UFISADI MKUBWA KATIKA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA
Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
PILIKA zilikuwa nyingi wakati gari la binafsi linapofunga breki mbele ya eneo la mapokezi katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Mlango wa gari hili dogo unafunguliwa haraka ambapo watu kadhaa wanamshusha mgonjwa ambaye hajiwezi, Mahmoud Abdullah (45), na kumpandisha kwenye kitanda maalum ili kumwahisha kupata huduma za matibabu.

Kutokana na hali yake na kwa muda huu wa saa 10:20 jioni ambao watu ni wengi, Mahmoud analazimika kukimbizwa kwenye chumba cha daktari huku jamaa mwingine aliyekuja naye akishughulikia kujaza, kwa niaba yake, fomu maalum ya Bima ya Afya.
Kwa kuwa muuguzi anayeshughulikia wagonjwa ambao ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ameziona pilika hizo, hajisumbui kuichunguza na kuithibitisha kadi ya uanachama wa mfuko huo kama ni ya mgonjwa husika ama la, hivyo anatoa fomu na kuijaza mambo kadhaa ya msingi na kumpatia jamaa wa mgonjwa, anayeonekana kuchanganyikiwa kutokana na kuuguliwa.
Kitambulisho kinabaki hapo, ambapo jamaa huyu wa mgonjwa anaanza kuipitisha fomu kuanzia kwa daktari ambaye baada ya uchunguzi wa haraka anajaza kwenye fomu vipimo kadhaa vinavyotakiwa kuchukuliwa huku akimpatia huduma ya kwanza.
Fomu hiyo inazunguka kila mahali ambako kunatakiwa, na kila mhusika anajaza huduma iliyotolewa pamoja na gharama zake.
Mahmoud anaonekana kuwa na tatizo la shinikizo la damu, typhoid na malaria kali, lakini kutokana na mazingira ya hospitali yalivyo, hasa msongamano mkubwa wa wagonjwa, daktari anashauri ndugu wakamchukulie dawa na kurudi naye nyumbani.
“Hali yake itakaa sawa, nadhani shinikizo la damu ndilo limemfanya azidiwe, lakini kwa mazingira yalivyo, nashauri mchukulieni dawa na akazitumie nyumbani, hali itatengemaa,” daktari huyo anashauri.
Licha ya kupatiwa huduma ya kwanza huku daktari akishauri apumzike, Mahmoud bado hawezi hata kuketi, hivyo anatolewa nje kwa kitanda maalum cha wagonjwa hadi kwenye gari iliyomleta.
Jamaa wa mgonjwa huyo anakusanya dawa zote zilizoandikwa – japokuwa nyingine hazipatikani hapo na itawalazimu ndugu na jamaa kununua kwenye duka la dawa – na kuirejesha fomu kwa mhudumu wa Bima ya Afya ili isainiwe, kugongwa muhuri pamoja na kurejeshewa kitambulisho huku akipewa pole nyingi kwa kuuguza.
Hata hivyo, katika hali halisi, inaonekana kwamba kitambulisho kilichotumika kumtibu Mahmoud kupitia Bima ya Afya siyo chake, wala siyo cha jamaa aliyekuwa akihangaika kupita kila kona, bali ni cha Abdallah Uledi, rafiki wa Mahmoud, ambaye ameamua kutumia kadi yake kwa hila ili mgonjwa huyo apate matibabu.
Kwa haraka tu, huduma zote alizopatiwa Mahmoud zinakaribia Shs. 25,000 ambazo zinahusisha vipimo, ushauri (kuonana na daktari) pamoja na dawa.
Kiwango hicho kinaweza kuonekana kidogo, lakini kwa mujibu wa uchunguzi wa Fikra Pevu, ujanja uliofanywa na jamaa zake Mahmoud umekuwa ukifanyika na wananchi wengi kwani kadi moja tu ya Bima ya Afya ya NHIF inaweza kutibu hata watu 10, achilia mbali wale watano walioandikishwa kama wanufaika.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, kadi hizo za NHIF ambazo ni karatasi tu zilizotengenezwa kama vitambulisho vya kawaida, na hakuna utaratibu makini unaotumika kukagua na kujiridhisha kwamba kadi hizo zinatumiwa na walengwa pekee.
“Tunajitahidi kufuatilia na kukagua kadi kila wagonjwa wanapoletwa, lakini kusema ukweli zoezi ni gumu kwa sababu wapo watu wanaofanana kwa sura na wanaweza kutumia kadi hizo kwa kadiri wanavyoweza,” anasema muuguzi katika Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam, ambayo ina hadhi ya Hospitali ya Wilaya.
Muuguzi huyo ambaye anagoma kutaja jina lake, anabainisha kwamba, gharama zinazolipwa na Mfuko wa NHIF kutokana na matumizi hayo ya matibabu ndicho kitu cha uhakika, lakini kwamba imetumiwa na walengwa ama la ni jambo ambalo linaleta changamoto kubwa.
Uchunguzi wa Fikra Pevu unaonyesha kwamba, utaratibu wa kianalogia unaotumiwa na NHIF pamoja na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ndio unaoitia hasara kubwa serikali kwa kulipia matibabu hata kwa watu wasiohusika, tofauti na mifuko mingine ya Bima ya Afya, hususan ya binafsi.
Katika sekta binafsi, kwa mujibu wa uchunguzi huo, kadi zinazotumika kwa wateja zina alama maalum ambayo ni lazima isome kwenye mashine na kwa baadhi ya kampuni hizo, mteja lazima athibitishwe kwa alama za vidole.
Ingawa utaratibu wa kampuni nyingi za binafsi kama Jubilee, AAR, Strategis na nyinginezo zinahudumia zaidi watumishi wa taasisi na makampuni huku gharama zao zikiwa juu, lakini usalama unaonekana kuwa mkubwa kuliko bima zinazotolewa na taasisi za umma.
Inaelezwa kwamba, ufisadi huo unafahamika na watendaji wa mfuko huo, lakini kwa miaka kadhaa sasa hawajafanya lolote kudhibiti hali hiyo, jambo ambalo linaleta taswira kwamba wapo vigogo wa mfuko wanaojinufaisha pia.
Ingawa vitambulisho vya sasa vinadaiwa kutengenezwa kwa ubora (kama vya upigaji kura) na kuwekewa alama tambuzi, lakini vingi ambavyo vilitolewa kabla havina alama hizo, jambo ambalo wataalamu wa teknolojia wanasema haviwezi kuwemo kwenye kanzidata husika.
“Kwa muda mrefu kumekuwepo na wito wa wadau kuutaka mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa kuboresha vitambulisho vya wanachama wake ili kupambana na kughushi ambako kunaupotezea mapato mfuko na kuanza kutishia uwepo wake, lakini inaonekana wahusika wameweka pamba masikioni,” anasema Hassan Makange, mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Hassan anasema kwamba, watu wanatibiwa kwa vitambulisho visivyo vya kwao na pia mfumo mzima hauko makini katika kudhibiti malipo endelevu, jambo ambalo linaigharimu serikali mabilioni ya fedha.
“Kwa mfano, baadhi ya watu wanaoripotiwa kuwa walilazwa wakati siyo kweli, na wale wenye magonjwa ya kudumu kama Kansa, Kisukari, Shinikizo la Damu na magonjwa ya figo, gharama zinajazwa kubwa sana na zinapelekwa serikalini!” anabainisha Hassan.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Fikra Pevu, tafiti kadhaa zimefanyika za kuweka mfumo bora utakaowezesha kufanya utambuzi sahihi wa wanachama wanapokwenda kupata huduma katika hospitali na maduka ya dawa na kuwawezesha watoa huduma walipwe kwa mujibu wa huduma sahihi walizotoa.
Hata hivyo, jitihada hizo zinadaiwa kuvurugwa na vitendo vyenye viashiria vya ufisadi.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, tangu mwaka 2010 kumefanyika zaidi ya tafiti tano na watu kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya kupata uzoefu, lakini jitihada zote zinadaiwa kuvurugwa na watu wa kitengo cha Tehama katika mfuko huo pamoja na vigogo wake ambao inadaiwa huenda wananufaika na udhaifu huo.
Taarifa za ndani ya NHIF zinaeleza kwamba, badala ya kutekeleza tafiti zilizofanyika huko nyuma, uongozi wa mfuko huo uliwapa tena kazi watu binafsi ambao wanadaiwa kuja na andiko ambalo kwa kiasi kikubwa linaakisi tafiti za awali zilizotumia mamilioni ya fedha za umma.
Katika andiko hilo, inaelezwa kwamba utekelezaji wa kutengeneza vitambulisho bora vya Bima ya Afya utagharimu zaidi ya Shs. 50 bilioni ambazo NHIF wanatakiwa wazitoe kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).
“Mpango huu ulikuwa ukiasisiwa kwa siri na umakini mkubwa na pande tatu – Nida, NHIF na Wawezeshaji (majina yanahifadhiwa kwa sasa),” kinaeleza chanzo cha habari kutoka ndani ya NHIF.
Utengenezaji wa vitambulisho vipya vya NHIF unaofanywa na Nida unaelezwa kwenda kwa mwendu wa kinyonga ikilinganishwa na kasi iliyoonyeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo pamoja na udhaifu uliojitokeza ukisababishwa na mambo ya kisiasa, lakini walifanikiwa kutoa vitambulisho vya wapiga kura ndani ya miezi mitano.
Hata hivyo, wadau wanahofu kwamba, vitambulisho vya NHIF vinaweza kutolewa kwa watu wasio raia kama ilivyoshuhudiwa kwa vitambulisho vya uraia, ambapo inaelezwa kwamba Nida walitoa vitambulisho hivyo hata kwa wageni.
“Kama vitambulisho vya uraia vilitolewa mpaka kwa wageni, je, wakitoa vitambulisho vya NHIF kwa wasio raia si utakuwa mzigo mkubwa kwa serikali,” wanahoji baadhi ya wananchi.
Habari za ndani ya NHIF zinaeleza kwamba, suala la wateja kughushi vitambulisho (kutumia kwa watu wasiostahili) wanalijua na wanalifanyia kazi, ingawa haijulikani tatizo hilo litakoma lini.
“Watu wengi wamekuwa wakitumia kadi moja kwa familia nzima na  kusababisha hasara kubwa,” kinaeleza chanzo kimoja kutoka ndani ya mfuko huo.
Mwaka 2016, Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF, Raphael Mwamoto, akitoa mada kwenye kongamano la wahariri na wanahabari lililofanyika kwenye Chuo cha Ualimu Mtwara, alisema mfuko huo ungebadili utaratibu wa wategemezi wanne wa wanufaika wa bima hiyo baada ya kuwapo kwa wizi usiothimilika na matumizi mabaya vinavyotishia uhai wa mfuko.
Kutokana na hali hiyo, sasa wategemezi wa mnufaika wa bima yao watakuwa ni mwenza wa mhusika, watoto na wazazi wake, na siyo mtu mwingine yeyote.
“Kumekuwapo na wizi kwa kiwango kilichokithiri, usiothimilika. Licha ya wizi kumekuwapo na matumizi ya huduma yasiyo sahihi yaliyokithiri. Hali hii haiwezi kuvumilika tena kwa sababu yanatishia uhai wa mfuko,” alisema Mwamoto.
Alisema kumekuwapo na matumizi mabaya ya utegemezi kiasi kwamba baadhi ya wanufaika wanauza nafasi hizo, na hivyo kusababisha hasara.
Akitoa mfano wa ukubwa wa tatizo hilo, alisema endapo mtu asiye mnufaika wa bima ya afya, akaweza kutumia kadi ya mwanachama kwa ugonjwa wa figo, malipo yake ni kiasi cha Shs. 6 milioni kwa mwezi.
Ilitolewa mifano ya mtu aliyepewa kadi ya mnufaika na kutaka kuitumia kupata huduma za matibabu ya saratani na kama angefanikiwa, mfuko ungepata hasara ya Shs. 8 milioni na mwingine ni mwanachama aliyekuwa amefariki na kugundulika kutumia jina lisilo lake, na kama lisingebainika hilo, NHIF ingelipa Shs. 15 milioni.
Alisema wizi na matumizi hayo mabaya yanafanyika katika ngazi mbili; ngazi ya mwanachama kwa kadi yake kutumika vibaya kujipatia huduma au asiyestahili kutumia kadi hiyo ya mwanachama kupata huduma.
Hata hivyo, uchunguzi wa Fikra Pevu umebaini kwamba, ngazi nyingine ya wizi huo ni mtoa huduma kushiriki katika wizi na matumizi yasiyo sahihi kwa huduma kwa kudai malipo kwa huduma ambazo hakuzitoa au kuweka malipo makubwa tofauti na huduma iliyotolewa.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulianzishwa rasmi mwaka 2001 kama njia mojawapo ya serikali kutekeleza mpango wa afya kwa wote, ambao unaendana pia na Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2025 pamoja na Malengo Endelevu ya Dunia (SDG), hususan lengo namba tatu linahusu ‘afya njema na ustawi’.
NHIF inakwenda sambamba na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), ambao unatumiwa zaidi vijijini na unawafaa wananchi kwa matumizi ya kaya.
Mfuko huo unaendeshwa kwa fedha za wanachama, ambapo wapo waajiriwa wanaolipa kwa kukatwa 3% ya mishahara yao huku 3% nyingine ikichangwa na mwajiri, lakini wapo ambao wanalipa kwa uchangiaji maalum, ambapo kima cha chini ni karibu Shs. 79,000 kwa mwaka.
Wateja wa mfuko huo wanapata huduma katika Hospitali za taifa za rufaa, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za wilaya, teule, vituo vya afya pamoja na zahanati ambazo zimesajiliwa na mfuko huo, zikiwemo za umma na binafsi.
Aidha, baadhi ya maduka ya dawa na vituo vya kupimia au kuchunguza magonjwa (laboratories) vimesajiliwa kwenye utoaji huduma kwa wanachama wa mfuko huo.
Kwa sasa Serikali inajiandaa kufanya marekebisho ya Sheria ya Bima ya Afya kwa lengo la kuhakikisha kila kaya nchini inakuwa mwanachama wa mfuko huo na kutekeleza mpango wa afya kwa wote.
Utaratibu wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ni kwa kujiunga kama kaya, mtu binafsi au vikundi na kupatiwa kadi ya uanachama ambapo kila kaya inatakiwa kuchangia kiasi kitakachokubalika kwa mwaka.
Hadi kufikia Septemba 2016, NHIF imekuwa na ongezeko la wanufaika kwa asilimia 8 ambayo imefanya kuwa na jumla ya wanufaika 3,528,449 huku CHF ikiwa na ongezeko la asilimia 34 ambayo imefanya wanufaika wafikie 9,333,978.
Jumla ya wanufaika wa mifuko hiyo miwili hadi kipindi hicho ni 12,862,427, ambao wanaweza kutibiwa katika vituo takriban 6,439 vilivyosajiliwa na NHIF.

CHANZO: FIKRAPEVU