JENEZA KUTOKA HONG KONG - (SEHEMU YA 16)
Alionekana kufurahia zaidi kuwa mwenyeji wangu, nikamwambia nitakunywa Scotch. Akachukua chupa na glasi mbili kwenye saraka na kumimina kiasi cha kutosha. Akaomba radhi kwa kutokuwa na barafu. Nikamwambia nimezowea kugonga vitu vikali na hiyo haikuwa shida. Tulitaniana na tukagugumia vinywaji vyetu. Ilikuwa ni Scotch nzuri sana.
“Ulichoniambia kuhusu Herman Jefferson kimenivutia sana,” nikamweleza. “Nilikuwa nafikiria kama unaweza kunipatia taarifa zaidi. Ninajaribu tu kupapasa. Jambo lolote linaweza kunisaidia.”

“Kwa nini, hakika nitakupa.” Alinitazama kwa namna mbwa wa Mchungaji anaweza kuonekana mara anaposikia sauti ya fadhaa. “Ulikuwa na mtazamo gani mawazoni mwako?”
Nikampa mtazamo wangu wa mshangao wa kama-ningejua ambao huutumia ninapokutana na watu wa aina ya Jay Wayde.
“Sielewi,” nikamwambia. “Kazi yangu ni kukusanya taarifa sahihi kwa kadiri yoyote kwa matumaini ya kwamba zinaweza kuleta maana. Kwa mfano, kama ulimfahamu Jefferson. Uliniambia jambo fulani kuhusu tabia yake. Uliniambia alikuwa na fujo, mlevi kidogo, alianzisha ugomvi na kusababisha fujo. Alikuwaje wakati alipokuwa na wanawake?”
Uso wa Wayde ghafla ulionyesha matumaini. 
Nilifikiri jinsi alivyokuwa katika suala la wanawake. Hisia zake za mapenzi zingeweza kuzuiwa na rungu la kuchezea golfu.
“Alikuwa anapenda mno wanawake. Sawa, unapokuwa kijana, unaweza kutembea na wasichana — Mimi pia nilikuwa na wasichana, lakini Herman alikuwa ameoza. Kama baba yake asingekuwa na uwezo mkubwa katika jiji hili, kungekuwa na skendo kila siku kumhusu yeye.”
“Kulikuwa na msichana yeyote maalum?” nikamuuliza.
Alisita, kisha akasema, “Sipendi kutaja majina, lakini kulikuwa na huyu msichana, Janet West. Ni katibu muhtasi wa Bwana Jefferson. Ali . . .” Alisita ghafla na macho yake yakaangalia pembeni. “Tazama, samahani, sidhani kama ni sahihi kuzungumzia hili. Hata hivyo, hili lilitokea takriban miaka tisa iliyopita. Najua kwa sababu Herman aliniambia, lakini hilo halinipi haki ya kukueleza.”
Niliona kwamba alikuwa anapenda sana kunieleza: akipenda kushiriki katika kumsaka muuaji na akijiona ni mtu muhimu sana kiasi kwamba mimi nilikuwa na nia ya kusikia kile atakachoniambia.
Hivyo nikamwambia kiujanja, “Kila kipande cha taarifa nitakachopata kinaweza kuniongoza kwa muuaji. Unaweza kujiuliza mwenyewe kama una haki ya kunieleza ama kutonieleza.”
Hili lilimfurahisha sana. Macho yake yakarejewa na nuru na kuinamia mbele, akinitazama usoni.
“Sawa, ni vyema, kwa kuliweka namna hiyo, ninajua unachomaanisha.” Alipapasa nywele zake zilizokatwa vyema na kisha kuonyesha mtazamo wa mtu ambaye hana rekodi za skendo, akasema, “Herman na Janet West walikuwa na uhusiano wa mapenzi takriban miaka tisa iliyopita. Walipata mtoto.  Herman akamkataa na Jane West akamwendea baba yake ambaye alifadhaika sana. Bahati mbaya mtoto alikufa. Yule mzee alisisitiza Herman amuoe binti huyo, lakini Herman akakataa kata kata. Nadhani yule mzee akaamua mwenyewe kumchukua jumla. Akampeleka nyumbani kwake na kumfanya kuwa katibu muhtasi wake. Herman aliniambia kuhusu hili. Alikuwa amekasirika kuona baba yake amemchukua binti huyo na kumpeleka nyumbani kwake. Nahisi mzee alitarajia Herman angeweza kubadili moyo wake na kumuoa, lakini wakati matumaini yalipokufa na kubaini kwamba Herman asingeweza kubadili uamuzi wake, akaamua kufanya mipango ya Herman kwenda Mashariki. Janet amekuwa na mzee tangu wakati huo.”
“Ni mzuri sana,” nikamwambia. “Sielewi kwa nini hajaolewa mpaka sasa.”
“Hainishangazi kabisa. Yule mzee asingependa. Anamtegemea sana yule binti, na zaidi ya yote, hakuna mtu mwingine yeyote atakayemwachia urithi wake wa mamilioni baada ya Herman kufariki.”
“Hakuna yeyote?” Nikajaribu kuficha hamu yangu ya kusikia kipengele hicho. “Anaweza kuwa na ndugu.”
“Hapana. Nilikuwa naifahamu familia ile vizuri sana. Herman aliniambia kwamba ndiye angerithi kwa sababu hakukuwepo na watu wengine. Nina uhakika Janet anaweza kupata urithi, hata sehemu yake tu, mara mzee atakapofariki.”
“Ni bahati yake, mke wa Herman hawezi kuidai.”
Akaonyesha kugutuka.
“Sikuwahi kufikiria kuhusu upande huo. Hana nafasi kubwa. Sidhani kama yule mzee angeweza kumwachia mwanamke wa Kichina chochote.”
“Kama mke halali wa Herman, angeweza kufungua madai. Kama jaji atakuwa na huruma, angeweza kuchukua urithi.”
Mlango wa upande wa kulia ukafunguliwa na msichana  akaingia akiwa na rundo la barua zilizohitaji kusainiwa. Alikuwa ni aina ya wasichana ambao nilitarajia Wayde angewaajiri: mrembo, na mwenye miwani.
Nikasimama wakati alipoweka barua hizo mezani.
“Ngoja niende,” nikasema. “Tutaonana tena.”
“Kuna maendeleo yoyote?” aliuliza baada ya yule binti kuondoka. “Polisi wamegundua chochote?”
“Hakuna chochote walichogundua. Uchunguzi rasmi wa kisheria utafanyika kesho, lakini watalazimika kuleta mashtaka ya mauaji yanayowahusu watu wasiojulikana. Yalikuwa ni mauaji yaliyotumia akili nyingi sana.”
“Nitakwambia.” Akavuta barua mbele yake. “Kama kuna lolote nitakaloweza kulifanya. . .”
“Nitakueleza.”
Niliporudi ofisini kwangu, nikampigia Retnick na kumweleza nini nilichokipata kumhusu Janet West.
“Mpira sasa uko miguuni mwako,” Nikamwambia. “Kama ningekuwa wewe, ningependa kujua ni wapi alikokuwa Bi West majira ya saa tisa alfajiri wakati mwanamke wa Kichina alipouawa.”
Kulikuwa na utulivu wakati nikisikiliza jinsi alivyokuwa akipumua kwa nguvu.
“Lakini sasa wewe siyo mimi,” hatimaye akajibu. “Tutaonana katika uchunguzi. Usisahau kuvaa shati zuri. Ofisa mchunguzi wa vifo ni mwanaharamu,” na akakata simu.
 
Itaendelea kesho...