JENEZA KUTOKA HONG KONG - (SEHEMU YA 15)
“Jina lake ni Jo-An Cheung—ni jina la ajabu sana, au siyo? Miaka mitatu iliyopita alikamatwa akiingia Hong Kong kwa mashua kutoka Macau. Alitumia wiki sita akiwa gerezani na akapewa nyaraka za utambulisho. Alifanya kazi kama mcheza shoo kwenye klabu ya Pagoda na hiyo inamaanisha alikuwa kahaba.” Alilikuna sikio lake, akitazama dirishani kwa muda kabla ya kuendelea. “Alifunga ndoa na Jefferson mbele ya Balozi wa Marekani mnamo Septemba 21 mwaka jana. Waliishi pamoja katika katika hoteli ya Wachina iitwayo Celestial Empire Hotel. Jefferson anaonekana hakuwa na kazi ya kufanya. Alikuwa akitegemea kipato cha mwanamke na kiasi kidogo alichokipata kutoka kwa baba yake. Mnamo Septemba 6 mwaka huu, alikufa kwenye ajali ya gari na mwanamke akaomba kibali kutoka kwa Ubalozi wa Marekani ili ailete maiti yake nyumbani. Hiyo ndiyo habari yenyewe. Kwa nini uende Hong Kong?”
“Nimelipwa ili niende. Hata hivyo, nitakuwa nje ya njia yako, sitakuingilia.”
Akatabasamu kinafiki. “Usijali kuhusu kuingilia upelelezi wangu, mpekenyuzi. Ninaweza kukuondoa kwenye anga zangu wakati wowote.”
Nilimwacha ajisifu. Kuna nyakati ambazo alijiona ni muhimu: huu ulikuwa mmojawapo.
“Sawa, vipi kuhusu maendeleo ya kesi? Umefika popote?”
“Hapana.” Akatazama chini kwenye dawati lake lililoonekana kuchafuliwa na wino muda mrefu. “Kinachonishangaza zaidi ni kwamba kwa nini alikuja ofisini kwake saa tisa alfajiri.”
“Yeah. Pengine nitapata jibu nikienda Hong Kong.” Nilitulia kuwasha sigara yangu, halafu nikaendelea, “Kikongwe Jefferson ana thamani ya fedha nyingi sana. Ninajua mwanaye angeweza kuirithi. Labda kama baba yake angebadili usia, lakini Jo-An ndiye angekuwa mrithi wake sasa baada ya mwanaye kufariki. Yawezekana kuna mtu ameamua kumuua ili asiirithi mali hiyo. Ningependa kujua ni nani sasa ambaye atakuwa mrithi wa mali hiyo. Kinaweza kkuwa kichocheo cha mauaji.”
Alitafakari, halafu akasema, “Unajua wakati mwingine unakuwa na mawazo mazuri sana. Yeah: kweli wazo lako linaweza kuwa sahihi.”
“Umewahi kukutana na katibu muhtasi wake: Janet West? Haitaweza kunishangaza kama hataweza kuchukua sehemu ya fedha za Jefferson atakapokufa. Ninadhani, wakati fulani, aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaye. Litakuwa ni wazo jema kuchunguza alikuwa wappi majjira ya saa tisa alasiri wakati mwanamke wa Kichina alipouawa.”
“Utafanyaje hilo?” Retnick akauliza. “Nimekutana naye. Yule mzee anamuamini sana. Kama nitaanza kuchimba kuhusu maisha yake binafsi, ninaweza kuingia matatizoni na hilo ni jambo ambalo huwa silifanya. Yule mzee anaweza kuleta matatizo makubwa kwenye mji huu.”
Retnick akanitazama kwa makini. “Nini kinachokufanya uamini alikuwa na uhisiano wa kimapenzi na mwanaye?”
“Nimetoka kuzungumza naye. Ana uwezo mzuri wa kujidhibiti, lakini ulimponyoka kidogo. Siwezi kusema ndiye aliyemuua mwanamke wa Kichina, lakini pengine anajua zaidi kuhusiana na mauaji hayo kuliko anavyojifanya. Inawezekana anaye mpenzi mwenye tamaa.”
“Siwezi kumfukuza yule mbuzi,” alisema Retnick. “Ninachotaka kukichunguza ni kwa nini yule mtu wa manjano alikuja ofisini kwao. Mara nitakapopata ukweli, kesi imekwisha.”
Nikasimama.
“Unaweza kuwa sahihi. Lini wanaifanyia uchunguzi maiti na kuaga kwa ajili ya mazishi? Ningependa kuondoka mapema iwezekanavyo.”
“Kesho saa nne asubuhi. Haiwezi kuwa na maana yoyote, lakini unatakiwa uwepo.” Akaigonga peni yake kwenye dawati. “Usisahau, kama utagundua jambo lolote, nahitaji kufahamu.”
“Huwezi kufanya jambo lolote kutokana na mshahara unaopata?”
Akakunja ndita zake.
“Nani anayeita mshahara? Ninatakiwa kuchunga nyendo zangu. Jefferson anaweza. . .”
“Najua. . . ulikwishaniambia.”
Nikamuacha akiendelea kuigonga peni yake kwenye dawati na kutengeneza vitundu vidogo. Muuaji wa Jo-An Jefferson angeweza kupenda kumuona alivyo sasa. Muonekano wake ungeweza kumpa nguvu kubwa za kujiamini.
Nikarejea ofisini kwangu. Wakati nilipotaka kufungua mlango wangu, wazo likanijia. Nilitembea hatua chache kwenye korido na kugonga kwenye mlango wa Jay Wayde, na kuufungua.
Nikaingia kwenye ofisini kubwa, iliyopambwa vizuri, huku meza ikiwa inatazama mlangoni ambapo juu yake kulikuwa na mashine ya kurekodia (tape recorder), simu, mashine ndogo ya kupigia chapa na trei mbili za chuma moja ikiwa imeandikwa ‘In’ na nyingine ‘Out’ kwa ajili ya kuwekea nyaraka na mafaili mbalimbali ambayo yalihitaji kufanyiwa kazi ama tayari yalikwishafanyiwa kazi.
Wayde aliketi nyuma ya dawati, akivuta mtemba, peni ikiwa mkononi, karatasi zikiwa mbele yake.
Kulikuwa na mlango mwingine upande wake wa kulia. Kupitia huko vilisikika vishindo vya mamshine ya kupiga chapa.
Ofisi yake ilikuwa na mazingira bora zaidi kuliko ya kwangu, lakini kuwa mkemia wa viwanda ilikuwa ni kazi yenye maslahi makubwa kuliko kuwa mpelelezi wa kujitegemea.
“Hello habari gani,” Wayde alisema, akionyesha kufurahi kuniona. Akainuka kidogo, akiniashiria niketi kwenye kiti maridadi pembeni ya dawati lake. “Karibu ndani na uketi.”
Niliingia ndani na kuketi.
“Ujio huu si wa kutarajiwa.” Aliitazama saa yake ya dhahabu aina ya Omega. “vipi utakunywa nini? Inakaribia saa kumi na mbili. Utakunywa Scotch?”

Itaendelea kesho...