HUYU HAPA NDIYE SOPHIA NYAMBI MATHEW SIMBA ALIYETIMULIWA CCM!MNAMO Mei 2012, gazeti la Rai Mwema lilichapisha mahojiano maalum na Sophia Simba ambayo yalikuwa na kichwa cha habari ‘Si kweli kwamba sipendwi na wanaume – Sophia Simba’.
MaendeleoVijijini inakuletea moja kwa moja mahojiano hayo hapa, ili kuweza kumfahamu mwanamama huyo ambaye Jumamosi Machi 11, 2017 ilikuwa siku mbaya kwake baada ya kutimuliwa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa makosa ya kinidhamu.

Wakati mahojiano hayo yakifanyika, Sophia alikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora – ndiyo inayoshughulikia pia masuala nyeti ya nchi), na pia alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Endelea na mahojiano hayo, ambapo pamoja na mambo mengine, alizungumzia masuala ya uhusiano wake wa kimapenzi…
Raia Mwema: Wasomaji wetu wangependa kukufahamu kwa sababu mengi yamekuwa yakisemwa na  yakinong’onwa hususan kuhusu elimu yako; labda kwa vile hawaifahamu vizuri. Unaweza kutupa CV yako kwa kifupi?
Mama Sophia Simba: Asante kwa kunipa nafasi hii adimu. Nimefurahi kwamba  umeweza kufika ofisini kwangu na kuweza kuongea na mimi. Nashukuru kwamba umeona upo umuhimu wa watu kunijua mimi Sophia ni nani hasa.
Ni kweli maneno mengi yamekuwa yakisemwa ambayo hayapendezi, lakini nitafanyaje?  Kwa hiyo, kwa kifupi sana ningependa nikufahamishe  labda pengine kwa kupitia wewe watu watanifahamu.
Mimi naitwa Sophia Simba. Ni Sophia Mathew Simba. Nyambi ni jina langu la nyumbani. Wazaramo wana majina yao ya ukoo, kwa hiyo mimi ni Nyambi na mdogo wangu alipewa jina lingine. Nilipokuwa mdogo baba yangu akasema huyu ni Nyambi.
Kwa kifupi sana, mimi ni mtoto wa mfanyabiashara. Baba yangu alitokea Kisarawe, kijiji kinachoitwa Sungwi. Baba yangu alisoma Minaki. Alipomaliza Minaki alirudi hapa Dar es salaam. Baba yangu aliwahi kufanya kazi mpaka ya uvuvi.  Aliacha shule kutokana na umbali kutoka kijijini kwake Sungwi kwenda Minaki.
Watoto waliokuwa wakitoka bara walikuwa wanasoma boarding, lakini watoto wa Kisarawe wenyewe walikuwa wanatakiwa watembee umbali mrefu. Kwa hiyo, kutokana na hiyo alifikia mahali  haikuwezekana.
Baba yangu mwanzoni  alikuwa Mwislamu. Alikuwa anaitwa Omari Simba. Kutokana na kusoma pale Minaki, aliamua kubadilisha dini. Baba yangu alibatizwa katika Kanisa la St. Albans –  hili la hapa mjini. Na baada ya hapo baba yangu aliondoka akaenda Morogoro kufanya shughuli za biashara.
Kule alikutana na mama yangu, mwanamke wa Kiluguru ambaye naye historia yake alikuwa Sister wa Roman Catholic. Kwa hiyo walikutana na wakaoana.
Katika maisha yetu yote tumeishi kama Wakristu wa Roman Catholic. Mpaka leo mimi ni Mroman Catholic ingawaje kila mtu ananipa dini ambayo anaitaka. Kwa hiyo, mimi ni mmoja wa watoto tisa. Mimi ni wa pili.
Raia Mwema: Makazi yenu hasa yalikuwa wapi?
Mama Sophia Simba: Makazi yetu yalikuwa Dar es salaam na Morogoro. Dar es Salaam tuliishi Bungoni, Ilala. Lakini tukiwa wadogo kabisa baba yangu alijenga nyumba yake ya kwanza kabisa Morogoro, Kwa Kingu.
Alifanikiwa sana kwa shughuli za baa. Mimi ni mtoto ambaye nimesomeshwa kwa pesa za pombe. Baba yangu alikuwa na baa inayoitwa Uzaramo Bar, Morogoro lakini pia alikuwa na baa inayoitwa Simba Bar. Kwa hiyo, mimi kufungua vizibo vya bia najua.
Nikiwa bado mdogo nilikuwa nauza mishikaki. Siku zote nyumba yetu ilikuwa upande baa, upande tunaishi sisi. Kwa hiyo, baba yangu aliendelea na shughuli za baa muda mrefu.
Raia Mwema: Ulianza shule wapi?
Mama Sophia Simba: Mimi nilianza shule  Morogoro katika shule inayoitwa Kilakala,  baada ya hapo nikapelekwa shule ya boarding inayoitwa Ilonga Middle School, Kilosa. Baada ya hapo nikasoma Forest Hill Secondary School. Sisi ndiyo waanzilishi wake.
Ule mwaka ambao wanafunzi wengi tuliambiwa hatukuchaguliwa  tuliunganishwa darasa la saba na la nane. Kwa hiyo sisi tulimalizia darasa la nane. Huo ulikuwa mwaka 1965.  Shule nyingi (za binafsi) zilianzishwa mwaka huo. Shule za Kibohehe, Forest Hill, Mzizima na Kinondoni, zote zilianza wakati huo.
Baada ya pale nikaenda Kibosho Secondary School. Kwa bahati mbaya baba akafariki, wakati huo nikiwa nafanya kazi NDC. Kabla hajafariki, baba alitaka sana nifanye shughuli za biashara, niendeleze biashara ya familia.
Baada ya kumaliza shule nilichaguliwa nikasomee ualimu lakini sikwenda,  na badala yake nikapata kazi NDC. Hapo NDC nilianza kazi 1971 hadi mwaka 1979.
Baada ya hapo nikaingia Lonrho Group of Companies baada ya kuacha kazi NDC. Kutoka pale nikaanza kazi Metal Engineering Industries Development Association (MEIDA) ambayo ilianzishwa na Waswedish. Nikiwa hapo nikaamua kwenda kusoma. Nilianza mafunzo ya Certificate of law mwaka 1985. Nilipenda sana kusomea sheria.
Mwaka 1987 nilianza kusomea shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na nikahitimu mwaka 1992 au 1993. Kuna mwaka hapo katikati chuo kilifungwa kwa sababu ya kuwapo mgomo.
Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu nikarudi kufanya kazi Metal Industries; kwani wakati nasoma walikuwa wamenipatia likizo isiyokuwa na malipo. Baada ya kurudi walinipandisha cheo kuwa legal and administrative officer; kwani kabla ya kwenda chuo kikuu cheo changu kilikuwa administrative officer tu.
Wakati niko NDC nilikuwa katibu wa tawi la UWT la NDC na Mama Anna Mkapa alikuwa mwenyekiti wetu, tulifanya mambo mengi mazuri.
Nilipokuwa MEIDA niliomba pia kuwa diwani wa viti maalumu. Kulikuwa na uchaguzi mwaka 1993 au 1994. Nikawa diwani hadi 1995. Mwaka 1995 wakasema kuna viti maalumu vya ubunge kwa akina mama. Mimi nikagombea vitu maalumu.
Mwaka huo wa 1995 nilipata invitation ya kwenda Beijing, China kuhudhuria mkutano wa wanawake duniani. Nikakataa, nikampa mwenzangu nikamwambia mimi siendi nitabaki hapa kwa ajili ya kampeni za ubunge. Sikwenda mimi Beijing kwa sababu ya kampeni hiyo. Kwa hiyo mwaka 1995
Nikashinda, na hivyo nikaingia bungeni.
Mwaka 1995 nilifanya mafunzo ya Post Graduate Diploma on Women Law kwenye Chuo Kikuu cha Zimbabwe na mwaka  2005 nilifanya Masters ya Community Economic kwenye Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Thesis yangu  ilikuwa Women  and Economic Empowerment in Tanzania.
Mwaka 1972 mimi niliolewa. Mume wangu alikuwa ni mwanasheria wa Chama cha Ukombozi cha Afrika Kusini cha ANC. Siku zile walikuwa wakiwaita wakimbizi, lakini wenyewe walikuwa wanataka waitwe freedom fighters.
Mume wangu aliruhusiwa pia kufanya kazi za uanasheria nchini. Kabla ya kufariki aliwahi kufanya kazi pia benki. Alikuwa anaitwa Clifford Zex Senge. Wengi walikuwa wanamwita kwa jina la Cliff. Wanasheria wengi wanamjua.
Kwa hiyo, niliolewa na Cliff na nikazaa naye watoto wawili. Watoto hao walikwenda Afrika Kusini kwa baba yao lakini sasa wote wamerudi. Maisha ya Afrika Kusini ni magumu hayako that easy.
Kuna watu wanasema mimi ni kituo cha polisi, wanaume wananikimbia. Nilisoma kwenye gazeti (eti) wanaume hawanitaki. Lakini I was married.
Raia Mwema: Uliolewa na Msouth Afrika na kwa bahati mbaya akafariki dunia. Lakini nasikia ulikuwa na mahusiano na ulionekana mwaka 1995 ukiwa na Kitwana Kondo, Meya wa zamani wa Dar es Salaam na mbunge wa zamani wa Ilala. Uhusiano wako na yeye ulikuwa wa aina gani?
Mama Sophia Simba: Sawa, mimi nilikutana na Mzee Kondo… Kwanza nakubali nilikuwa na mahusiano naye, na nimezaa naye mtoto wa kiume. Nilikuwa na Mzee Kondo kutoka mwaka 1975. Nilikutana naye wakati akigombea ubunge; mimi nikiwa kama mpiga debe wake. Kwa hiyo tulikutana mwaka 1975 na tukaachana mwaka 1983.
Siyo kama tulioana, hapana, alikuwa boyfriend. Yeye siku zote amekuwa na mke wake. Kwa hiyo, nilizaa naye kweli mtoto mmoja na mpaka sasa hivi mimi namuheshimu Mzee Kondo. Na baada ya hapo, mwaka 1983, ameshaoa mara mbili au mara tatu lakini mimi bado namheshimu mpaka watu hawaelewi mahusiano yangu mimi na yeye yakoje.
Hata tulipokwenda bungeni watu wengine walidhania ni mtu na mkewe, lakini mimi sijaolewa na Kitwana Kondo. Namheshimu sana, ni baba wa mtoto wangu.
Raia Mwema: Sasa tuje kwenye nafasi  yako ya uenyekiti wa UWT. Wewe katika miaka yako hii mitano unataka UWT iwe ya namna gani baada ya kuvaa kofia iliyovaliwa na wanawake wazito huko nyuma kama Bibi Titi Mohammed, Sophia Kawawa na Anna Abdallah?
Mama Sophia Simba: Asante kwa swali hilo. Kwanza nishukuru walionitangulia kwamba wamefanya kazi kubwa. Wao ni role models ambao tulikuwa tukiwatizama na sisi kufanya kazi chini yao.
Nikiri kwamba nimefanya kazi chini ya Mama Sophia. Alipokuwa mwenyekiti, mimi nilikuwa katibu wa tawi. Mama Abdallah  alipokuwa mwenyekiti wa taifa, mimi nilikuwa mwenyekiti wa UWT tawi la kata ya Upanga Magharibi. Kwa hiyo, hawa wote wamekuwa viongozi wangu na nimewaona walivyokuwa wakifanya kazi.
Mimi katika kipindi hiki cha miaka mitano nitaendeleza yale yote ambayo nimejifunza kutoka kwao, lakini pamoja na hivyo; mambo yamebadilika. Itabidi na sisi UWT tubadilike.
Ukumbuke kwamba hapo nyuma mimi nilipoinga UWT nilikuwa mfanyakazi. Sasa hivi baada ya matawi ya kazini ya chama kuvunjwa, kumekuwa na gap hapo.  Wafanyakazi wengi  wapo wapo tu. Wanawake wengi hawapo katika chama, hawapo katika jumuiya, wapowapo tu.
Wapenzi wengi wa CCM wako kama vile wa Simba na Yanga – hawana kadi, hawana nini. Kwa hiyo, mimi mkakati wangu mmoja mkubwa ni kuhakikisha nawapata hawa akina mama. Nitawafuata hukohuko waliko katika maeneo yao kuwahamasisha kuinga UWT.
Hadi sasa tunaendelea vizuri. Tuna kitengo kizima kinachoelezea jinsi ya ku-capture na kuwahamasisha akina mama na kuwaambia; na wewe pia unaweza kuwa mwanachama wa UWT, unaweza kuwa mwanachama wa CCM, usikae tu bure hivi hivi.
Kwa kufanya hivyo, UWT itakwenda na wakati. Tunawahitaji hawa young generation twende nao tusiwaache nyuma. UWT isiwe jumuiya ya wazee na watu wazima tu.
UWT iwe ni jumuiya ya wanawake vijana pia, kwa sababu naamini ukishirikiana na vijana kuna mengi ambayo utaweza kujifunza. Tunaweza tukaifanya UWT ikawa hatua moja zaidi kutoka hapa tulipo.
UWT tumejipanga kuanzisha tawi la UWT makao makuu. Na lingine ambalo tumesema tutafanya ni kuifanya UWT isiwe tegemezi kiasi hicho. UWT ina mali zake nyingi ambazo zimekuwa dormant kwa muda mrefu. Kwa hiyo, tunataka tuzitumie ili tuweze kwa kiasi fulani tujitegemee.
Hivi sasa watendaji wote UWT wanategemea ruzuku kutoka CCM.  Kwa hiyo, tunakipa mzigo mkubwa sana Chama cha Mapinduzi. Lazima tuangalie ni jinsi gani tunaweza tukatumia raslimali  tulizokuwa nazo, nadhani tutaipunguzia mzigo CCM.
Kama nilivyosema siku yangu ile ya kwanza, ni lazima twende na wakati.  Nilitumia maneno: ‘UWT iende na dot com.’ Generation ni dot com, tusirudi nyuma.
Raia Mwema: Lakini baadhi ya watu wanasema kwamba labda umeanza na gea ngumu kidogo baada ya Katibu Mkuu wako, Husna Mwilima kuwa amewajibishwa na Baraza Kuu. Huoni kwamba kitendo hicho cha kumwondoa ni hatua ngumu kwako?
Mama Sophia Simba: Kwanza nikiri kwamba si jambo zuri kwamba katibu mkuu wangu imebidi Baraza Kuu limwondoe. Mimi binafsi siyo kitu ambacho nilitarajia, kwa sababu mimi ndiye niliyemtafuta yeye na  jina lake kulipeleka kwenye vikao vya chama ili lipitishwe.        
Kwa hiyo, hiyo imeonyesha kwamba ni udhaifu kwa upande wangu. Nikiri kwamba sikulifanyia kazi vizuri lile jina. Pengine nilikuwa sikujiandaa vizuri. Binadamu kufanya makosa ni kawaida, na pale nilikosea.
Hata hivyo, nilijitahidi sana kufanya naye kazi vizuri. Nimekaa naye kipindi cha mwaka mmoja. Unapopewa madaraka inabidi kwanza ujifunze, kwa hiyo nilijitahidi sana kuhakikisha kwamba katibu mkuu  huyu, ambaye mimi mwenyewe nilimtafuta, aweze ku-cope na ile ofisi.
Lakini kukawa kuna matatizo ya… Kwanza huwezi kumfananisha huyo na akina Thecla Mchauru, Kate Kamba, Dk Msimu ambao kiwango cha elimu yao kidogo ilikuwa zaidi. Hata Halima Mamuya elimu yake iko juu zaidi ya huyu.
Huyu alibebeshwa mzigo ambao hakustahili, tulifanya makosa. Tulimbebesha mzito mkubwa wa kiutendaji. Pengine kisiasa kazi nyingine angeweza kuzifanya, lakini kiutendaji… Kuna kazi za utendaji zina miiko yake ambayo kiwango cha elimu yake ilikuwa kidogo kina matatizo.
Raia Mwema: Sawa kulikuwa na makosa, lakini wewe ulimpataje pataje hadi akaukwaa ukatibu mkuu wa UWT?
Mama Sophia Simba: Huyu alikuwa mjumbe wa Baraza Kuu la UWT, ndicho kitu kimoja ambacho kilinifanya nimteue. Nimekuwa naye kwenye baraza tokea mwaka 2003. Mimi nimemjua Husna wakati nikigombea ujumbe wa Baraza Kuu. Kwa hiyo, nilipokwenda Arusha yeye ndiye aliyenisaidia kutafuta kura, siyo campaigner, lakini ndiyo  nilianza kumfahamu. Lakini nikamfahamu pia ndani ya vikao. Kwa hiyo nilimjua kwa hivyo.
Na kwa bahati mbaya sana, sikujaribu kuomba ushauri kwa mtu yeyote kutaka kujua habari zake zaidi. Ndiyo maana nasema nakiri makosa. Hakuna mtu aliyenishawishi  kuhusu yeye.
Raia Mwema: Eneo lile la Maria Hostel kulikuwa na mpango wa kujenga jengo kubwa kuondoa hali ya utegemezi  ya UWT ambayo umekwishaieleza. Je mpango huu bado upo?
Mama Sophia Simba: Mpango wa kuendeleza  kiwanja cha mtaa wa Lindi cha Maria Nyerere Hostel upo. Tumekuta mpaka na ramani zimeshachorwa, lakini sisi kamati yetu ya utekelezaji tunataka tujiridhishe, tutumie utaalamu zaidi. Lile jengo tulilolikuta pale linataka kujengwa lilikuwa haliendani na wakati.
Kwa hiyo, tulichokuwa tukingojea kwanza ni kupata Baraza la Wadhamini kwa sababu lile baraza la wadhamini lililopita la UWT, limemaliza muda wake. Sasa limepatikana jipya. Majuzi walikuwa na kikao chao cha kwanza cha Baraza la Wadhamini. Mwenyekiti wao ni Mzee Said El Maamry ambaye ni mwanasheria.
Tumelizindua baraza letu na sasa tunachotaka ni kupata hati ya pale Maria Nyerere. Maria Nyerere ilikuwa trusteeship ya Tanganyika Women, sasa hivi ni Tanzania Women. Jina limeshabadilishwa, na sasa tunangojea hati mpya. Tukishapata hati  tutaweza kuwekeza pale na kujenga kitu kizuri.
Raia Mwema: Kitu kizuri namna gani, kwani mnataka kujenga kitu gani?
Mama Sophia Simba: Tunataka tujenge office blocks na apartments, na sisi wenyewe tutakuwa na floor moja kwa ajili ya ofisi zetu. Tutakuwa na ukumbi wetu mkubwa wa mikutano, ni vitu kama hivyo.
Raia Mwema: Sasa hebu tuelezee kuhusu jengo jipya lile ambalo lilikuwa makao makuu. Nini mnachotarajia kupata kutoka hapo kwa sababu nalo lilileta minong’ono.
Mama Sophia Simba: Jengo jipya limekwisha, linangojea kufunguliwa. Lakini kwa kifupi sana niseme kwamba  jengo hilo jipya haliko chini ya management  ya UWT. Jengo jipya mkataba uliosainiwa ulikuwa ni mkataba wa UWT kulipwa certain amout of money kwa mwaka, hakuna percentage.
Mkataba uliosainiwa haukuwa mzuri. Kwa hiyo, sisi UWT hatuna eneo lolote. Sisi tutakuwa tunapata kodi ndogo tu. Kiwanja bado ni cha kwetu,  lakini lile jengo wale tumeingia nao mkataba wa miaka 33. Kwa hiyo they will run that thing kwa muda wa miaka 33. Sisi tutapata pesa kidogo.
Naona aibu hata kuzisema. Pesa tutakazozipata kwa mwaka hazisaidii hata kuwalipa mishahara makatibu wetu wote wa jumuiya lakini ndiyo hivyo tumejifunza kutokana na makosa.
Raia Mwema: Hivi hakuna namna ya kuweza kukutana na waliowekeza mkajadiliana nao kurekebisha huo mkataba?
Mama Sophia Simba: Mkataba uliopo ni binding, mkataba umeshaingiwa. Hiyo amount ambayo imefikiwa ni ambayo baada ya kuzungumza nao wakaongeza. Lakini sisi tunasema  tumeshajua pale yeye anakodisha kwa kiasi gani, basi tunataka tumwambie, basi, na sisi tuongezee kigogo, lakini hiyo ni subject ya mazungumzo ya sisi na yeye.
Raia Mwema: Bunge linalokwisha kwa sasa lina  wanawake wanaowakilisha majimbo 17. Je, mnao mkakati wowote wa kuweza kuwasaidia wanawake kuwa na ushindani wa kutosha na wanaume kwenye majimbo?
Mama Sophia Simba: UWT tayari tumeshatengeneza mkakati wetu wa kuhakikisha  wanawake wengi zaidi wanajitokeza kugombea kwenye majimbo. Majimbo siyo ya wanaume, majimbo ni yetu sote kwa hiyo kuna ziara  tumeshajipanga. Tutazunguka nchi nzima kuhakikisha wanawake wanajitokeza kugombea kwenye majimbo.
Tutahakikisha wanakwenda kupiga kura na kuhamasisha wanawake kuipigia kura CCM. Kwa hiyo tunakwenda kupiga ndege watatu kwa jiwe moja.
Naamini itakapofika mwaka 2015 wanawake watakaokwenda kwenye majimbo watakuwa wengi zaidi kwa sababu tumeshawawekea ukomo.
Wengine wamekuwa wabunge wa vitu maalumu kwa miaka 15 na wengine hivi sasa wameshaingia miaka 20, na bado hawajathubutu kugombea kwenye majimbo. Lakini kwa sasa mkakati tulionao ni  kuhakiksiha wanawake wengi wanajitokeza.
Raia Mwema: Halmashuri Kuu ya CCM imekubaliana na pendekezo la Baraza Kuu lako juu ya ukomo wa viti maalumu, lakini baadhi ya wabunge waliopita wa muda mrefu ambao wanadhani mlikuwa nao, wanadai mumewatosa. Hayo manung’uniko yao wewe unayajibuje?
Mama Sophia Simba: Nafurahi kupata nafasi hii nijibu hilo. Suala la ukomo wa viti maalumu halikuanza na mimi. Suala la ukomo wa vitu maalumu tumeanza kulizungumzia mwaka 1998 au 1999. Lakini kwa sababu sisi wenyewe tuko mle mle kwenye baraza Kuu, likaminywa.
Likarudi tena 2000 hadi  2005. Likazungumzwa tukiwa Arusha, likazungumzwa tukiwa Moshi. Watu wanalipooza kwa sababu kila binadamu tuna kitu kinaitwa choyo, unajifikiria wewe. Kwa hiyo, lile jambo ni jambo la siku nyingi. Hao wote wanaolalamika wanalijua, wanaiongopea jamii.
Suala la ukomo halikuletwa na Sophia Simba, suala la ukomo lililetwa na Baraza Kuu, isipokuwa kwenda kwenye NEC ndiyo limepelekwa safari hii.
Tatizo ni kwamba siku zile tulikuwa tunalizungumza kwenye Baraza Kuu  lakini halitoki kwenda NEC. Hivi sasa limekwenda kwenye NEC, na kwa bahati mbaya sana hao wanaolalamika wengine wameshakuwa wabunge miaka 15, wengine miaka 10.
Baraza Kuu lilisema kuwa nafasi za vitu maalumu ambazo ni za upendeleo, siyo wapendelewe hao hao tu kila siku. Ziliwekwa ili kumuwezesha mwanamke aweze kupambana na vile vigezo ambavyo tumesema vinatufanya wanawake tushindwe kuingia kwenye majimbo nao kwa sababu ya kuwapo mfumo dume.
Tumesema wanawake kwa sababu ya mfumo dume tuna aibu, hatuwezi kuongea kwenye majukwaa. Kwa sababu ya mfumo dume wanatutukana (eti) tunaogopa lakini tunasema pia kwamba mwanamke hana pesa za kwenda kwenye kampeni.
Sasa Baraza Kuu linasema huyu mwanamke au mama baada ya miaka kumi amekaa bungeni amekwenda kwenye mikutano, ana pesa anashindwa nini? Aende zake kwenye jimbo.
Hiyo  ndiyo concept tuliyozungumza kwamba tayari ile kazi ya upendeleo imeshafanya kazi. Imeshamtengeneza huyu mwanamke kuwa mwanasiasa.
Sisi shida yetu tunakata tuwe na wanawake wanasiasa wengi. Sasa hawa wanakuwa kama selfish, wanaona wao. Kuna mwingine anathubutu anasema ‘he  mimi kule kwangu nikitoka mimi, sina jimbo kule. Lakini kama huna jimbo wewe ukitoka mwanamke mwingine atachukua nafasi yako, kaa pembeni.
Kwa hiyo mimi wananionea kusema kwamba nimewacha kwenye mataa. Na hao kwanza waliokaa wanaosema kwamba nimewatosa, mimi UWT nimechaguliwa na wanawake wa Tanzania yote.
Na nimechaguliwa; hivyo siyo kazi yangu kulipa fadhila. Nimechaguliwa niwahudumie wanawake wa Tanzania na kwa kufanya hivyo, kwa kuweka ukomo baada ya miaka kumi tutaona majimbo mangapi wanawake watachukua.
Watajitokeza tu, sisi wanawake tunapenda sana kusukumwa. Sasa nenda hapa, sasa nenda pale. Mama Anna Abdallah aliweza mwaka 2005 kutusukuma. Aliniambia Sophia nenda Ilala, wewe fulani nenda pale.
Isitoshe siku hiyo kwenye Baraza Kuu ajenda ya kuwe na ukomo haikutoka kwenye kamati yangu ya utekelezaji, ilitoka pale pale barazani.
Hilo ndilo lililotokea kwa hiyo kina mama popote walipo naomba wasilichukulie hilo kama ni langu binafsi isipokuwa hofu ya wale wanaotaka waendelee na wasiotaka wenzao wengine wapata hizo nafasi ndiyo iliyofanya waende wakapeleke hadithi hizo.
Lakini siku moja wataniona shujaa. Kwa suala hili kulipeleka kwenye NEC  ilikuwa kazi kubwa, lakini imewezekana. Hata hivyo, NEC imesema lisianze mwaka 2010, litaanza mwaka 2015. Mwaka 2015 ni keshokutwa tu panapo na uhai. Kwa hiyo tutaona sura mpya zinaingia.