Featured Post

MAKONDA MGENI RASMI SIKU YA WANAWAKE DUNIANI


Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Mkuu wa Mkoa wa Dar  es Salaam, Paul Makonda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika Machi 8 Mwaka huu, katika uwanja wa Mwembeyanga Temeke Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa  iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam jana  maadhimisho hayo yataongozwa na maandamano ya Wanawake na wadau mbalimbali, na  yataanzia katika Shule ya Msingi Mabatini kuelekea viwanja vya Mwembeyanga.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mwaka huu yanaongozwa na  kauli mbiu isemayo “Tanzania ya viwanda, Wanawake ndio Msingi wa Mabadiliko ya Kiuchumi”.

Kauli mbiu hiyo inalenga kuikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa kujenga mazingira wezeshi kwa Wanawake  hasa kutambua mchango wao  katika kuleta Maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla.

Taarifa hiyo pia imeikumbusha jamii kuhusu wajibu wake ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha, kuwaamini na kuwapa Wanawake haki sawa katika nafasi za Elimu, Uchumi na uongozi ili wawe chachu ya mabadiliko yenye lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya kazi za ujasiriamali yanayoendelea katika uwanja wa Mwembeyanga, ambapo Asasi za kiraia na  vikundi mbalimbali vya wanawake vitaonesha bidhaa zao.

Aidha, Wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam  wanakumbushwa kushiriki  kwa wingi katika maadhimisho hayo ikiwa ni pamoja na kuwa na mikakati ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinanazowakabili Wanawake kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa.

Comments