KWA MTINDO HUU, CHADEMA ITAWAZOA WENGI, SIYO WEMA SEPETU PEKE YAKE!
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
FEBRUARI 23, 2017 msanii wa runinga Wema Isaack Sepetu aliamua kufanya kile ambacho wengi waliojeruhiwa wamekuwa wakikifanya kwa hasira. Alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wema, ambaye ni Miss Tanzania wa mwaka 2006, alichukua uamuzi huo siku hiyo baada ya ‘kumsindikiza’ Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwenye Mahakama Kuu alikokwenda kuwasilisha kesi ya kikatiba Namba 1 ya mwaka 2017 akiitaka mahakama hiyo itoe amri ya kuwazuia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, na Mkuu wa Makachero wa kanda hiyo, ZCO Camillius Wambura, wasimkamate kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.

Lakini hata kabla ya kwenda mahakamani, tayari uamuzi wa Wema kujiunga na Chadema ulikuwa umekwishafanyika, kwani ilielezwa mapema tu kwamba, baada ya kuwasilishwa kwa kesi hiyo mahakamani, uongozi wa chama ungetangaza ama kuwakaribisha wanachama wapya waliojiunga siku hiyo, akiwemo msanii huyo.
Uamuzi wa Wema ‘kutafuta hifadhi ya kisiasa’ ndani ya Chadema ulifuatia kukamatwa kwake na kushtakiwa yeye na wenzake wawili, mfanyakazi wake wa ndani Angelina Msigwa (21) na mkulima Matrida Abas (16), baada ya kukutwa na kete ya bangi nyumbani kwake katika operesheni kabambe iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda.
Hata alipokamatwa na kuwekwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Kati, Wema aliona ‘ameonewa’ na akiwa mahabusu anadaiwa kuropoka maneno mengi akiilaani serikali kwa nini imemkamata.
Baada ya kusota mahabusu kwa siku kadhaa, hatimaye akafikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba, kufanikiwa kupata dhamana wakati akiwakilishwa na Wakili Msomi Albert Msando na wanatetewa na mawakili Albert Msando na Nictagon Itege.
Haikushangaza siku kesi yake ilipotajwa kwa mara ya pili Februari 22, 2017 kuona akiwakilishwa pia na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki. Kesi hiyo itatajwa tena Jumatano hii Machi 15.
Wema Sepetu, au yeyote yule, anayo haki ya kuchagua kuiunga na umoja ama chama chochote kwa sababu ni haki yake ya Kikatiba.
Hata hivyo, alichokifanya Wema pamoja na wengine ni uamuzi hasira ama kutaka kupata hifadhi ya kisiasa kwa kuamini kwamba ‘wameonewa’ hata kama wamefanya makosa.
Wema, inawezekana na wengine wote ‘wenye majina’, aliamini kwamba kwa umaarufu alionao, basi ana kinga (immunity) ya kutokamatwa na yeyote, achilia mbali kuwekwa mahabusu kwa siku kadhaa na kushtakiwa.
Msanii huyo aliamini kwamba, kwa kuwa alikuwa mstari wa mbele kukiunga mkono chama tawala, CCM, kiasi cha kugombea ubunge wa viti maalum huko mkoani kwao Singida, ikiwa ni pamoja na kuzunguka na wasanii wenzake nchi nzima wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015, basi hakuna ambaye anaweza kumgusa hata kama atakuwa amefanya hatia.
Ndiyo maana baada ya kujiunga na Chadema alikaririwa akisema kwamba, kama asingejiunga na chama hicho alitamani kutoroka nchi akaishi kwingine, sijui wapi!
Jambo ambalo amelisahau ni kwamba, linapokuja suala la kisheria hakuna mtu ambaye anaweza kuwa salama.
Kosa kubwa ambalo amelifanya Wema na yeyote  ambaye ameamua kuvuka upande wa pili ni kuifanya operesheni ya dawa za kulevya kuwa ya kisiasa, na mbaya zaidi Lissu naye ameamua kuvaa joho la utetezi siyo kwa sababu ya kwamba Wema anayo haki hiyo tu, bali anataka kulifanya suala hilo kama la kisiasa.
Wengi wameunga mkono uamuzi wa Wema kukimbilia Chadema, wakisema kwamba huko ‘ndiko nyumbani kwao’ na hakupaswa kuwa CCM.
Wanashindwa kutambua kwamba, jinai haichagui mtu wala ni kikundi gani ambacho mtu huyo amejiunga nacho, na zaidi wanaamini kwama operesheni ya dawa za kulevya imechukuliwa kisiasa, jambo ambalo siyo kweli.
Wengine wanaona Wema kujiunga na Chadema ni turufu kubwa kwa chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania Bara, kwamba anaweza kutumika kuushambulia upande wa pili na wao wakajiongezea umaarufu kwa umaarufu wa msanii huyo.
Wema si mwanaCCM peke yake aliyekumbwa na sakata hilo, kwani wapo wengi, wakiwemo viongozi wa kuchaguliwa na wananchi ambao wamepata misukosuko hiyo kutokana na kashfa za dawa za kulevya.
Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, Yussuf Mehboob Manji, ni miongoni mwa washtakiwa kwa sasa na alikaa mahabusu kwa siku sita mfululizo bila kuliona jua.
Vigogo wengine wengi, wakiwemo makada wa CCM nao ni miongoni mwa watu walio kwenye orodha ya watuhumiwa 65 wa dawa za kulevya.
Aidha, wasanii wenzake kama ‘video queen’ Agnes Gerald ‘Masogange’, Naseeb Abdul ‘Diamond Platinumz’ ambaye walikuwa wote kwenye mzunguko wa kampeni za Chama cha Mapinduzi, nao wamekwishafikishwa polisi na kuhojiwa.
Masogange (28), ambaye naye alikaa mahabusu kwa siku nane, alikwishafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Februari 22, 2017 mbele ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri akikabiliwa na mashtaka mawili ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin diacety na oxazepam. Kesi yake itatajwa tena Machi 21, 2017.
Ninachoweza kusema ni kwamba, serikali huwa haikurupuki kufanya mambo yake kama baadhi ya watu wanavyoaminishwa na wanasiasa, tena Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa weledi mkubwa na kamwe maofisa wake hawawezi kwenda kumkamata mtu bila hatia ama pasipo kujiridhisha.
Ni masogange huyo huyo na mwenzake Melissa Edward (27) ambao Ijumaa ya Julai 5, 2013 walikamatwa kwenye uwanja wa ndege wa Oliver Tambo, Johannesburg nchini Afrika Kusini wakiwa na shehena ya dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya zaidi ya Shs. 6.8 bilioni wakitokea Tanzania.
Tukio hilo lilitokea takriban wiki moja tu baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Juni 28, 2013 kutangaza kuwa tatizo la dawa za kulenya ni janga la kitaifa.
Hata hivyo, Masogange na mwenzake waliachiliwa huru Septemba 19, 2013 na Mahakama ya Kempton ya jijini Johannesburg, baada ya kulipa faini ya R30,000 (Sh4.8 milioni) kwa kosa la kubeba kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya.
Uamuzi wa Wema kujiunga na Chadema kama ni wa kulazimishwa kutokana na mazingira yaliyopo ya msako wa vigogo wa dawa za kulevya, basi unaweza kuwa ni mwanzo wa watu wengi kukimbilia huko upinzani ikiwa wanaona serikali ya CCM inawaonea.
Binafsi siwezi kushangaa kwa Chadema kuwapokea watuhumiwa wa aina yoyote, kwa sababu ni kawaida yao kuifanya ‘haramu kuwa halali’.
Tumeshuhudia namna viongozi wa chama hicho walipoyalamba matapishi yao kwa kuwazoa watu wote ambao wao wenyewe waliwaita ni ‘mafisadi’, lakini wakawatakasa na kuona ‘malaika wa nuru’.
Tuliona namna walivyomshawishi Edward Lowassa na hatimaye kumakabidhi mikoba ya kugombea urais kupitia Chadema na hatimaye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambayo awali alikuwa ameandaliwa Dk. Wilbrod Slaa, mara tu baada ya waziri mkuu huyo wa zamani kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia CCM.
Ni Lowassa huyo huyo ambaye walimtuhumu kwa ufisadi na wakamwita majina mengi yasiyofaa, lakini baadaye wakamtakasa na kumpamba kwa nyimbo na mapambio kwamba ndiye ‘rais wa mabadiliko’.
Kwa maana hiyo, hata katika kadhia hii ya dawa za kulevya, wala sitashangaa kuona vigogo wengi na makada wa CCM waliotajwa ama kuhusishwa wakikimbilia Chadema, chama ambacho kinaleta tafsiri ya kupokea watuhumiwa wa aina zote na kuwaona wasafi.
Ni dhahiri kwamba, kadhia hii ya dawa za kulevya imewajeruhi wengi, tena wale ambao walikuwa wakionekana maarufu, wema na wakarimu mbele ya uso wa jamii.
Kwa maana hiyo, ili kujitakasa kwamba ‘walionewa tu’ lazima watakimbilia mahali kupata hifadhi. Huu ndio ukweli wenyewe.
0656331974