini, lakini kwa muda wote huo ameshindwa kuwajengea wananchi wake barabara kuanzia Katumba hadi Mwakaleli yenye urefu wa kilometa 30 tu.
“Hata kama Prof. Mwandosya akichaguliwa kuwa rais hatawakumbuka wananchi wa Rungwe na badala yake atafanyia sherehe za kujipongeza Dar es Salaam, kwa kuwa huku kwao hakuna barabara alizojenga anazoweza kupitisha magari ya Ikulu,” alisema Sugu.
Aidha, Sugu alisema anamshangaa Prof. Mandosya kutotumia elimu kubwa aliyonayo kusoma alama za nyakati na kuendeleza fikra za kutaka urais akiwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho Sugu alidai kuwa kulikuwa na kila dalili kwamba kufikia mwaka 2015 chama hicho kisingeweza kuwepo.
“Nawaomba siku akija hapa mpeni ujumbe huu kuwa ajiandae kustaafu kwa kuwa hakuna urais wala ubunge tena kwake, namshauri arudi kufundisha darasani kwa kuwa hilo ndilo bado tunalihitaji kutoka kwake,” alisema Sugu huku akishangiliwa.






Comments